Du'aa Iombwe Wakati Unasujudu Ndani Ya Swalaah Au Usujudu Baada Ya Kumalizika Swalaah?

 

 

 

 

 

 

 

SWALI:

Asalam Aleikum

Tunaelekezwa mara nyingi sana unapo omba wakati unasujudu dua ina paa haraka maana wakati huo unakuwa karibu sana na Allah.  Suala langu ni hili  

Unaposujudu wakati umo ndani ya sala au usujudu wakati umeshamaliza sala? 

WABILLAH TAUFIQ  

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Du'aa ni ibada kama alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni ibada muhimu  sana kwani mja hudhihirisha Tawhiyd yake kwa kumuelekea Mola Muumba kwa mahitaji yake na sio kumuelekea kiumbe.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ))

((Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi Nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka )) [Al-Baqarah:186]

Ni kweli kwamba Du'aa katika sujuud hukubaliwa haraka kwa vile unakuwa karibu na Mola wako, kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo:

   قال صلى الله عليه وسلم :  (( أقرب ما يكون العبد من ربه وهو ساجد فأكثروا الدعاء )) رواه مسلم  

 

Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Mja huwa karibu kabisa na Mola wake anapokuwa anasujudu, kwa hiyo zidisheni Du'aa)) [Muslim]

Kuomba Du'aa katika kusujudu imekusudiwa wakati wowote mtu anaposujudu, na aghlabu ya kusujudu ni ndani ya Swalah, kwani baada ya Swalah hakuna kusujudu. Sijda za nje ya Swalah ni kama sijda ya Shukr au Sijda ya tilaawah (kusoma Qur-aan).  

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share