Zingatio: Je, Hatuoni Hayaa? (Hatustahi?)

 

Zingatio: Je, Hatuoni Hayaa? (Hatustahi?)

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika ya Binaadamu sote tupo kwenye hasara kubwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ametuumba sisi, halafu sisi tunaabudia yule asiyekuwa Yeye. Tumeruzukiwa kwa ukarimu wa Muumba, sisi binaadamu tunamshukuru asiyekuwa Yeye.

 

Rahmah Zake zinatuelekea sisi lakini sisi tunarejesha Kwake dhambi. Ilhali Rabb wetu hahitaji zawadi lakini Yeye Anatupatia zawadi nzuri na za kila aina lakini sisi tunarudisha Kwake zawadi ya dhambi, ila tunamkumbuka wakati wa msaada (shida) tu.

 

Yeyote atakayerudi Kwake, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atamkubali hata awe yupo umbali gani. Na yeyote Anayemkimbia, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamuelekea na kumuita. Yeyote anayeacha dhambi kwa ajili Yake, Allaah Atamlipa (baada ya kutubia) kwa malipo mema. Yeyote anayemridhisa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atampatia Radhi Zake. Yeyote anayethamini Wasia na Nguvu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa anayofanya, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakifanya chuma kipinde kwa ajili yake. Waja wema ni wale walokuwa wapo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) [Anayetaka kuwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ajikurubishe na kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)]. Yeyote anayemshukuru, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atampatia kheri nyingi, Yeyote Anayemtii Yeye. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atamnyanyua na kumpatia heshima zaidi. Yeyote anayemuasi, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaiachia milango Yake ya Rahmah wazi kwa ajili ya aliyeasi. Akirudi Kwake, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anampokea kwa mapenzi Yake. Kwani hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawapenda wanaorudi na kujitakasa kwa ajili Yake. Kama bado hajarudi, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamlea muasi huyu kwa mitihani migumu. Yeyote anayemjali Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuliko kiumbe chengine chochote, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atamfadhilisha dhidi ya kiumbe chochote.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatoa malipo ya kila jema mara kumi zaidi au mara mia saba hadi kufikia malipo yasiyo na hesabu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anahesabu kila baya kama ni moja mpaka unaporudi na kuomba msamaha. Hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamsamehe hata lile kosa moja. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anahesabu kila jema dogo na makosa makubwa. Rahmah Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni nyingi kuliko hamaki. Ustahamilivu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hauna kifani na Unaficha lawama. Msamaha wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni mkubwa kuliko adhabu.

 

Hakika Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mwingi wa Rahmah kwa waja wake kuliko mama kwa mwana.

 

Jee! Sisi Binaadamu hatuoni hayaa kutenda dhambi mbele ya Mwingi wa Rahmah?

 

 

 

 

Share