Nimemuingilia Mke Wangu Akiwa Katika Hedhi. Je, Ndio Sababu Ya Kukosa Uzazi/Watoto?

 

SWALI:

 

ASSALAAM ALEIKUM!

NASHUKURU KWA MTANDAO HUU AMBAO UNATUELIMISHA SISI WAISLAAM KWA MAIDHA MBALIMBALI YANAYOPATIKANA KATIKA MTANDAO HUU! NINA SWALI MUHIMU AMBALO NAPENDA KUPATA JIBU LAKE, KAMA KICHWA CHA HABARI KISEMAVYO!

KWA BAHATI MBAYA NIMESHAWAHI KUMUINGILIA MKE WANGU AKIWA KATIKA SIKU ZAKE KAMA MARA MBILI KATIKA NYAKATI TOFAUTI, TOFAUTI YA MUDA NI KAMA MIAKA MIWILI IMEPISHANA,

NA KUNA MARDHI YANAYOPATIKANA KUTOKANA NA KITENDO HICHO AMBACHO LEO NASIKILIZA MAWAIDHA YA SHEIKH UTHMAN MAALIM KATIKA TAFSIRI YA QUR’AN SURAT AL BAQAR (220-223) NIKASIKIA MADHARA YA KITENDO HICHO.

NA MIMI NA MKE WANGU SASA TUNATAFUTA MTOTO KARIBU MWAKA WA TATU BILA MAFANIKIO TANGU TUOWANE, TUMEHANGAIKA SANA HOSPITALI NA KWA MASHEIKH KUTOOMBEA LAKINI HAKUNA MAFANIKIO, JE INAWEZEKANA KUWA HICHO KITENDO TULICHOKIFANYA KIKAWA SABABU? JE JINSI GANI TUNAWEZA KUFANYA ILI TUBAARIKIWE KUPATA WATOTO? JE KUNA DAWA YA KUWEZA KUJITIBU MARADHI HAYO

TUNAOMBA JIBU USTAADH ILI TUPATE FURAHA KATIKA NDOA YETU.

TUNATUNGULIZA SHUKHRAN ZETU KWA MSAADA WOWOTE UTAKAO TUPATIA NA INSHA-ALLAH MWENYEZI MUNGU ATAKUBARIKI

WAHADHA SALAAM

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa ndugu yetu kwa swali lako kuhusu suala hilo lililo na kichwa cha habari hapo juu. Maelezo yako hayajakamilika na hivyo kuwa vigumu kukusaidia kwa njia bora zaidi kama inavyotakiwa.

 

Kitendo cha kumuingilia mkeo katika ada yake kimetazwa katika Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa uwazi kabisa. Hivyo, machimbuko hayo mawili hayajaacha upenyo wowote. Huenda likaja swali kuwa, lakini mimi sikuweza kujizuilia sasa itakuwaje au nifanyeje? Hiyo si hoja kwani Uislamu umekupatia fursa ya kuongeza mke wa pili. Ikiwa huwezi hilo basi unaweza kucheza cheza naye akiwa amejifunga sehemu ya utupu wake na mkafanya yote isipokuwa jimai. Kwa hakika kufanya hivyo kunatoa matamanio kwa kiasi kikubwa katika kipindi hicho cha ada yake. Ukiwa unaona huwezi kujizuilia katika muda huo mfupi wa ada yake sijui ikiwa atakaa kwa muda mrefu zaidi baada ya kuzaa itakuwaje. Yapo mengi ambayo unaweza kufanya ya kukutimizia haja yako ya kiume bila ya kufanya jimai.

Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuelezea kuwa kuwaingilia wake zenu katika ada zao ni ugonjwa. Anasema Aliyetukuka: “Na wanakuuliza kuhusu hedhi; waambie huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi zao. Wala msiwakaribie mpaka watahirike” (2: 222). Maana ya maneno mume asimkaribie mkewe katika Aayah hii, sio kujitenga kabisa naye bali maana yake halisi ni kuwa wanafaa wale nao, wakae nao, walale pamoja kwenye kitanda kimoja na hata kucheza cheza nao. Jambo linalokatazwa ni kujamiiana nao (kufanya tendo la ndoa).

 

Allaah Aliyetukuka hapa Anasema kuwa wanawake katika damu zao ni adhaa kumanisha uchafu na pia ugonjwa. Tunaelewa kuwa damu ndio chombo kikuu katika hayawani na pia mwanadamu kinachobeba virusi, vidudu, viini vya maradhi, bakteria na kemikali tofauti ambazo nyengine ni sumu mwilini. Ni kwa ajili ya kuchunga maslahi yetu ya kiafya ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akatukataza kunywa damu. Sasa katika kumuingilia mkeo wakati wa hedhi huenda ikawa damu nayo inatoka japo kidogo na ikaingia katika utupu wako na hivyo kukuathiri kidogo au vibaya sana.

 

Ikiwa umeathiriwa kwa kiasi chochote kile madaktari katika hospitali ulizokwenda wangekuwa wamekueleza hilo. Ni ajabu kuwa katika swali lako hukutueleza matokeo ya hospitali ili tuweze kukusaidia. Hatujui hospitalini wewe na mkeo mlipimwa nini na mkambiwa nini? Kitu cha kwanza ambacho unatakiwa wewe na mkeo mfanye ni kupima nani mwenye tatizo la uzazi. Je, wewe ndiye mwenye tatizo la uzazi au ni mkeo? Katika hilo hakuna aibu ukipata matokeo kuwa wewe si mzazi na ikajulikana shida uliyonayo ni kadhaa. Sababu ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ndiye mpaji watu watoto Anavyotaka kwa hekima Yake bila ya kuulizwa na yeyote yule. Anasema (Subhaanahu wa Ta‘ala):

“Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allaah; Anaumba Apendavyo, Anampa Amtakaye watoto wa kike na Anampa Amtakaye watoto wa kiume. Au Huwachanganyia watoto wa kiume na wa kike, na Humfanya Amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi, Muweza” (42: 49- 50).

Tatizo la kutozaa wakati mwengine inakuwa ni maradhi yanayotibika au inawezekana kuwa wakati mwingi mnakutana katika tendo la ndoa wakati yai la mke halijafika sehemu linapotakiwa liwepo au limeanza kuvunjwa vunjwa. Upo wakati wa hatari ambapo mnapokutana na mkeo uwezekano mkubwa wa mkeo kushika mimba na upo wakati ambao ni salama kwa yeye kutoshika mimba. Daktari au hata nurse anaweza kukusaidia katika hili. Ikiwa wewe uko sawa na mkeo pia yu hali kadhalika basi mkeo anatakiwa ajue masiku yake na mpate usaidizi wa daktari kama tulivyoeleza. Mkishajua jadwali hiyo munaweza kuitumia na huku mnamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Awaruzuku mtoto wa kheri na mwema.

Ama kuhusu hicho kitendo ulichofanya ni haramu na inatakiwa utake msamaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), umuombe maghfira na uweke azma ya kweli kuwa hutarudia tena kosa hilo katika uhai wako. Kuhakikisha hilo unatakiwa umwambie mkeo asikukubalie kabisa akiwa katika ada yake wewe kumuingilia. Hilo kwa hakika si kosa ambalo linaweza kuwakosesha mtoto/ watoto. Hilo linaweza kuwa ni sababu ya kuzorota afya zenu au huwa ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kupima subira yenu na kushikamana kwenu na Dini hata baada ya kukosa kitu mnachokitamani sana.

Ama kile ambacho mnatakiwa mfanye ili mbarikiwe kupata mtoto ni kuleta Istighfaar kwa wingi (kumtaka msamaha Allaah kwa kusema AstaghfiruLlaah). Hii ni kwa mujibu wa Qur-aan inayosema: “Nikawaambia: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na Atakupeni mali na watoto, na Atakupeni mabustani, na Atakufanyieni mito” (71: 10 – 12).

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akusaidieni Akupeni mtoto mwema mwenye Dini awe ni pozo la mioyo yenu.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share