Unapohamia Katika Nyumba, Unatakiwa Usome Au Kufanya Chochote

SWALI:

Asalam Aleykum
Mimi nimejaaliwa kujenga nyumba na nilipokuwa nikianza msingi tu nikachinja na kutoa sadaka. Baada ya nyumba kwisha nimekuwa nikipata ushauri kwa ndugu jamaa na marafiki kuwa niite watu tufanye kisomo kwa ajili ya kuizingua nyumba. Naomba kuuliza nini hasa ninatakiwa kufanya??

 
Wabillah Tawfiq -  


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Mas-ala ya kuchinja inategemea ulichinja kwa nia gani. Ikiwa umechinja pia kwa ajili ya furaha na kutoa sadaka basi imefaa. Lakini ikiwa umefanya kama wafanyao wengi kuchinja kwa ajili ya kumwaga damu kwa itikadi kwamba damu hiyo itakuwa ni kinga ya majini au uovu wowote katika nyumba, jambo hilo litakua ni la shirki.

Kutoa sadaka kwa aina yoyote ni jambo linalopendekezeka na njia moja wapo ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Unaweza pia kumshukuru kwa kusema du'aa ifautayo kwa vile ni jambo la kukupendesha kama alivyotufunza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):   

 كَانَ النبي صلى الله عليه وسلم  إِذَا رَأَى مَا يَسُرُّهُ قَالَ:  (( الحَمدُ لِلَّهِ الذِي بِنِعمَتِهِ تَتِمُّ الصَّالِحَاتُ))  رواه ابن ماجه   وقال النووي : إسناده جيد  

 Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapoona jambo la kumpendesha akisema: ((AlhamduliLLaahi-lladhiy Bi-Ni'matihi Tattimus-Swaalihaat [Sifa njema ni za Allaah Ambaye kwa neema Yake yanatimia mambo mema])) [Ibn Maajah na An-Nawawy kasema isnaad yake ni nzuri]

Ama kuita watu kukusanyika kwa ajili ya kisomo ni jambo lisilokuwa na dalili katika Dini yetu. Muislamu anapasa kutambua kwamba kila aina ya ibada anayotaka kuifanya lazima apate dalili kutoka mafunzo ya Dini yetu, au sivyo itakuwa ni jambo la kuzushwa na juu ya hivyo iwe ni kupoteza muda na gharama wakati ibada yenyewe au du'aa yenyewe haina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani tumeonywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika Dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

Soma Swali na Jibu katika kiungo kifuatacho upate ufafanuzi wa mas-ala haya na upate manufaa zaidi:

Kualika Watu Kusoma Qur-aan Kuomba Haja

Hakuna du'aa khaswa iliyotajwa kwa ajili ya nyumba mpya lakini kuna mafunzo mbali mbali ya kusoma Qur-aan na du'aa zinazohusiana na kinga ya nyumba kama ifuatavyo:

Unapoingia katika nyumba useme du'aa ifuatayo iliyoko katika kitabu cha Hiswnul-Muslim:

     ((بِسْـمِ اللهِ وَلَجْنـا، وَبِسْـمِ اللهِ خَـرَجْنـاَ، وَعَلـى رَبِّنـا تَوَكّلْـناَ))

BismiLLaahi waljanaa wa BismiLLaahi kharajnaa wa 'alaa Rabbinaa tawakkalnaa.

((Kwa jina la Allaah, tunaingia, na kwa jina la Allaah tunatoka, na Mola wetu tunamtegemea))

Kisha unatoa salamu kama tulivyofunzwa katika Qur-aan:

((فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَى أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً))

((Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayotoka kwa Allaah, yenye baraka na mema..)) [An-Nuur: 61]

Hivyo ni kinga kwani:

 عن جابر بن عبد الله أنه سمع النبي صلى الله عليه وسلم يقول : (( إِذَا دَخَلَ الرَّجُلُ بَيتَهٌ فَذَكَرَ اللهَ عِندَ دُخُولِهِ وَعِندَ طَعَامِهِ ، قَالَ الشََّيطَانُ : لَا مَبِيتَ لَكُم وَلَا عَشَاءَ ، وَإِذَا دَخَلَ فَلَم يَذكُرِ اللهَ عِندَ دُخُولِهِ ، قَالَ الشَّيطَانُ : أَدرَكتُمُ المَبِيتَ ، وَإِذَا لَم يَذكُرِ اللهَ عِندَ طَعَامِهِ قَالَ : أَدرَكتُمُ المَبِيتَ وَالعَشَاءَ )) رواه مسلم

Imetoka kwa Jaabir bin 'Abdillaahi kwamba kamsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Anapoingia mtu nyumbani kwake au anapokula akamtaja Allaah, Shaytwaan husema (kujiambia mwenyewe): 'Huna mahali pa kukaa wala chakula'. Lakini akiingia bila ya kumtaja Allaah, Shaytwaan husema (kujiambia mwenyewe): 'Umepata mahali pa kukaa'. Na asipomtaja Allaah wakati wa kula, husema:(kujiambia mwenyewe)  Umepata mahali pa kukaa na kula')) [Muslim]

 

Kusoma Suratul Baqarah:

   عن ‏ ‏أبي هريرة ‏ رضي الله عنه ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال‏ : ((لا تجعلوا بيوتكم مقابر إن الشيطان ينفر من البيت الذي تقرأ فيه سورة ‏ ‏البقرة))   مسلم

 

Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba  Mtume (Swallah Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msifanye nyumba zenu makaburi, hakika Shaytwaan anakimbia nyumba ambayo inasomwa Suratul-Baqarah)) [Muslim]

Du'aa ya kujikinga na kila shari ya Viumbe:

عن خولة بنت حكيم أنها سمعت النبي صلى الله عليه وسلم يقول: من نزل منزلاً ثم قال: أعوذ بكلمات الله التامات من شر ما خلق لم يضره شيء حتى يرحل من منزله ذلك)) مسلم

Kutoka kwa Khawlat bint Hakiym kwamba kamsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aksiema: ((Atakayeteremka katika kituo (au makazi) kisha akasema: 'Auwdhu bikalimati-LLaahit-taammati min sharri maa Khalaq' [Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia na shari Alichokiumba], hakuna kitakachomdhuru hadi atakapoondoka katika kituo (au makazi) hicho)) [Muslim]

Vile vile kauli na mafunzo kutoka kwa Maulamaa wetu kuhusu kuhamia nyumba mpya:

Ibn 'Uthaymin: Alipoulizwa kuhusu la kusema mtu anapoingia katika nyumba mpya asema nini mojawapo ya du'aa aliyopendekeza isomwe ni:

  ((رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ))

Rabbi Anziliniy Munzalam-Mubaarakan wa Anta Khayrul-Munziliyn

((Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji)) [Al-Muuminuun: 29]

 

Ibnul-Qayyim katika Al-Waabil As-Swayyib (155-156) kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema katika kisa cha watu wawili:

 ((وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاء اللَّهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّهِ إِن تُرَنِ أَنَا أَقَلَّ مِنكَ مَالًا وَوَلَدًا))                      

((Na lau kuwa ulipoingia kitaluni kwako ungelisema: Mashaa-Allaah! Alitakalo Allaah huwa! Hapana nguvu ila kwa Allaah. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe)) [Al-Kahf: 39]

Hivyo anayeingia katika bustani yake au nyumbani kwake au akaona chochote cha kumpendezesha katika mali yake au familia yake asiache kusema maneno hayo (Maa Shaa-Allaah Laa hawla wa Quwwata Illa BiLLaah) kwani akisema hivyo hakuna ovu litakalomfika kwa kile alichokihusudu.

Shaykh Ibn Baaz katika Majmuu' Al Fataawa (23/413): Kwamba kwa kusoma Suratul Baqarah ima mwenyewe mtu kuisoma au kwa kuweka isomwe katika kaseti au CD basi kilichotajwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitapatikana yaani shaytwaan kukimbia nyumba [inayosomwa Suratul Baqarah]   

Tunatumai kwa mafunzo yote hayo utakapoyatimiza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakulinda Insha Allaah kwa kila ovu na Akutilie Baraka na Kheri nyingi katika nyumba yako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share