Kufanya Kazi Ya Upishi Kwa Wasio Waislam Katika Ramadhaan

SWALI:

 

Asalamu Alaikum warahmatullahi wabarakatu

ndugu zangu waislamu bismilliahi rahmani rahim ningependa kuuliza kama inasihi mwislamu afanye kazi ya kijakazi katika nyumba ambayo si waislamu katika mwezi wa ramadhani na awapikie chakula .naomba munijibu kwa haraka kama inawezekana.. Mungu awajaze kheri,waalaikum salam warahmatullahi wabarakatu

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hatuoni kama kuna tatizo kufanya kazi za nyumba za wasio Waislamu madamu maagano yametimia ya kufanya kazi na kupatikana mshahara. Hayo hayakataliwi na Uislam maadam makubaliano yatatekelezwa na haki yako itapatikana.

 

Lakini ikiwa kupika huko, au mapishi unayofanya yanahusisha vyakula vya haramu au nyama zisizo halali Muislam kuzila kama wanyama walioharamishwa kuliwa mfano wa nguruwe, mbwa n.k., au kuna mchanganyiko wa pombe n.k. basi kazi hiyo itakuwa haifai kisheria na unapaswa uepukane nayo haraka sana. Na ni vyema kuwekeana mkataba tangu mwanzo kuwa hakutakuwepo na vitu hivyo katika kazi yako ili daima uwe katika usalama wa Dini yako na pia kuepukana na mshtukizo wa kuingizwa katika balaa hilo baada ya kuanza kazi hiyo.    

 

Na hili linahusu siku zote; ziwe za Ramadhaan na zisizo za Ramadhaan.

Na ikiwa hakuna kupika vitu vya haramu kama nguruwe na nyama haramu zilizokatazwa kuliwa au mapishi yenye pombe n.k. basi hakuna ubaya kufanya kazi kama hiyo.

 

Ama ukiwa unakusudia kuwapikia watu wasiofunga kama hao wasio Waislam na hali wewe umefunga, hilo halikatazwi kabisa maadam utatekeleza masharti yaliyotajwa hapo juu. Na si wasio Waislam tu hakukatazwi kuwapikia ikiwa wewe umefunga, bali hata Waislam ambao hawajafunga hukatazwi kuwapikia mwezi wa Ramadhaan. Kuna Waislam wagonjwa, watoto, wazee, kina mama wenye mimba au wanyonyeshao ambao hali zao haziwaruhusu kufunga kutokana na madhara ya afya zao na watoto, pia wasafiri n.k. wote hao wanatakiwa wapate chakula mwezi wa Ramadhaan na bila shaka kuna wa kuwapikia wao.

 

Vilevile kwa nyongeza, ikiwa una Mkahawa wako, au unafanya kazi katika mkahawa (imezoeleka kuitwa Hoteli japokuwa Hoteli ina maana pana zaidi ya sehemu ya chakula tu), Wanachuoni wanaonelea ni bora kuufunga katika mchana wa Ramadhaan na kufungua jioni kwa ajili ya kuuza Futari, kwani kufungua mchana ni katika kusaidiana katika madhambi kwa kuwa utakuwa unawalisha wale wasiofunga na kutouadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhaan.

 

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share