Fidia Ya Kutokufunga Ramadhwaan Zilizopita Kwa Sababu Ya Kushika Mimba

 

Nini Fidia Ya Kutokufunga Ramadhwaan Zilizopita Kwa Sababu Ya Kushika Mimba?

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Assalamu allaikum wa rahmatullulahi

Nina sikitiko sana, nimepitwa na ramadhani mbili mufililizo bila kufunga kwa juu nimekuwa na mimba ya watoto wangu (two following years I  had two children) je sikufanya fidiya, aw kulipa hizo siku zote 60. Nimewawuliza mashehe, nimejibiwa kwamba kwa vile nimekuwa na mimba si mana kulipa hizo siku hawo kulipa fidiya. Je ni kweli hawo? Nasikitika sana kwa hili swali.

Nawatakia Ramadhan Mubaaraka Waislamu wote.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Shariy’a inataka yeyote anayekula katika mwezi wa Ramadhwaan kwa sababu inayokubalika ni wajibu kwake kulipa siku alizokula.   Kwa mfano mtu kuwa safarini, kunyonyesha na kubeba mimba (ikiwa atahofia afya yake au ya mtoto wake), ugonjwa, wanawake katika damu ya mwezi au baada ya kuzaa, na kadhalika.  Hii ni kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala):

 

أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٨٤﴾

(Swiyaam ni) Siku za kuhesabika. Lakini atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika, watoe fidia; kulisha masikini. Na atakayefanya kwa khiari yake jema lolote, basi hilo ni bora kwake. Na mkifunga Swiyaam ni bora kwenu mkiwa mnajua. [Al-Baqarah 2: 184].

 

Inatakiwa kufanya haraka kulipa Swiyaam za  Ramadhwaan lakini mtu akichelewa na kuzilipa kabla ya Ramadhwaan nyengine kuingia hapana neno. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa): “Nilikuwa nina deni la Ramadhwaan, sikuweza kulipa hadi ilipofika mwezi wa Sha‘baan  kwa sababu ya kumhudumikia Rasuli wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Hivyo, ikiwa Sha‘baan imeingia ni wajibu kwa anayedaiwa funga ya Ramadhwaan kulipa siku zote kabla Ramadhwaan mpya kuingia.

 

Mtu akichelewa kulipa siku alizokosa mpaka Ramadhwaan nyingine kuingia itampasa afunge Ramadhwaan hii ya sasa na kulipa siku anazodaiwa baada yake. Ikiwa kuchelewa huko kulipa ni kwa sababu ya udhru wa kishariy'ah kama alivyo dada yetu muulizaji swali, kwake itakuwa ni kulipa hiyo miezi miwili peke yake punde tu udhru wa mimba utakapoondoka. 

 

Na ikiwa mtu hakulipa deni pasi na udhuru wowote wa kishariy'ah anawajibika kulipa siku alizokosa za Ramadhwaan zilizopita pamoja na kulisha masikini kwa kila siku aliyokosa (yaani nusu swaa‘ kama kilo moja na robo au nusu).

 

Bonyeza hapa upate majibu ya maswali yanayohusu kulipa Swawm na fidia:

 

Fataawaa: Kulipa Swawm Na Kafara

 

Fataawaa: Kujuzu Au Kubatilika Swawm, Kulipa Na Kafaara: Hedhi, Mja Mzito, Kunyonyesha, Nifaas

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share