Makosa Yafanywayo Na Wenye Swawm Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Makosa Yafanywayo Na Wenye Swawm Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

  

Yafuatayo ni makosa ambayo yameonekana yakitendeka katika mwezi wa Ramadhwaan ima wanapokuwa Waislamu katika Swawm au baada ya kufuturu na katika Swalah za Qiyaamul-Layl. Hivyo inapasa tuyazingatie na kujiepusha nayo ili tubakie katika usalama wa Swawm zetu, Swalah zetu na mengine yote yanayohusu mwezi huu mtukufu:

  

1. Kutia Niyyah Kwa Kutamka:

 

Baadhi wanaamini kuwa niyyah usipoitamka basi haijawa niyyah. Na pia huwafunza watoto kutamka maneno ya kutia niyyah, au kuwaamrisha wasikose kwenda kunuizwa Msikitini na mashekhe. Itambulike kuwa niyyah mahali pake ni moyoni na kutamka ni uzushi. 

  

2. Kufunga bila kuswali:

 

Baadhi ya watu wanafunga bila ya kuswali au kutimiza Swalah ipasavyo. Watu kama hawa Swawm zao hazifai kwani Swalah ni nguzo ya Dini ya Kiislamu.

 

3. Kudhani kwamba Swalah ya Taraawiyh inaanzwa siku ya kwanza ya Ramadhwaan:

Hali inaanza usiku ule unaoandama mwezi. Sunnah ni Waislamu waanze kuswali usiku huo na si baada ya kufunga siku ya kwanza.

 

4. Kuchelewa Kufuturu/Kufutari:

Baadhi ya watu husubiri hadi adhana imalizike na wengine husubiri hadi kiza kiingie na hali tumehimizwa tukimbilie kufuturu. Matokeo yake ni kukiuka Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia huenda kufanya hivyo wakachelewa Swalah ya Magharibi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

 لا تزال أمتي بخير ما عجَّلوا الإفطار - رواه الإمام أحمد

Ummah wangu utabakia katika khayr watakapokimbilia kufuturu. [Imaam Ahmad]

  

5. Kuomba Du'aa Zisizo Sahihi Wakati Wa Kufuturu:

Wengi wameizoea du’aa hii na kuisoma wakati wa kuanza kufuturu, ingawa ni du’aa yenye mapokezi dhaifu yasiyo sahihi:

 اللَّهمَّ! لك صُمتُ، وعلى رِزقك أفطرتُ

Allaahumma Laka Swumtu wa 'alaa Rizqika aftwartu.

 

Wanachuoni wa Hadiyth wanaeleza kuwa hakuna du’aa yoyote iliyothibiti wakati wa kufuturu.

  

7. Kufuturu Kwa Vitu Vya Haraam Kama Kuvuta Sigara N.k.

Wanakosa kutambua kwamba hii fursa kubwa kwa waliozoea kuvuta sigara kuacha moja kwa moja kuanzia mwezi wa Ramadhwaan, kwani ikiwa wameweza kufunga siku nzima na kujizuia kuvuta, vipi washindwe kujizuia na usiku?

  

8. Kula Futari Kupita Kiasi:

Utakuta mtu akifuturu huwa anafanya kisasi, anataka ale kulipiza ile njaa ya siku nzima, matokeo yake anashiba kiasi kushindwa hata kwenda kuswali Taraawiyh.

  

9. Kukithirisha Michezo na Upuuzi:

Utakuta watu wakati uingiapo mwezi wa Ramadhwaan, ndio wanaanza kutoa ile michezo waliyoiweka pembeni mwaka mzima, au kwenda kununua michezo mipya kama karata, carrum (keram), drafti, domino (dhumna) n.k. wakicheza mchana kutwa ili kupitisha muda uende haraka. Na kisha ifikapo usiku badala ya kwenda kuswali Taraawiyh.

Wanakesha kwa kuangalia televisheni, filamu na mipira.

 

Na wengine wakiyaambatanisha hayo kwa kula mirungi na kuvuta sigara. Hayo ni mambo ya haramu na yenye kuwapotezea fadhila na ujira upatikanao katika Ramadhwaan, wakati ambapo wangeutumia mchana wao kuchuma kwa kusoma Qur-aan sana na kuhudhuria darsa za Dini au kusoma vitabu vya Dini, kusikiliza mawaidha, Qur-aan n.k. Na ifikapo jioni wangeutumia muda wao kusimamisha Swalah za usiku (Taraawiyh), na pia kupumzika ili waweze kuwahi Swalah ya Alfajiri. Gumzo lisilokuwa katika mas-ala ya Dini jambo lililochukizwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama usimulizi ulivyopokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas-uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

 عن عبد الله بن مسعود: ((لا سمر إلا لمصل أو مسافر))  السلسلة الصحيحة - المحدث: الألباني 

  Hakuna kupiga gumzo la usiku isipokuwa kwa mwenye kuswali au msafiri. [As-Silsilat Asw-Swahiyhah – Al-Muhaddith Al-Albaaniy]

 

وعن أبي برزة "أن رسول الله صلى الله عليه وسلم كان يكره النوم قبل العشاء والحديث بعدها" رواه البخاري، ومسلم  

Na kutoka kwa Abu Barzah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichukia kulala kabla ya 'Ishaa na gumzo baada yake) [Al-Bukhaariy na Muslim]

  

10. Kusengenya, Kudanganya, Kupiga Porojo Na Kukaa Mabarazani Kupoteza Wakati:

Wanajisahau wengi wetu kwa kupiga soga zisizo na maana na pia kusema wenzao, kutukana, kulaani na kuongea mambo ya uongo n.k. Pia wengi wetu wakifunga huwa na khasira sana. Huko kunapelekea mtu kupoteza ujira wa funga yake na pia hata kuibatilisha (kwa maoni ya ‘Ulamaa wengine), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: Ambaye hatoacha maneno ya uongo na matendo yake, basi ajue kwamba Allaah hana haja ya yeye kuacha chakula chake na kinywaji chake. [ameisimulia Imaam al-Bukhaariy]

  

11. Kuwachukua watoto wadogo Misikitini ambao wanafanya fujo na kusababisha kushawishi Imaam na Maamuumiyn (wanaoswali) washindwe kupata khushuu (unyenyekevu) katika Swalah.

Kuwazoesha watoto Msikiti ni jambo zuri kabisa, lakini panapoonekana kuna matatizo kama hayo, basi ni bora kuwaepusha ili wasiharibu Swalah za wengi.

  

12. Kutokukamalisha Swalah ya Taraawiyh na Imaam ili kupata fadhila za Qiyaamul-Layl kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ((مَنْ قَامَ مَعَ الإِمَامِ حَتَّى يَنْصَرِفَ كَتَبَ اللَّهُ لَهُ قِيَامَ لَيْلَةٍ)) رواه الترمذي وصححه الألباني في صحيح الترمذي

 Atakayesimama (kuswali) na Imaam hadi amalize ataandikiwa (fadhila za) Qiyaamul-Layl. [Imesimuliwa na at-Tirmidhiy na kaipa daraja ya Swahiyh al-Albaaniy katika Swahiyh at-Tirmidhiy]

 

13. Kushika Mus-haf na Kumfuatiliza Imaam Anaposwalisha:

Kufanya hivyo, kunamkosesha mtu kuipata Sunnah ya kufunga mikono yake na pia kupoteza fadhila za kuisikiliza Qur-aan kutoka kwa Imaam ambayo tumeamrishwa kuisikiliza inaposomwa, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا قُرِىءَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُواْ لَهُ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [A'raaf:204]

  

14. Kusoma Tasbiyh Fulani Kila Baada Ya Rakaa Nne Ya Mapumziko:

Hakuna dalili ya kufanya hivyo. Lililothibiti ni kusoma tasbiyh mwisho kabisa unapomaliza Swalah ya Witr kwa kusema mara tatu:

سُبْحَانَ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ

Subhaanal-Malikul-Qudduus   

 

(Kisha ya tatu utaivuta na kuisema kwa sauti ya juu)

 

15. Kuharakisha kula Daku:

Utakuta baadhi ya watu wanawahisha Daku na kuila saa sita za usiku au hata baada tu ya Taraawiyh, ima kwa kutaka walale moja kwa moja hadi Alfajiri au kwa sababu ya uvivu wa kuamka kwa ajili ya Daku. Kufanya hivyo ni makosa kwa sababu kunakwenda kinyume na mafunzo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pia kunapelekea kuikosa ile baraka iliyojaaliwa kwenye Daku. Na Daku si lazima kula mlo mzito, japo tende au maji yatosha. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

((عجلوا الإفطار، وأخروا السحور)) صحيح الجامع - صححه الآلباني

Harakisheni kufuturu na chelewesheni daku [Swahiyh al-Jaami' na kaipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

 

16. Kudhani Mwisho Wa Kula Daku Ni Dakika Kumi Kabla Ya Adhana Ya Alfajiri:

Hivyo mtu akichelewa kula daku na ikawa karibu na dakika chache tu kabla ya Alfajiri hujinyima daku kwa khofu kuwa Swawm yake itabatilika. Wengine wameweka mipaka ya dakika kumi, hivyo si sawa. Mtu anaweza kula daku hadi karibu na Alfajiri hata kunapoadhiniwa. Na pindi Muadhini akiadhini ndipo unapoanza kufunga na Swawm yako inasihi. Na hata Muadhini akiadhini na kama una tonge au fundo la maji mdomoni usiliteme, kamilisha kulimeza kisha ndio uanze kufunga. Haya yamethibiti katika Sunnah kama inavyoonyesha Hadiyth ifuatayo:

 

Kutoka kwa Sufyaan bin ‘Uyaynah kutoka Az-Zuhriy, naye kutoka kwa Saalim naye kutoka kwa baba yake, kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Hakika Bilaal anaadhini usiku (adhana ya mwanzo), basi kuleni na mnywe hadi aadhini Ibn Ummi Maktuwm)) [At-Tirmidhiy]

  

17. Kudhani Kwamba Mtu Anapoamka Na Janaba Huwa Swawm Yake Haifai:

Dhana hiyo si sahihi, bali sahihi ni kuwa mtu anaweza kujitwaharisha hata baada ya kuingia Alfajiri mradi tu aiwahi Swalah ya Alfajiri isije kumpita. Na Swawm yake ni sahihi.

  

18. Kufunga ukiwa safarini:

Walioko safarini kujikalifisha na kujitia katika mashaka ya kufunga na kuacha kuchukua rukhsa iliyotolewa kufuturu; si jambo jema kufanya hivyo kama ilivyo dalili ya Hadiyth:

 

عن جابر بن عبد الله أن رسول الله صلى الله عليه وسلم رأى رجلا يظلل عليه والزحام عليه فقال: ((لَيْسَ مِنَ الْبِرِّ الصِّيَامُ فِي السَّفرَ)) صحيح أبي داود    

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah ambaye amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa amewekwa chini ya kivuli hali yake taabani baada ya kudhoofika kutokana na Swawm akamwambia: ((Sio katika wema (Kumcha Allaah) kufunga katika safari)) [Swahiyh Abiy Daawuud]. Lakini ikiwa hakutokuwa na taklifa wala mashaka, mtu anaruhusiwa kufunga.

  

19. Kutokujua Hukmu za Swawm:

Baadhi ya watu hawajui Hukmu sahihi za funga kisha huwa hawaulizi, ima kwa kuona hayaa au wakidhani wanajua. Ni vizuri mtu aulize lile asilo na hakika nalo kwa wale wenye elimu, ile asije akakosa fadhila na khayr hizi zipatikanazo kwa nadra mno. Na hali ya kutokujua Fiqh ya Swawm, kama kujua mambo yenye kufunguza na yale yasiyofunguza, kunaweza kumpelekea mtu kushinda na njaa bure huku Swawm yake ishabatilika, au kumfanya mtu afungue na hali Swawm yake bado ni sahihi. Mfano wa mambo yasiyobatilisha Swawm ni; kudungwa sindano, kung'oa jino, kujipulizia dawa ya pumu, wanawake kufanyiwa ukaguzi sehemu zao za siri na daktari (gynaecology checkup) - mtu ahakikishe anampata daktari wa kike na akiwa Muislam ndio bora zaidi, na akikosa kabisa hapo ni dharura tena na halaumiwi - na hili si katika Ramadhwaan tu, bali ni wakati wowote mwanamke anapokwenda Hospitali awe anafanya jitihada na kuuliza apatiwe daktari wa kike.

  

20. Kumjua Allaah Katika Ramadhwaan Pekee:

Baadhi ya watu humkumbuka Allaah katika mwezi huu tu, utakuta wanafunga na kuswali katika Ramadhwaan kisha baada ya Ramadhwaan kila kitu kinasimama kana kwamba Allaah Hayupo tena! Ni vyema watu wajue kuwa Allaah ni wa miezi yote na si mwezi wa Ramadhwaan pekee.

  

21. Kutamani Ramadhwaan Iishe:

Baadhi ya watu wanahesabu masiku na wakiwa wanaomba Ramadhwaan imalizike upesi ili warejee katika hali yao ya kawaida ambayo wanaiamini kuwa ina uhuru wa kufanya wanayoyataka. Lau angelijua mja fadhila na khayr zilizo katika mwezi huu, hakika angetamani usiishe.

 

Katika mwezi ambapo tendo dogo lakuingizia ujira zaidi ya maradufu. Katika mwezi huu kuna usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu. Katika mwezi huu vishawishi na balaa za Shaytwaan vimewekwa mbali. Katika mwezi huu Malaika wametapakaa kukusanya ‘amali zako za khayr hata za udogo wa sisimizi

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa Atuongezee elimu ya Dini Yake Tukufu ili tuzidi kutoka katika kiza na kuingia katika mwanga utuongoze katika Swiraatwul-Mustaqiym.

 

Share