32-Fatwa: Kutoa Nyama Kwa Ajili Ya Zakaatul-Fitwr

Kutoa Nyama Kwa Ajili Ya Zakaatul-Fitwr

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je, inaruhusiwa kutoa nyama kwa ajili ya Zakaatul-Fitwr?

 

 

JIBU:

 

Zakaatul-Fitwr lazima itolewe katika mfumo wa chakula kinachotumika na watu kwa sababu ya usimulizi uliosimuliwa na Al-Bukhaariy (151) kutoka kwa Abuu Sa'iyd al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: "Zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  tulikuwa tukitoa siku ya ('Iyd) al-Fitwr, swaa’ moja ya chakula" Na Abuu Sa'iyd kasema: "Chakula chetu kilikuwa ni shayiri, zabibu, mtindi mkavu na tende."

 

Ikiwa aina ya chakula cha watu  wa mji wako ni nyama basi inaruhusiwa kutoa Zakaatul-Fitwr.

 

Shaykhul-Islaam (Rahimahu Allaah) katika Al-Majmuwu' Al-Fataawa (25/68): "Ikiwa aina ya chakula cha watu ni mojawapo wa aina hizi, basi hakuna shaka kuwa kinaruhusiwa kutoa aina yao ya chakula.”

 

Lakini je, wanaweza kutoa chakula kisichokuwa miongoni mwa hivyo?  Mfano ikiwa chakula chao ni mchele au mahindi, je, watoe ngano au shayiri au inakubalika kwao kutoa mchele na mahindi?

 

Ikhtilaaf mashuhuri ya rai kuhusu (Swali) hilo lipo. Rai iliyo sahihi baina ya mbili ni kwamba chakula kinachotumika na watu kitolewe japokuwa sio miongoni mwa aina hizo. Hii ni rai ya wengi wa ‘Ulamaa, kama ash-Shaafi'y na wengineo. Hikma asasi kutoa sadaka ni kusaidia masikini kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

((chakula cha wastani mnachowalisha ahali zenu)) [Al-Maaidah 5:89]

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamrisha Zakaatul-Fitwr iwe ni swaa’ ya tende au swaa’ ya shayiri, kwa sababu hivyo ndivyo vilivyokuwa vyakula vya watu wa Madiynah. Ingelikuwa chakula chao ni kitu kingine basi asingeliwaamrisha watoe chakula ambacho sio kinachotumika kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyokuwa Hakuamrisha katika hali ya kafara" [mwisho wa kunukuu]

 

Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika I'laam Al-Muwaqqi'iyn (3/12):

"Hicho ndicho  kilichokuwa chakula cha Madiynah. Ama kwa watu wa nchi nyingine, watoe swaa’ ya chakula chao, ikiwa mfano chakula chao ni mahindi au mchele au tiyn au aina yoyote ya nafaka. Ikiwa chakula chao sio aina ya nafaka, kama maziwa, nyama, samaki, basi watoe Zakaatul-Fitwr yao katika mfumo wa chakula kinachotumika chochote kitakachokuwa. Hii ni rai ya ‘Ulamaa wengi wao na ndio rai iliyo sahihi na hakuna rai nyingine itakayoshauriwa. Nia ni kutimiza haja ya masikini siku ya 'Iyd na kuwasaidia kwa kuwapa chakula wanachotumia sana. Kutokana na hivi, inakubaliwa kutoa unga japokuwa haikutajwa katika Hadiyth Swahiyh" [mwisho wa kunukuu]

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema katika Ash-Sharh Al-Mumti' (6/182):

"Lakini ikiwa chakula kinachotumika na watu sio mbegu (nafaka) au mazao bali ni chakula kama nyama, kama mfano wa watu wanaoishi Ncha Ya Kaskazini (North Pole), ambao chakula chao zaidi ni nyama, basi rai iliyo sahihi kabisa na kukubalika ni kuitoa nyama." [mwisho wa kunukuu]

 

 

 

Share