Kazi Katika Uislam

 

Kazi Katika Uislaam

 

Alhidaaya.com

 

 

Utangulizi

 

Kulingana na Kamusi ya Kiingereza ya Collins, kazi imefafanuliwa kama juhudi za kimwili au kiakili zilizoelekezwa kufanya/kutengeneza kitu, malipo anayopewa kwa amali, biashara, utaalamu, shughuli au ufahamu.

 

 

Katika Uislam, kazi inamaanisha juhudi au uajiriwa unaofanywa ili mtu kupata pato la halali na katika mipaka ya maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kanuni Zake. Pale Muislam anapofanya hivyo kwa nia safi na ikhlasi, anapata ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Katika Uislam dunia ni sehemu ya kuvuna kwa ajili ya Akhiraah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّـهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ ۖ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا ۖ وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّـهُ إِلَيْكَ ۖ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٧٧﴾

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi. [Al-Qaswas: 77]

 

Na Anasema vilevile:

وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾

Na Tukafanya mchana kuwa ni wa kutafutia maisha. [An-Nabaa: 11]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuwekea mchana hasa ili tuweze kuhangaika kimaisha.

Kwa sababu sisi tuko katika ardhi hii, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametufundisha du’aa ifuatayo ya sisi kutaka kheri za nyumba mbili. Anasema Aliyetukuka Anasema:

 

وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿٢٠١﴾أُولَـٰئِكَ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّمَّا كَسَبُوا ۚ وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٢٠٢﴾

Na miongoni mwao kuna wasemao: Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto. Hao watapata pato lao kutokana na waliyoyachuma, na Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu. [Al-Baqarah: 201-202].

 

 

Waislam katika eneo la Afrika Mashariki wanachukuliwa kuwa sawa na wavivu kwa sababu ya jinsi walivyojiweka katika hali ya uzembe wa hali ya juu. Utawaona vijana wenye miili imara wanakaa mabarabarani, kwenye mabustani na mabarazani, nje ya Msikiti na sehemu nyengine za anasa wakizembea na kuzungumza mambo ya upuuzi. Pia vijana waliohamia nchi za kimagharibi kwa sababu ya ruzuku inayotolewa na serikali wamechukua mienendo hiyo mibaya.

 

 

Si halali kwa Muislam kutofanya kazi ili kujikimu kimaisha kwa kisingizio cha kuyaweka maisha yake kuwa wakfu kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah au kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa njia hiyo. Pia haifai kwao kutegemea sadaka japokuwa wana uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na nguvu zao. Katika hili, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sadaka si halali kwa tajiri wala mwenye uwezo wa kimwili” [at-Tirmidhiy].

Katika riwaya nyengine ya Abu Daawuud na an-Nasaa’iy, ‘Ubaydullah ibn ‘Adiyy al-Khiyaar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ameripoti: “Watu wawili waliniambia kuwa walikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa Hijjatul Widaa alipokuwa akigawa Zakaah. Walimtaka usaidizi. Aliwatazama kuanzia utosini hadi chini na kuwaona kuwa wamejenga vizuri na wenye nguvu. Aliwaambia: ‘Ikiwa mwataka, nitawapatia (Zakaah), lakini hakuna Zakaah kwa aliye tajiri wala kwa yule mwenye nguvu anayeweza kupata pato”.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislam kuomba omba pasi na dharura yoyote, hivyo kukosa heshima na hadhi. Hili lengo lake ni kuwafundisha na kuwahimiza Waislam kulinda na kuwa mbali na mienendo ya kupe kwa kuwanyonya wenziwe (watu wengine).

 

 

Hadhi Ya Kazi

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anataja misingi inayotakiwa katika kufanya ukulima. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameitandaza ardhi na kuifanya kuwa muruwa na yenye rutuba kwa ajili ya ukulima na kumeza pamoja na kupata mazao. Zipo ayah nyingi kuhusu hilo lakini unaweza kutazama baadhi yake kwa mfano

 

وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْزُونٍ﴿١٩﴾وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ﴿٢٠﴾وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَائِنُهُ وَمَا نُنَزِّلُهُ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ﴿٢١﴾وَأَرْسَلْنَا الرِّيَاحَ لَوَاقِحَ فَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَسْقَيْنَاكُمُوهُ وَمَا أَنتُمْ لَهُ بِخَازِنِينَ﴿٢٢﴾

Na ardhi Tumeitandaza na Tukatupa humo milima iliyosimama thabiti, na Tukaotesha humo kila kitu kwa uwiano. Na Tukakujaalieni humo njia na mbinu za maisha na ya hao ambao nyinyi si wenye kuwaruzuku.  Na hakuna kitu chochote isipokuwa Tuna hazina zake, na Hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri maalumu. Na Tukatuma pepo (za rahmah) zikibeba umande na Tukateremsha kutoka mbinguni maji kisha Tukakunywesheni kwayo; wala nyinyi si wenye kuyahifadhi. [Al-Hijr: 19-22]

 

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالْأَرْضَ وَضَعَهَا لِلْأَنَامِ ﴿١٠﴾فِيهَا فَاكِهَةٌ وَالنَّخْلُ ذَاتُ الْأَكْمَامِ ﴿١١﴾ وَالْحَبُّ ذُو الْعَصْفِ وَالرَّيْحَانُ ﴿١٢﴾ فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٣﴾

Na ardhi Ameiweka chini kwa ajili ya viumbe. Humo mna matunda na mitende yenye

mafumba. Na nafaka zenye maganda na nyasi kavu na rehani; miti yenye harufu nzuri ya kunukia. Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?  [Ar-Rahmaan: 10-13]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema pia: 

 

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ بِسَاطًا﴿١٩﴾لِّتَسْلُكُوا مِنْهَا سُبُلًا فِجَاجًا﴿٢٠﴾

Na Allaah Amekufanyieni ardhi kuwa (kama) busati. Ili mpite humo njia pana.

[Nuwh: 19-20]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema: 

 

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ﴿٢٤﴾أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ﴿٢٥﴾مَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ﴿٢٦﴾فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ﴿٢٧﴾وَعِنَبًا وَقَضْبًا ﴿٢٨﴾

Basi atazame mwana Aadam chakula chake. Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu. Kisha Tukairarua ardhi miraruko. Tukaotesha humo nafaka. Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena). [‘Abasa: 24-28]

 

 

Na kadhalika katika ayah zote hizo kuna kuhimizwa watu kuwa wakulima na kutilia maanani ukulima. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Pindi Muislam anapopanda mti au mmea, hakuna ndege wala mwanaadamu atakayekula kwayo isipokuwa anaandikiwa sadaka” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika Hadiyth nyingine anasema: “Kikisimama Qiyaama na mkononi mwa mmoja wenu ana mche akaweza kuumeza basi afanye hivyo kwani atapata ujira kwayo”. Hii ni hima ya hali ya juu aliyotupatia Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata katika wakati mgumu kama huo wa Qiyaama ambapo mambo yote yatabadilika.

 

Mbali na ukulima, Muislam anaweza kujishughulisha na sayansi za msingi, viwanda na taalamu nyengine kwa idadi kubwa inayoweza kukidhi mahitaji yetu ya kijamii.

Qur-aan imetaja viwanda na taaluma nyingi na kuziita ni fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza kuwa:

 

Nabiy Daawuud (‘Alayhis-salaam) alikuwa mfua vyuma hivyo akitengeneza nguo za chuma za kivita.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

وَعَلَّمْنَاهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍ لَّكُمْ لِتُحْصِنَكُم مِّن بَأْسِكُمْ ۖ فَهَلْ أَنتُمْ شَاكِرُونَ ﴿٨٠﴾

Na Tukamfunza (Daawuwd) uundaji wa mavazi ya kivita ya chuma kwa ajili yenu ili yakuhifadhini kutokana kupigana vita kwenu. Je, basi mtakuwa wenye kushukuru? [Al-Anbiyaa: 80]

 

Aliyetukuka anasema:

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ مِنَّا فَضْلًا ۖ يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ ۖ وَأَلَنَّا لَهُ الْحَدِيدَ ﴿١٠﴾أَنِ اعْمَلْ سَابِغَاتٍ وَقَدِّرْ فِي السَّرْدِ ۖ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Daawuwd fadhila kutoka Kwetu, (Tukasema): Ee majabali! Rejesheni kumsabbih (Allaah) pamoja naye na ndege pia. Na Tukamlainishia chuma. Na kwamba: Tengenezeni mavazi ya chuma mapana, na kadiria sawasawa katika kuunganisha daraya, na tendeni mema; hakika Mimi ni Mwenye kuona myatendayo. [Sabaa: 10-11]

 

Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-salaam) alikuwa mjengaji,

 

وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ غُدُوُّهَا شَهْرٌ وَرَوَاحُهَا شَهْرٌ ۖ وَأَسَلْنَا لَهُ عَيْنَ الْقِطْرِ ۖ وَمِنَ الْجِنِّ مَن يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَمَن يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿١٢﴾يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ۚ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

Na kwa Sulaymaan Tulimuitishia upepo; safari yake ya asubuhi ni mwezi, na safari yake ya jioni ni mwezi, na Tukamtiririzia chemchemu za shaba. Na miongoni mwa majini wanaofanyia kazi mbele yake kwa idhini ya Rabb wake. Na yeyote atakayezikengeuka amri Zetu, Tutamuonjesha adhabu ya moto uliowashwa vikali mno. Wanamfanyia kazi atakayo; (kujenga) ngome ndefu za fakhari na tasawiri, na madeste makubwa kama mahodhi na masufuria makubwa yaliyothibiti imara. (Tukasema): Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani! Na wachache miongoni mwa waja Wangu ni wenye kushukuru. [Sabaa: 12-13].

 

Dhul Qarnayn alitengeneza ukuta mrefu kama kizuizi dhidi ya maadui,

 

قَالَ مَا مَكَّنِّي فِيهِ رَبِّي خَيْرٌ فَأَعِينُونِي بِقُوَّةٍ أَجْعَلْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ رَدْمًا ﴿٩٥﴾آتُونِي زُبَرَ الْحَدِيدِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا سَاوَىٰ بَيْنَ الصَّدَفَيْنِ قَالَ انفُخُوا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَعَلَهُ نَارًا قَالَ آتُونِي أُفْرِغْ عَلَيْهِ قِطْرًا ﴿٩٦﴾فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا ﴿٩٧﴾

Akasema: Alivyonimakinisha Rabb wangu ni bora zaidi (kuliko ujira), basi nisaidieni kwa nguvu (za watu) niweke baina yenu na baina yao kizuizi imara. Nileteeni vipande vya chuma. Mpaka aliposawazisha kujaza baina ya kingo mbili za majabali; akasema: Pulizeni. Hata alipovifanya moto, akasema: Nipeni nimwagie juu yake shaba iliyoyayushwa. Basi (Ya-juwj na Ma-juwj) hawakuweza kuukwea, na wala hawakuweza kuutoboa. [Al-Kahf: 95-97]

 

 

Nabiy Nuwh (‘Alayhis Salaam) alikuwa seremala,

 

وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۚإِنَّهُم مُّغْرَقُونَ﴿٣٧﴾وَيَصْنَعُ الْفُلْكَ وَكُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ مَلَأٌ مِّن قَوْمِهِ سَخِرُوا مِنْهُ ۚ قَالَ إِن تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ﴿٣٨﴾

Na unda jahazi mbele ya macho Yetu na ufunuzi wa Wahy Wetu, na wala usinisemeze kuhusu wale waliodhulumu; hakika wao ni wenye kuzamishwa. (Nuwh) Akawa anaunda jahazi; basi kila walipompitia wakuu katika kaumu yake walimfanyia dhihaka. Akasema: Ikiwa mnatufanyia dhihaka, basi nasi tunakufanyieni dhihaka kama mnavyotufanyia dhihaka. [Huwd: 37-38].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia Anatutajia merikebu kubwa sana kama milima, ambazo zinavuka baharini.

وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ﴿٣٢﴾

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni merikebu zinazotembea baharini kama milima. [Ash-Shuwraa: 32].

 

Zaidi ya hayo, Qur-aan imetufahamisha kuwa chuma kina thamani kwa kutilia mkazo jambo hilo. Anasema Aliyetukuka:

 

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ ۖ وَأَنزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ وَرُسُلَهُ بِالْغَيْبِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢٥﴾

Kwa yakini Tuliwapeleka Risuli Wetu kwa hoja bayana, na Tukateremsha pamoja nao Kitabu na Miyzaan (shariy’ah) ili watu wasimamie kwa uadilifu. Na Tukateremsha chuma chenye nguvu shadidi na manufaa kwa watu, na ili Allaah Ajue nani atakayeinusuru (Dini Yake) na Rusuli Wake hali ya kuwa ni ghayb. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu zote, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika. [Al-Hadiyd: 25].

 

 

Kazi yoyote yenye kukidhi mahitaji ya jamii au inayoleta faida ya kihakika inachukuliwa kuwa ni nzuri, ilimradi anayeifanya aifanye kwa njia nzuri, kama inavyotakikana na Uislam. Baadhi ya watu wanazitweza baadhi ya kazi, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha kuwa heshima na hadhi ya mtu imefungamana na yeye kufanya kazi – kazi aina yoyote ila zile zilizo haramishwa. Hivyo, Uislam ulinyanyua hadhi na vyeo vya kazi nyingi ambazo watu walikuwa wanaziona kuwa duni.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni bora kwa mtu kuchukua kamba na kuleta mzigo wa kuni mgongoni mwake na kuzuiza ili Allaah Ailinde heshima yake, kuliko yeye kuomba kutoka kwa watu bila kujali kama watampatia au watamnyima” [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Ndio yule Swahaba alipokariri kuja kumtaka msaada Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza kama ana akiba yoyote nyumbani kwake. yule bwana akamwambia anacho kitambara. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwagizia akilete, na kilipoletwa alikinadi nacho kikanunuliwa kwa dinari mbili. Moja kati ya hizo dinari mbili Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia anunulie chakula na akiache nyumbani. Ya pili Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe alikwenda sokoni na kununua kile chuma cha shoka na kumtilia mpini kwa mkono wake. Kisha alimwambia asionekane pale mpaka baada ya muda fulani. Swahaba huyo alielekea msituni ili kukata kuni. Baada ya muda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana na huyo bwana kukiwa na sauti ya pesa zikilia mfukoni kwake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia hii ni bora kabisa kuliko kuomba omba.

 

 

Rusuli na Manabii (‘Alayhim-salaam) ndio ruwaza njema kwetu. Wao walifanikiwa katika kazi zao kwa kiasi kikubwa. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Daawud alikuwa mtengenezaji makoti ya chuma na ngao zake, Aadam alikuwa mkulima, Nuuh alikuwa seremala, Idriys mshonaji na Muwsa mchungaji” (Al-Haakim).

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hakumtuma Nabiy bila ya yeye kuchunga kondoo”. Wakamuuliza Swahaba: “Hata wewe, ewe Rasuli wa Allaah?” Akajibu: “Hata mimi, nilikuwa nikichunga kondoo wa watu wa Makkah kwa ujira” (Al-Bukhaariy).

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Swahaba zake hivi ili kuwafunza kuwa heshima inakuwa kwa wale wanaofanya kazi, na sio wale wenye kukaa na kuzembea na kuwa kupe kuwala wengine. Nasi tunaakiwa tufuate mtindo huo wa kufanya kazi. Zipo fursa nyingi, ambazo zinaonekana na sisi Waislam kama ni kazi duni zinazotuteremsha vyeo ambapo wengi wanaishi kwa kufanya kazi hizo na vile vile kuwa na hadhi zao nzuri. Na hivyo kuwa na heshima na hakuna wa kumkebehi au kumdharau kwa kuwa yeye anafanya juhudi na anakula kwa jasho lake.

 

Uislam umetuhimiza sisi kufanya biashara, na kuziita kutafuta fadhila ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Tafadhali tazama ayah zifuatazo kuhusu mas-ala hayo 2: 198; 24: 37; 28: 57; 73: 20 na kadhalika.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanya biashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe aliweka nidhamu kabambe na kanuni za kibiashara mbali na ghushi (udanganyifu), kuwasilisha kwa namna nyengine, kuficha bidhaa na kufanyiana hiyana.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupigia mfano wa jinsi ndege anavyofanya juhudi kutafuta riziki na akakuita kuwa ni kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika hilo. Hivyo kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni mwanzo kumfunga ngamia kisha kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) asimfanye atoroke. Imepokewa kwa ‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ikiwa nyinyi mtamtegemea Allaah upeo wa kumtegemea basi Atawaruzuku nyinyi kama Anavyomruzuku ndege. Anatoka katika kiota chake asubuhi tumbo lake likiwa tupu na anarudi ikiwa tumbo lake limejaa” (At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Sahihi).  

 

 

Kazi Zilizoharamishiwa

 

Uislam umeharamisha baadhi ya kazi, ambazo zinakwenda kinyume na kiini cha misingi yake. Ni haramu kumeza, kula au kuvuta mti kama hashiysh, tumbaku, marijuana, na mihadarati mingineyo ambayo ni haramu kuliwa, kutafunwa au kuvutwa, kwa kuwa mimea kama hiyo haina matumizi mengine ila ya kuleta madhara. Pia si sababu sahihi kwa Muislam kusema anapanda miti au anafuga wanyama kwa ajili ya kuwauzia wasiokuwa Waislam, kwani Muislam haruhusiwi kushiriki katika kueneza vilivyo haramu na vyenye madhara.

Uislam pia umekataza taalamu fulani na viwanda kwa wafuasi wake kwa sababu zina madhara kwa itikadi, maadili, heshima, muruwa na kadhalika. Mfano ni kama ukahaba ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَلَا تُكْرِهُوا فَتَيَاتِكُمْ عَلَى الْبِغَاءِ إِنْ أَرَدْنَ تَحَصُّنًا لِّتَبْتَغُوا عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَمَن يُكْرِههُّنَّ فَإِنَّ اللَّـهَ مِن بَعْدِ إِكْرَاهِهِنَّ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٣﴾

Na wala msiwalazimishe vijakazi wenu kufanya ukahaba kama wakitaka kujisitiri, ili mtafute mafao ya uhai wa dunia. Na yeyote yule atakayewalazimisha, basi hakika Allaah, baada ya kulazimishwa kwao huko, ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nuwr: 33].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alikataza hilo, bila kuangalia wala kujali nani atafaidika kwayo. Uislam umekataza dansi, muziki hata nyimbo zenye kuamsha hisia za kiume au kike au shughuli nyingine yoyote kama hiyo, kama nyimbo zenye kuashiria au zilizo chafu au michezo ya kuigiza yenye kuelekeza kwenye uasherati na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32].

 

Utengenezaji wa vileo, mihadarati na masanamu pia umeharamishwa. Uislam umekataza biashara yenye dhulma, udanganyifu, kuongeza faida kubwa sana katika biashara au kueneza vitu vya haramu. Pia ni haramu kufanya biashara ya pombe, nguruwe, masanamu au kitu chengine chochote ambacho utumiaji wake umeharamishwa na Uislam. Wafanya biashara wawe na tahadhari ya kughushi, kugeuza au kuvuruga vipimo na ratili, kuzuilia na kuficha bidhaa ili asiwe ni mwenye kukosa ulinzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Pia atahadhari kwa hilo, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema yafuatayo kuhusu kupunja katika kupima:

وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

 Ole kwa wanaopunja. Ambao wanapopokea kipimo kwa watu wanataka wapimiwe kamilifu. Na wanapowapimia (watu) kwa kipimo au wanawapimia kwa mizani wanapunja. [Al-Mutwaffifiyna: 1-3].

 

 

Watu wa Madyan, waliotumiwa Nabiy Shu‘ayb (‘Alayhis-salaam) ili kuwaonya dhidi ya kupunja wanapopima waliadhibiwa vikali sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumkadhibisha Nabiy wao (Tazama 7: 85-93 na 11: 84-95).

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatoa onyo kali kwa mwenye kuchukua na kutoa riba na Ametangaza vita dhidi yao.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿٢٧٨﴾فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ ﴿٢٧٩﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na acheni yaliyobakia katika ribaa ikiwa nyinyi ni Waumini. Na msipofanya basi tangazeni vita kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake. Na mkitubu basi mtapata rasilimali zenu msidhulumu na wala msidhulumiwe. [Al-Baqarah: 278-279]. 

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dirhamu moja ya riba ambayo mtu ataitumia kwa kujua ni mbaya zaidi kuliko kufanya zinaa mara 36” [Ahmad].

Haifai kabisa kuficha vyakula ili kupata faida nyingi zaidi au kuficha kasoro ya bidhaa yoyote unayouza.

 

 

Sifa Nzuri Za Mfanyakazi Muislam

 

Mfanyakazi Muislam mzuri ana sifa maridhawa zifuatazo:

 

1.    

Mjuzi na Mwenye Elimu: Ujuzi na elimu ni sifa muhimu sana ili shughuli zote ziendeshwe kitaalamu kama inavyotakiwa. Ndio Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis-salaam) alimwambia mfalme wa Misri yafuatayo:

قَالَ اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ ۖ إِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ ﴿٥٥﴾

(Yuwsuf) Akasema: Niweke katika kusimamia hazina ya nchi; hakika mimi ni mhifadhi mjuzi. [Yuwsuf: 55].

 

2.  Uaminifu na Nguvu: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anazungumzia kuhusu tazkiya aliyotoa binti ya mzee mkongwe kwa babake kwa sifa alizokuwa nazo Muwsaa (‘Alayhis-salaam):  

قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ ۖ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴿٢٦﴾

Mmoja wao akasema: Ee baba yangu, muajiri! Hakika mbora uwezaye kumwajiri ni mwenye nguvu mwaminifu. [Al-Qaswasw: 26].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanyabiashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Muislam ni lazima awe muaminifu katika shughuli zake zote na kutokuwa muaminifu ni kuwa na moja wapo wa alama ya unafiki.

 

 

3.   Kutunza Vitu vilivyo chini yake: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anamzungumzia Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis-salaam) pale aliposema:

 

اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ ۖ إِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ ﴿٥٥﴾

Niweke katika kusimamia hazina ya nchi; hakika mimi ni mhifadhi mjuzi. [Yuwsuf: 55].

 

4. Bidii na Juhudi: Pato la kufanya kwa mikono yako ndio kazi bora kabisa ambayo mtu anaweza kufanya. Imepokewa na Rafi‘ ibn Khadij (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasulu wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni pato gani lililo bora zaidi, naye akajibu: “Ni mtu kufanya kazi kwa mikono yake na kila biashara iliyokubaliwa (na sheria)” (Ahmad na at-Tirmidhiy).

Rusuli wote (‘Alayhim-salaam) walikuwa wakila kwa pato la jasho lao kwa kufanya kazi.

 

5. Kutunza Wakati wa Kazi: Hii ni sifa ya Muumini aliyejikita katika Iymaan. Mtu anapoanza kazi huwa ana mkataba na mkubwa wa kampuni au shirika na kila mfanyakazi huwa ana masaa yake ya kuwa kazini. Kutotekeleza hilo huwa unajiingiza katika sifa ya unafiki kwani Muislam mwema na mzuri ni yue anayetunza mkataba na ahadi.

 

 

Sifa Nzuri Za Mwajiri Muislam

 

Mwajiri Muislam ni lazima afikirie na azingatie zile hisia za wanaadamu wenziwe. Hivyo, asimtwike mwajiriwa kwa kumpatia kazi au mzigo asiouweza. Tazama jinsi gani yule mzee mkongwe na mcha Allaah alivyomwambia Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam):

 

قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ۖ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ ۚ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾

Akasema: Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane; ukitimiza kumi, basi ni kutoka kwako. Na wala sitaki kukutia mashakani; utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa Swalihina. [Al-Qaswasw: 27].

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema yafuatayo kuhusu hayo kama ilivyopokewa na Safwaan kutoka kwa Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema: “Tahadharini sana, kwani yeyote atakayemdhulumu mtu aliyeandikiana naye mkataba, au akampunja haki yake, au akamlazimisha kufanya kazi ngumu upeo wa nguvu zake, au akamchukulia chochote pasi na idhini yake, mimi nitamtetea Siku ya Qiyaama” [Abu Daawuud].

 

 

Mwajiri hafai kumtwika mzigo mkubwa hata mtumwa wake kwa kumpatia kazi zaidi ya uwezo wake, basi mwajiriwa ndio haifai zaidi. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni muhimu sana kumlisha mtumwa, kumvisha (sawa sawa) na kutomtwika mzigo wa kupita uwezo wake” [Muslim].

 

 

Katika riwaya ya Imaam Maalik, Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amepokea kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtumwa anafaa apatiwe chakula na mavazi kwa njia ya kawaida, na anawajibika kufanya zile kazi anazoweza bila ya shida”. Maalik amesema kuwa ‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akienda vijijini kila siku ya Jumamosi na pindi anapomuona mtumwa anafanya kazi inayopita uwezo na nguvu zake basi alikuwa akimpunguzia.

 

 

Mfanyakazi anatakiwa alipwe ujira au mshahara wake kikamilifu pindi tu anapomaliza kazi yake hiyo au mwisho wa mwezi. Kuhusu hili amepokea Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana, lakini mfanyakazi analipwa ujira wake kamili pale tu anapomaliza kazi yake” [Ahmad na at-Tirmidhiy]. Na katika riwaya nyengine: “Kabla jasho lake halijakauka”.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anamchukia na Atakuwa dhidi ya mwajiri asiyelipa ujira au mshahara kwa ukamilifu kwa waajiriwa wake. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Anasema: ‘Nitakuwa dhidi ya watu watatu Siku ya Qiyaama:

 

1.      Mtu anayefanya ahadi kwa jina Langu, lakini anafanya khiyana,

2.      Mtu anayemuuza mtu huru (kama mtumwa) na kula thamani yake, na

3.   Mwajiri anayemwandika kibarua ambaye anafanya kazi yake kiukamilifu lakini yeye hamlipi ujira wake’” [Al-Bukhaariy].

 

 

Hitimisho

 

Kwa muono wa Uislam, Waumini wa kweli ni wale wenye kutekeleza amali na kutia bidii katika kazi zao za halali, ambao sifa zao za kipekee ni kuwa shughuli za hii dunia haziwafanyi wao kusahau wajibu wao kwa Rabb wao Mlezi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

رِجَالٌ لَّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ ۙ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ ﴿٣٧﴾

Wanaume ambao haiwashughulishi tijara wala uuzaji na kumdhukuru Allaah na kusimamisha Swalaah na kutoa Zakaah wanakhofu Siku zitapopinduka humo nyoyo na macho [An-Nuwr: 37].

 

Muislam mzuri ni yule ambaye baada ya amali yoyote ya ‘Ibaadah moja anajitupa uwanjani ili kutafuta fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿١٠﴾

Na inapomalizika Swalaah, tawanyikeni katika ardhi, na tafuteni katika fadhila za Allaah, na mdhukuruni Allaah sana ili mpate kufaulu. [Al-Jumua’ah: 10].

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kwa hima na sisitizo Alilotupatia kwa kazi Hakuiacha hata siku tukufu na siku kuu ya wiki, Ijumaa iwe sisi hatufanyi kazi bali Anataka baada ya Swalah ya Ijumaa tutawanyike katika ardhi ili tufanye kazi na tupate riziki ya halali.

 

Muislam anapotunukiwa fadhila na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa), anafaa amuhimidi na kumshukuru Muumba wake kwa kushikilia amri Zake na kukaa mbali na makatazo Yake. Huu ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa), kwani Yeye Anasema:

 

هَـٰذَا مِن فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ ۖ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ ﴿٤٠﴾

Hii ni katika fadhila za Rabb wangu, Anijaribu; je, nitashukuru, au nitakufuru. Na yeyote yule anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na yeyote yule asiyekuwa na shukurani, basi hakika Rabb wangu ni Mkwasi, Mkarimu. [An-Naml: 40].

 

Lau waajiri Waislam watachukua maagizo haya na kujipamba na sifa tulizozitaja zilizowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waajiriwa nao wakatekeleza wajibu na majukumu yao basi hakungekuwa na matatizo aina yoyote katika jamii yetu ya Kiislam. Inabidi sisi turudi katika Uislam sahihi uliokamilishwa na Nabiy wetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tupate kufanikiwa hapa duniani na kesho Akhera.

 

Share