Zakaatul-Fitwr: Hikmah Na Hukmu Zake

 

Zakaatul-Fitwr : Hikma Na Hukmu Zake

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Nini Makusudio Ya Zakaatul-Fitwr Na Nini Hikmah Yake?

 

1. Muislamu anayetoka kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhwaan anatakiwa amalizie funga yake kwa kutoa Zakatul-Fitwr kama shukurani kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kumuwezesha kutekeleza Swawm.

 

2. Juu ya hivyo, Zakatul-Fitwr itamsafisha mwenye kufunga kutokana na maovu ya ulimi aliyotamka kama maneno machafu na ya upuuzi.

 

3. Kumuepusha Muislamu na ubakhili.

 

4. Zakaatul-Fitwr pia itawaepusha masikini na wanaohitaji kutokana na kuomba siku ya 'Iyd.

 

Hayo ni kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ قَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْل َالصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ". رواه أبو داود   قال النووي : رَوَاهُ أَبُو دَاوُد مِنْ رِوَايَةِ ابْنِ عَبَّاسٍ بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ 

 

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr iwe ni fardhi kwa ajili ya kumsafisha aliye funga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kwa ajili ya kuwalisha masikini. Atakayeitoa kabla Swalah basi ni Zakaah iliyokubaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalah itakuwa ni sadaka" [Abuu Daawuwd, na kasema An-Nawawy amesimulia Abuu Daawuwd katika riwaaya ya Ibn 'Abbaas kwa isnaad nzuri] 

 

 

Hukmu Zake:

 

Zakaatul-Fitwr Ni Fardhi Kwa Kila Muislamu

 

 

Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa kila Muislamu, mkubwa na mdogo, mwanaume na mwanamke, aliye huru na mtumwa. Hii ni kutokana na usimulizi Swahiyh ufuatao:

 

عَن ْابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْتَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ". البخاري

 

Kutoka kwa bin 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa' moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri." [Al-Bukhaariy] 

 

* swaa’ moja = kilo mbili na nusu (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.

 

Hivyo ni wajibu wa kila Muislamu atoe Zakaatul-Fitwr kwa ajili yake na kwa ajili ya familia yake na wote waliomo katika jukumu lake.

 

 

 

Nani Apasaye kutoa:

 

Yeyote mwenye uwezo na hata mwenye kumiliki chakula cha siku moja ajitolee mwenyewe pamoja na watu wake wote ambao wako chini ya jukumu lakekama mke, watoto, wazazi ambao hawana kipato.

 

Ikiwa mtoto amezaliwa baada ya kuzama jua usiku wa kwanza wa 'Iyd (siku ya mwisho ya Ramadhwaan) naye inapendekezeka kumlipia kwa sababu 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifanya hivyo ingawa sio fardhi. 

 

 

Nani Apokee

 

Ingawa ‘Ulamaa wengine wameona kuwa ni sawa na watu wanopasa kupokea Zakaah ya mali lakini rai iliyo sahihi kabisa na inayokubalika zaidi ni kwamba itolewe kwa maskini na wenye kuhitaji pekee.

 

 

Wakati gani wa kuitoa

 

Wakati unaopendekezeka zaidi ni kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhwaan hadi asubuhi kabla ya Swalah ya 'Iyd.

 

Pia inaweza kutolewa siku moja au mbili kabla ya 'Iyd kama ilivyokuja dalili katika Swahiyh Al-Bukhaariy kwamba, "Walikuwa (yaani Maswahaba) wakitoa (wakiwapa masikini) kabla ya Fitwr kwa siku moja au siku mbili."

 

Haipasi kutoa baada ya Swalah kwani huwa si Zakaah tena bali huwa ni sadaka kama alivyosimulia Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma)

 

 "...مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ". رواه أبو داود 

"Atakayetoa kabla ya Swalah itakuwa ni Zakaah iliyokubaliwa na atakayetoa baada ya Swalah itakuwa ni miongoni mwa sadaka" [Abuu Daawuwd]

 

 

Kitu gani kutoa?

 

Ni chakula kinachotumiwa na watu zaidi katika mji kama ni shayiri, au tende kavu, au mchele n.k. hii ni kutokana na dalili ifautayo:

 

قال أبوسعيد الخدري رضي الله عنه: "كنا نخرج يوم الفطر في عهد رسول صلى الله عليه وسلم صاعاً من طعام ، وكان طعامنا الشعير والزبيب و الأقط والتمر" أخرجه البخاري

 

Kutoka kwa Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allahu 'anhu): "Tulikuwa tukitoa siku ya Fitwr zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) swaa' ya chakula na kilikuwa chakula chetu ni shayiri, zabibu, jibini na tende" [Al-Bukhaariy]

 

 

Kiwango cha kutoa:

 

Ni swaa' moja ya chakula ambayo ni sawa na kilo mbili na nusu, au miteko ya mikono miwili ya mtu wa wastani mara nne. Hii ni kutokana na kauli ya:

Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukilipa Zakaatul-Fitwr swaa' moja ya chakula, au swaa' ya shayiri (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama hizo) au swaa' ya tende au swaa' ya aqit (mtindi mkavu) au swaa' ya zabibu." [Al-Bukhaariy]

 

 

Kutoa Pesa Inaruhusuiwa?

 

Haipendekezwi kutoa ila tu ikiwa hawapatikani masikini wa kupewa chakula katika mji. Ikiwa hivyo, basi kukusanywa pesa na watu wenye kuaminika na kutumwa katika nchi ambazo zina masikini zaidi na huku wawanunulie chakula kinachopaswa kugaiwa. Kwa hali hiyo imeruhusiwa.

 

 

 

 

Share