Uzito Wa Thawabu Za Kutoa Mali Yako Kwa Ajili Ya Allaah (سبحانه وتعالى)

 

Uzito Wa Thawabu Za Kutoa Mali Yako Kwa Ajili Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

  مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّائَةُ حَبَّةٍ ۗ وَاللَّـهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٦١﴾ 

261. Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja ya mbegu iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 261]

 

Kila unapotoa mali yako katika njia ya Allaah, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hukuzidishia hiyo mali. Mfano huo Alioutoa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hesabu yake ni kama ifuatavyo:

 

Punje moja imechipuza mashuke saba              1 x 7       =      7

Katika kila shuke moja zimo punje mia            7 x 100    = 700

 

Kwa hiyo jumla ya kuzidishiwa ni mia saba. 

 

Dalili nyengine inapatikana pia katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي مَسْعُودٍ الْأَنْصَارِيِّ، قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ بِنَاقَةٍ مَخْطُومَةٍ، فَقَالَ: هَذِهِ فِي سَبِيلِ اللهِ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لَكَ بِهَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ سَبْعُ مِائَةِ نَاقَةٍ كُلُّهَا مَخْطُومَةٌ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Mas-‘uwd Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba mtu mmoja alimleta ngamia wake pamoja na hatamu yake akasema: Huyu ni kwa ajili ya sabiliLLaah.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kwa huyo ngamia uliyemtoa, utalipwa ngamia mia saba Siku ya Qiyaamah wote wakiwa na hatamu))  [Muslim na An-Nasaaiy]

 

Hadiyth nyingine:

 

عن أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ( كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ  الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ إلى ما شاء اللهُ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kila ‘amali (njema) ya mwana Aadam inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba hadi Atakavyo Allaah…)). [Ahmad, Swahiyh Al-Jaami’ (4538)].

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema pia kuwa juu ya kumzidishia anayetoa kwa ajili Yake, pia humlipa malipo mema na matukufu:

 

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

11. Nani ambaye atamkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amuongezee maradufu na apate ujira mtukufu. [Al-Hadiyd: 11]

 

 

Tambua kuwa Yeye Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Anayeturuzuku hiyo mali, kisha Anatutaka tumkopeshe katika hicho alichotupa ili Atulipe zaidi ya Aliyoturuzuku. Basi nani atakayesita kumkopesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) huku ategemee  malipo kama hayo?

 

Kutoa mali kwa fiy Sabili-Allaah ni jambo lenye kutaka kuazimiwa kikweli kwani hakuna asiyependa kumiliki mali. Na wakati wa kutoa mali, shaytwaan husimama haraka kumtia wasiwasi mwana Aadam asitoe mali yake. Unapofika wakati huo basi ndugu Muislamu kumbuka kuwa thawabu zake ni nyingi mno na nzito mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ndio maana utaona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametanguliza mali kabla ya nafsi katika kuhimiza kufanya jihaad  katika njia ya Allaah:

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ﴿١٠﴾

10. Enyi walioamini! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?

 

تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿١١﴾

11. Mumuamini Allaah na Rasuli Wake, na mfanye jihaad katika njia ya Allaah kwa mali zenu, na nafsi zenu. Hivyo ndiyo bora kwenu mkiwa mnajua.

 

يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٢﴾

12. (Allaah) Atakughufurieni madhambi yenu, na Atakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito na masikani mazuri katika Jannaat za kudumu milele. Huko ndiko kufuzu adhimu. [Asw-Swaff: 10-12]

 

  

Vile vile:

 

 إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴿١٥﴾

15. Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Rasuli Wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakafanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah. Hao ndio wakweli. [Al-Hujuraat: 15]

 

Kama tunavyoona katika Aayah hizo za juu kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatupa nguvu na kutuzidishia iymaan kutoa mali zetu kwa kutuhakikishia kuwa ni kama kufanya biashara Naye ambayo matokeo yake ni kupata faida nyingi na juu ya hivyo ni kupata maghfirah kutoka Kwake. Anasema pia:

 

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾

29. Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea.

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾

30. Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake, hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwingi wa kupokea shukurani.   [Faatwir: 29-30]

 

 

Share