Ikiwa Ameandikiwa Ajiue Vipi Aingie Motoni?

 

Ikiwa Ameandikiwa Ajiue Vipi Aingie Motoni?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asallam alleikhum, swali langu ni kama ifuatavyo, kuna mawaidha nimeisha wahi kuyasikia na yalikuwa yakisema hivi, binadam unapozaliwa unaandikiwa jinsi uhai wako utakavyokuwa hiyo ikiwa pamoja na kifo chako. Sasa kuna watu ambao wamejiua wenyewe na pia dini inasema kuwa kujiua ni dhambi na ukijiua utaenda motoni, sasa kama ni kweli ukiwa umezaliwa na kuandikiwa jinsi gani utakufa, na kama umeandikiwa kujiua ni vipi uende motoni? Samahani naomba unijibu swali ili ingawa watu wanaweza kuona ni swali dogo lakini mimi linanisumbua, shukrani.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hayo uliyoyataja yamo katika Hadiyth nambari 4 ya kitabu al-Arba‘iyn an-Nawawiyyah kutoka kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan ‘Abdullaah bin Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) inayosema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ndiye msema kweli wa kusadikiwa:  "…kisha hutumwa Malaika akampulizia roho ndani yake, na akaamrishwa mambo manne: Kuandika riziki yake, ajali yake, amali yake, na kama ni mwema au muovu …" [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Sasa Hadiyth hii na nyinginezo na Aayah kadhaa zinazozungumzia mas-ala ya kudura zimeeleweka vibaya sana. Hivyo, zinavyotumiwa na watu ni kwa kujiweka katika hali ya kuwa wao hawana jukumu wala amri yoyote hivyo hawapaswi kuadhibiwa na Allaah Aliyetukuka kwani hawakutaka wao. Hii ni mantiki na itikadi potofu sana kwa kuwa Allaah Aliyetukuka Ametuumba na kutupatia uongozi kwa yale yanayofaa kufanywa na mwanaadamu. Baada ya hapo mwanaadamu huyo akapatiwa uhuru kamili wa kuchagua lakini akapewa bishara kuwa akifanya mema atalipwa mazuri na akaonywa akifanya maovu basi ajue kuwa ataadhibiwa vikali sana. Allaah Aliyetukuka Anasema:

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا﴿٣﴾

Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima (awe) ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru. [Al-Insaan: 3].

 

Kuwa na shukurani ni kutii maagizo ya Muumba kwa hiari yake mwenyewe na kukanusha ni kwenda kinyume.Miongoni mwa sifa za Allaah Aliyetukuka ni Mjuzi na Mwenye habari ya kila kitu. Hivyo, kuandikiwa wewe yote utakayoyafanya ni katika elimu yake pana ambayo sisi hatuna wala hatutakuwa nayo. Mfano mdogo ambao unaweza kueleweka na tutambue kuwa mifano ya Allaah ni ya juu zaidi. Mfano huu ni ule wa mwalimu ambaye amekufunza kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Na katika ule ujuzi alionao akawa ni mwenye kuandika kabla ya mtihani wa mwisho kuwa mwanafunzi ‘a’ atapasi kwa kupata daraja ya juu na mwanafunzi ‘b’ atafeli. Baada ya kufanya hivyo akaiweka karatasi hiyo katika meza yake na pindi matokeo yalipotokea akawaita wote wawili na kuwaonyesha alivyotabiri yamekuwa vile vile – mwanafunzi ‘a’ amepata daraja ya juu na mwanafunzi ‘b’ amefeli.

 

Hapa twaweza kujiuliza kuwa mwalimu alijuaje hayo naye hana elimu ya ghaibu. Jawabu ni kuwa alikuwa tayari amemsoma kila mmoja kwa yale matokeo waliokuwa wakiyapata na juhudi zao. Mmoja alikuwa na bidii na alikuwa akipasi vyema na mwingine alikuwa hana hima kabisa na alikuwa daima akifeli. Je, mwanafunzi ‘b’ hapa ataweza kumlaumu mwalimu kuwa ndiye aliyesababisha kufeli kwake? Jawabu litakuwa ni laa, bali lawama itarudi kwake mwenyewe kwa kutofanya bidii.

 

Sasa itakuwaje sisi tuwe ni wenye kumlaumu Allaah Aliyetukuka kwa kusema kuwa tayari Alikuwa Ametuandikia kwenda Motoni na ilhali sisi ndio tulikataa njia ya sawa. Pia tufahamu kuwa sisi hatujui lililoandikwa na Allaah, wala hali ya mtu baina yake na Mola Wake, lakini twaona mwisho wake. Kwa hivyo sisi twahukumu kwa tulionalo. Ipo Hadiyth nyingine iliyotajwa na Muslim, kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika mtu huja akafanya amali za watu wa Peponi kwa makisio ya watu naye kihakika ni mtu wa Motoni". Hapa yaonyesha kuwa mtu huyu amali zake si nzuri kwa uhakika.

 

Kwa ajili sisi kutojua aliyoandika Allaah Aliyetukuka na kwa kuwa Yeye Ametupatia muongozo mzuri sisi ni kufanya juhudi ili na kumuomba Allaah Aliyetukuka Atufanikishie. Naye Ametuahidi kuwa mwenye kumtaka kwa dhati basi Atampatia uongofu.

 

Soma vile vile Swali na Jibu katika kiungo kifuatacho ambalo limejibiwa kirefu kuhusu mas-ala haya:

 

Majaaliwa Na Makadario Ya Watu Wema Na Waovu

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share