Nabiy Aadam Alikuwa Na Rangi Gani?

 

Nabiy Aadam Alikuwa Na Rangi Gani?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam Alaykum,

Tafadhali naomba kufahamishwa kuhusu ni ipi rangi ya baba yetu Adam Alayhis salaam? je ni mwafrika, mzungu, au mwarabu n.k.

Wabillahi Tawfiq

 

Assalaam Alaykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani kwa swali hilo kuhusu maumbile ya Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam).

 

Hakika isiyopingika ni kuwa Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam) ndiye mwanadamu wa kwanza kuumbwa na Allaah na baada ya kukaa kwa muda fulani mbinguni aliteremshwa ardhini ili awe khalifa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alimuumba Nabiy Aadam (‘Alayhis-salaam) kwa mchanga au udongo, na asli ya vitu hivi ni kuwa vina rangi tofauti. Na hii ni dalili kubwa ya kuwepo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuwa Yeye Ndiye Muumbaji na Anavyotaka Anafanya na hakuna aliye na  uwezo wa kumuuliza lakini Yeye Ndiye Atakayetuuliza kwa yale ambayo tumeyafanya hapa duniani.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ ﴿٢٠﴾

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbeni kutokana na mchanga; tahamaki mmekuwa watu mnaotawanyika. [Ar-Ruwm: 20].

 

Na pia:

 

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ ﴿٢٢﴾

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni uumbaji wa mbingu na ardhi, na kukhitilafiana lugha zenu na rangi zenu. Hakika pana katika hayo, bila shaka Aayah (ishara, zingatio nk) kwa wenye ujuzi. [Ar-Ruwm: 22].

 

Hivyo, kuwa na rangi tofauti ni Ishara za kuwepo kwa Allaah na sifa Yake ya Uumbaji.  Na kwa kuwa uumbaji Wake ni kwa udongo wenye rangi tofauti kila mtu anayezalikana naye anakuwa na rangi tofauti na hata na nduguze wa kiume na kike.

 

Hivyo, ndivyo tulivyo pata rangi zetu kutoka kwa baba yetu kwa kurithi. Na leo tazama unaweza kukuta ndugu wawili wa baba na mama mmoja wanavyotofautiana katika rangi zao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share