Husda Inayofaa Na Isiyofaa

 

SWALI:

 

assalam aaleykum wa rahmatulalla wa barakatuh

napenda kuuliza kama binaadam umepatwa na husda dawa yake kitu gani au kuna duaa yoyote

 

waaleykumsalaam wa rahmatualla  wa barakatuh.  

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ingelikuwa ni vizuri kama muulizaji angelieleza hali yake ilivyo hata akahukumu kwamba amepatwa na husda. Kwa sababu maneno haya mara kwa mara tunayasikia, ni wepesi mtu kuhukumu kuwa kapatwa na husda anapofikwa na mtihani ukiwa ni mkubwa au mdogo.

 

Husda (al-hiqd) ziko aina mbili; husda nzuri na mbaya; nzuri ni ile ambayo umemuona mwenzio amejaaliwa neema ya mali na elimu ukatamani nawe uwe kama yeye. Haya ni mambo ya kupendekezeka kwani ni kujitamania mazuri ya Aakhirah. Hadiyth ifuatayo inaelezea aina hii ya husda:

 عن أبي سعيد قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((لا حسد إلا في اثنتين : رجل آتاه الله القرآن فهو يتلوه آناء الليل وآناء النهار , فيقول الرجل : لو آتاني الله مثل ما آتى فلانا فعلت مثل ما يفعل , ورجل آتاه الله مالا فهو ينفقه في حقه فيقول الرجل : لو آتاني الله مثل ما آتى فلانا فعلت مثل ما يفعل)). أحمد

 Kutoka kwa Abu Sa'iyd ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna husda isipokuwa kwa mawili; mtu aliyepewa na Allaah Qur-aan akawa anaisoma nyakati za usiku na nyakati za mchana akasema [huyo mtu anayemhusudu] “Allaah Angelinipa na mimi mfano alivyopewa fulani ningelifanya kama anavyofanya”. Na mtu aliyepewa mali na Allaah akawa anaipa haki yake kwa kuitoa akasema huyo mtu, “Allaah Angelinipa kama alivyopewa fulani ningelifanya kama anavyofanya”)) [Ahmad na wengineo kwa usimulizi mwengine]

 

 

Hivyo husda kama hii haimdhuru mtu na wala mtu mwenye kuhusudu kwa kutamani kupata neema kisha afanye mema hapati dhambi kuwa na husda kama hiyo. Ama husda isiyopasa mtu kuwa nayo kwa nduguye Muislamu ni ile iitwayo 'al-hiqdil-haqiyqiy' (husda ya kweli) nayo ni kuwa na chuki na kutamani neema aliyonayo mwenzio imuondoke na makatazo hayo tumepata mafunzo yake kama ifuatavyo:

 

 (( وَلاَ تَتَمَنَّوْاْ مَا فَضَّلَ اللّهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَى بَعْضٍ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُواْ وَلِلنِّسَاء نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ وَاسْأَلُواْ اللّهَ مِن فَضْلِهِ إِنَّ اللّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا))

 

((Wala msitamani alichowafadhili Allaah baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika waliovichuma, na wanawake wana fungu katika waliovichuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu)) [An-Nisaa: 32]

 

Kwa hiyo aliyekosa neema fulani inampasa aridhike na alivyojaaliwa na akipenda amuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ambaye Ndiye mtoaji rizki na neema zote Naye ni Rahiymun-Kariym (Mwenye kurehemu na Mkarimu).

 

 

 

Na kutoka katika Sunnah:

عن أبي هُريرةَ رضي اللهُ عنه قال: قال رسوُل الله صلى الله عليه وسلم : ((لا تَحَاسَدُوا، ولا تَنَاجَشُوا، ولا تَباغَضُوا، ولا تَدَابَرُوا، ولا يَبعْ بَعْضُكُمْ على بَيْعِ بَعْضٍ، وكُونُوا عِبادَ اللهِ إخْوَاناً، المُسْلمُ أَخُو المُسْلمِ: لا يَظْلِمُهُ، ولا يَكْذِبُهُ، ولا يَحْقِرُهُ، التَّقْوَى هاهُنا – (ويُشِيرُ إلى صَدْرِه ثَلاثَ مَرَّاتٍ ) بِحَسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أن يَحْقِرَ أخاهُ المُسْلِمِ، كُلُّ المُسْلِمِ على الْمسْلِم حَرَامٌ: دَمُهُ ومالُهُ وعِرْضُهُ)) مسلم

Kutoka kwa Abu Hurayra (Radhiya Allaahu 'anhum) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Msioneane choyo, wala msizidishiane bei (za vitu), wala msichukiane, wala msipigane mapande (msitengane), wala msishindane kwa kupunguza bei. Lakini kuweni ndugu, enyi waja wa Mwenyeezi Mungu, Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake, hamdhulumu wala hamvunji, hamwambii uongo wala hamdharau. Ucha Mungu uko hapa (huku akiashiria kifuani kwake kwa vidole vyake) mara tatu. Ni uovu wa kutosha kwa mtu kumdharau ndugu yake Muislamu. Muislamu ameharamishiwa kwa Muislamu mwenzake; damu yake, mali yake na heshima yake (Yaani haramu kuchukua mali ya mwenzako, kumuua na kumdhalilisha) [Imesimuliwa na Muslim]  

 

 

Husda hiyo huenda imamdhuru mtu akafikwa na maovu, kama kupungukiwa na hizo neema, au kupata maafa au kuumwa au aina yoyote ya mashaka. Ndio maana tumefunzwa adhkaar za kila aina ambazo zina kinga ya kutuhifadhi na kila aina ya maovu pamoja na husda. Inapomfika mtu hali hiyo inampasa ajitibu kwa Ruqyah (kinga) zenye mafunzo kutoka Qur-aan na Sunnah kama ifutavyo:

 

  1. Kusoma Qur-aan kwa wingi kwani Qur-aan ni uongofu, nuru, poza na tiba ya nyoyo na mwili.

 

  1. Aayah tano za mwanzo katika Suratul-Baqarah.

 

  1. Aayatul-Kursiy na Aayah mbili zinazofuatia.

 

  1. Aayah mbili za mwisho katika Suratul-Baqarah.

 

  1. Kusoma Suratul-Ikhlaasw (Qul-Huwa Allaahu Ahad) na Al-Ma'udhaataan (Qul-A'uudhu Birbbil-Falaq na Qul-A'uudhu Birabbin-Naas) mara tatu kila asubuhi na jioni.

 

 

  1. Nyiradi za asubuhi na jioni zilioko katika kitabu cha Hiswnul Muslim.

 

Nyiradi za asubuhi na jioni

 

Hizi pekee zinamtosheleza mtu kumkinga na kumtoa katika husda na kila aina ya shari ikiwa atazidumisha kila siku ipasavyo. Lakini wengi hawalitii manani hili jambo muhimu la kujikinga na pia kujipatia neema nyingi, na jambo ambalo hata halimchukui mtu zaidi ya dakika kumi. Wanasubiri hadi mtu yamfike maovu ndipo anapoanza kuhangaika.

Bonyeza upate du'aa pia:

Duaa ya kupatwa na janga au balaa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share