Kutubu baada ya kujiripua Je Rizki Nnayopata ni halali?

 

SWALI:

 

ASALAM ALEIKUM

NIMESOMA SWALA LA KUJIREPUA LILIVYOULIZWA NA KUJIBIWA VIZURI SANA. SASA MIMI NAULIZA KAMA VILE ILIVYOANDIKWA, KUWA KUOMBA MSAMAHA WA ALLAAH [SW] LAZIMA LILE KOSA ULIACHE. SASA KAMA MTU ANA WATOTO NA ANAOGOPA KWENDA KUSEMA UKWELI KWA SABABU WANAWEZA KUWAPOKONYA WATOTO. PILI VIPI UTAKAVYO TOKA KUINGIA NCHINI NYINGINE NA TATU JEE RIZKI UNAYOKULA NA KILA IBADAS UNAVYOFANYA NI BATIL? JEE KAMA UTASOMA KILILLAHI ILI UPATE KAZI UTAKAYO FANYA NCHINI NYINGINE ITAKUWA HARAM KWA KILA PESA UTAKAYOIPATA? TAFADHALI TUJIBU KWA HARAKA SANAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAA, INSHAALAAH TUELEZE NAMNA YA KUFAULU KATIKA TAWBA YA MTU ALIYEJIREPUA.


JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu mas-ala ya kujiripua. Kama tulivyoeleza katika jibu letu la awali ni kuwa ni makosa kwa Muislamu kusema uongo kwa hali yoyote ile. Hasa tena kwa nchi ambazo zinachukulia suala hilo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa na adhabu yake ukipatikana huenda ikawa kali.

Lakini kosa lenyewe lishafanyika kwa njia moja au nyingine na ni kwa aliyefanya hilo kuomba msamaha mwanzo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Kwa kuwa kunapatikana maafa makubwa sana pindi aliyefanya hivyo kwenda kuripoti kwa serikali basi kwa hali hiyo ataingia katika kanuni ya ki-Fiqhi. Nayo inasema: “Akhaffudh Dhwararayn – kuchagua jambo lenye dhara dogo zaidi katika mambo mawili”. Kwa kuwa unapokwenda kusema ukweli kama ulivyoeleza watoto wanaweza kudhurika kwa kuingia katika himaya ya wasiokuwa Waislamu itatosha kule kutubia kwa kutekeleza yale masharti matatu – kujuta, kuazimia kutorudia kosa na kujiondoa katika maasiya hayo. Pia itakuwa ni vyema kwako uwe utafanya mengi mengine katika mambo ya kheri.

Ama kuhusu swali lako la pili linalohusu kutoka katika nchi moja na kuingia nyingine ni juu yako. Sisi tunaweza kukupatia muongozo tu. Ushauri wetu wa dhati ni kwako kurudi kwenu ulikotoka ikiwa ni Kenya au Tanzania au nchi nyingine yoyote. Usitoke huko uliko ukaenda nchi nyingine katika Bara Ulaya na ukaanza kujiripua tena hivyo kuingia katika maasiya mengine ya uongo.

Ama kuhusu suala lako la tatu kwa kuwa tayari umetaka msamaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) chakula chako na ‘Ibaadah zako zitakuwa sawa kabisa. Ama ukasoma masomo ambayo hayajakatazwa katika Dini na kwayo ukapata kazi ya halali katika nchi nyengine pato lako litakuwa halali kabisa. Hivyo, kila pesa utakayopata katika kazi hiyo ni halali kwako kutumia na kusaidia wengine.

Hakika ni kuwa kufaulu kwa mtu aliyejiripua kunaweza kupatikana ikiwa mtu mwenyewe atakuwa na ikhlasi na atafanya juhudi kutekeleza yale masharti ya toba. Tunakutakia wewe na wengine mfano wako kila la kheri katika suala hilo na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Awawezeshe kupata mafanikio mema na utendaji mzuri wa yaliyo mema.

Soma pia Swali na Jibu lifautalo:

Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share