Mume Mwenye Mke Zaidi ya Mmoja Inafaa Kugawa Mirathi Kabla ya Kufariki?

 

SWALI:

assalam alaykum warahmatu llahi wabarakatu.

 

Naomba nijibiwe maswali yangu haya  Mungu awalipe kwa kutusaidia.

iwapo mume anamke zaidi ya mmoja , na ana nyumba mbili. jee atakosea akiwaandikia kila tumbo nyumba yake ikiwa mfano Mke wa kwanza ana watoto 4 na mke wa pili ana mtoto mmoja. Na akiziacha bila kuandika haitoleta hasara kwa mtoto mmoja peke yake kwa vile yeye sehemu yake ni ndogo tu na tumewaadhiwa na Mtume (SWA) kwa tusiwaachwe watoto wetu wakihangaika ( kuwaacha nje)( sina uhakika na hii Hadiyth ila nasikia tu kuwa ni maneno ya mtume (S.W.A) kama nimekosea M.Mungu anisamehe

Naomba majibu wabillahi taufik.

Assalam alaykum


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tumepokea maswali yako matatu ambayo umetuma katika barua moja, jambo ambalo tumesisitiza lisifanyike bali kila swali litumwe katika barua ya pekee. Kufanya hivi itakuwa wepesi kujibu kila swali na kulipa kila swali kichwa cha habari kinachostahiki na pia kupunguza usumbufu wa kuyagawa maswali. Hivyo tunakuomba wewe na ndugu wengine wote watekeleze haya muhimu wanapotuma maswali yao.

 

 

Tukirejea kwenye swali lako, Hadiyth yenye maana ifuatayo:

Ni bora kuwaacha watoto wako wakiwa wamejitosheleza kuliko wakiwa masikini wanaomba omba” (al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Sa‘d bin Abi Waqqaasw).

Pia tufahamu kuwa ni makosa kwa baba kutofanya uadilifu katika kuwapatia hadiya watoto wake. Hii ni kwa ile Hadiyth ya al-Baashir al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu), babake an-Nu‘man alipokuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutaka kumfanya shahidi kwa kitu alichompatia mtoto wake mmoja. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza: “Je, umewapa kama kitu hicho watoto wako wote?” aliposema hapana, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Mimi sishuhudii dhuluma” (al-Bukhaariy na Muslim).

Tukifanya hivyo katika mfano uliotoa utaona kuwa familia ndogo itakuwa imepata zaidi kuliko ile kubwa isipokuwa nyumba hizo mbili zikiwa zinalingana na mirathi ya kila familia. Vizuri zaidi ni kuzitia thamani nyumba kisha kugawa kama tulivyoamriwa katika sheria.

Inafahamika kuwa mirathi inagawanywa kwa mpangilio Aliouweka Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo hatuwezi kufanya tutakavyo.

Hivyo, Mirathi haiwezi kugawanywa kabla mtu hajafariki. Ama ikiwa mtu anataka kugawa mali yake akiwa hai, hilo halikatazwi, ana uhuru wa kugawa na kuwapa awatakao. Ama akishafariki mali yake itagaiwa kwa mujibu wa sheria inavyotaka.

Na Allaah Anajua zaidi

Share