Amemuingilia Mkewe Kimakosa Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

ASSALAMALEIKUM, NILKUWA NAULIZA KUWA WAKATI WA KITENDO CHA STARE YA MKE NA MUME KWA BAHATI MBAYA BALI YA KUTUMIA MBELE IKAINGIA NYUMA HUKMU YAKE NI NINI IWAPO MKE NA MUME WAMEINGILIANA KWA NJIA SIO LAKINI ILKUWA BAHATI MBAYA IKAINGIA NDANI TUNA HUKMU GANI KWA ALLAAH

SHUKRAN

WAASALAMALEIKUM 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako. Hakika ni kuwa ni madhambi makubwa kwa mwanamme kumuingilia mkewe kwa nyuma. Lakini suala hilo ni kama ulivyotuelezea kuwa uliingia sehemu hiyo ya nyuma bila kukusudia basi unasamehewa isipokuwa unatakiwa ujitahidi upeo wa uwezo wako ukiwa katika tendo la ndoa na usirudie tena. Tutambue kuwa kila jambo na kila kosa linategemea nia ya mtu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatambua yaliyo nyoyoni mwetu.


Pia omba msamaha kwa kosa hilo. Hakika Allaah
(Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametufundisha tusome: “Mola wetu! Usitutese kama tukisahau au tukikosa (tukafanya mabaya)” (2: 286).

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Awawezeshe musiwe ni wenye kurudia tena jambo hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share