Zingatio: Milango Ipo Wazi

 

Zingatio: Milango Ipo Wazi

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ee Muislamu, tambua wakati huu ambao milango ya toba ipo wazi, tofautisha na ule wakati ambao milango ya toba imefungwa, nao ni wakati ambao roho inatolewa. Jitahidi uulipize ule wakati ambao uliupoteza katika kutenda maasi. Jiweke karibu kwa Rabb Mlezi hapo ndipo utakaa mbali na Ibilisi. Kasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

 

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

 

Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]

 

Kutubia kwa Allaah ni katika sifa njema za Waumini. Kwani rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ilivyokuwa kubwa juu ya waja Wake Anawakubalia toba zao alimuradi bado hawajawa katika Sakaratul Mawt. Hapana toba kwa wenye kuchelewesha kutubia kwa makusudi hadi wakafikia kwenye mauti. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

 

 إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ

 

Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. [An-Nisaa: 17]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaendelea kusema: 

 

وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾ 

Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapohudhuria kwa mmoja wao husema: Hakika mimi sasa nimetubu. Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa: 18]

 

Basi nakunasihi ndugu yangu Muislamu, turejee pamoja kwa Rabb wetu kabla ya kufumba jicho. Tufanye haraka kwani hatujui mauti yatatukuta tukiwa wazima au wagonjwa. Tutambue kwamba hakuna mja asiyemkosea Rabb wake Mlezi wa Mbingu na Ardhi, lakini mbora wetu ni yule mwenye kurudi kwa haraka akiwa na majuto. Basi hapo Allaah Huwa na furaha kubwa juu ya mja kama huyu anayetubia toba ya kweli kweli. Tuangalie kwenye Hadiyth ifuatayo namna Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alivyo na huruma kupita mapenzi ya mama kwa mwana:

 

Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) amepokea kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutolewa na [Imaam al-Bukhaariy na Muslim]:

 

“Furaha ya Allaah kwa mja Wake Muumini ni kubwa pale atakapotubu, kuliko furaha ya mtu alioko katika jangwa, naye ana kipando chake, na mnyama huyo kabeba chakula na maji ya kunywa. Mtu huyo akafika pahala akalala, alipoamka hakumkuta yule mnyama wake, akaanza kumtafuta mpaka akachoka, akashikwa na kiu. Akasema: Bora nirudi pahala pangu nilipokuwa na nilale mpaka nife. Akalala (akingojea mauti), baada ya muda akazindukana na mnyama wake yuko chini yake pamoja na chakula chake na maji yake…

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anamalizia kwa kueleza kwamba furaha ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) huwa kubwa zaidi kuliko huyo aliyepotelewa na mnyama:

 

…Basi Allaah Huwa na furaha zaidi kwa mja Wake Muumini atakapotubu kuliko huyu mtu aliyepotelewa na mnyama wake kisha akamuona.”

 

 

Share