Ijumaa: Imaam Kutoa Khutbah Ya Ijumaa Bila Ya Kusimama Katika Mimbar

 

SWALI:

Assalaamu alaikum wr.wb. Mimi nina swala moja ambalo sijapata jibu na
Naomba munijibu ili nipatekuelimika na inshaallah Mwenyezi mungu
atuongoze kwa mema amin. Swali langu ni hili: Je inafaa Imam kutoa khutba ya ijumaa bila kusimama juu ya mimbar
? 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako kuhusu mas-ala ya mimbar ambayo hutumiwa na Khatwiyb wakati anapokhutubia Waumini siku ya Ijumaa. Mwanzoni alipohamia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah na kufaradhishwa Swalah ya Ijumaa alikuwa anakhutubia Waumini akiwa amesimama na huku ameegemea kwenye gogo la mtende. Wakati huo hakukuwa na mimbar, hivyo kumlazimu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusimama tu mbele ya Maswahaba zake. Akatokea Swahaba mmoja ambaye alimpatia rai Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ingekuwa bora lau angesimama juu ya kitu akiwa anatoa khutba kwa Waumini. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikubali rai hiyo, hivyo kutengenezwa mimbar ambayo aliitumia kuanzia wakati huo. Makhalifa pamoja na Maswahaba wengine waliokuwa wakitoa khutba wakawa ni wenye kuitumia na ikawa inatumia mpaka hivi leo katika Misikiti yetu.

Na tunaposema mimbar si lazima ziwe ni mimbar zile kubwa. Maana yake ni kitu tu ambacho kitamfanya Imaam awe juu, hivyo kinaweza kuwa kiti au kifaa chengine cha kusimamia Imaam wakati wa Khutba. Lakini ikiwa hakuna kifaa hicho cha kusimamia Imaam, naye akawa anakhutu bila kusimama juu ya chochote khutba yake itakuwa sawa na Swalah yenu ya Ijumaa itakuwa hivyo hivyo. Ila tu ikiwa hakuna cha kusimamia inambidi Imaam kama ada akae baada ya khutba ya kwanza kisha asimame tena kukamilisha khutba ya pili.

Hivyo, suala hilo lisikutie wasiwasi kabisa.

Na Allaah Anajua zaidi

Share