Fadhila Na Umuhimu Wa Swalaah Ya Jamaa

 

SWALI:

 

 

 

kusali nyumbani kwa uzuru kama vile alfajiri au isha je inawezekana au lazima kuwe na sababu maalummm?shukran kwa kutelimisha katika njia moja wapo ilyorahisi ALLLAH atakulipeni ujiraweni na akuzidishieni juhuni denu amina...WASSALA LAAHU ALA SAYYID NA MUHAMMAD WAALLA ALIHI WAASHABIHI WASSALAM..

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Hukumu ya Swalah ya Jamaa kwa wanaume:

Maulamaa wamekhitilafiana kuhusu kuwajibika kuswali Swalah ya Jamaa kwa wanaume katika kauli zifuatazo:

Kauli Ya kwanza: 

Swalah ya Jamaa kuwa ni wajibu wa kila mtu isipokuwa kunapokuwa na udhuru:

Hii kutokana na Ibn Mas'uud na Abu Muusa, na kasema 'Atwaa, Al-Awzaa'iy na Ath-Thawriy. Nao ni msimamo wa katika madhehebu ya Imaam Ahmad, na ibn Hazm na ni chaguo la Shaykhul-Islaam. Ila wamekhitilafiana baina yao kama je, ni sharti ya kuwa Swalah inaswihi au hapana!

Kauli Ya pili:

Swalah ya Jamaa sio wajibu wa kila mtu:

Nayo ni madhehebu ya wengi wao; Abu Haniyfah, Maalik na Shaafi'iy wakiwa wamekhitilafiana kama ni Sunnah, au Sunnah Muakkadah (Sunnah iliyosisitizwa) au ni Fardhu-Kifaayah.

Kwa vyovyote hivyo, inampasa Muislamu atambue kuwa Swalah ya Jamaa ina fadhila tukufu, nayo imesisitizwa sana na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ametuelezea fadhila na faida zake katika Hadiyth nyingi, baadhi yake:

 

عن ابنِ عمَر رضي اللَّه عنهما أَنَّ رسولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : ((صَلاةُ الجَمَاعَةِ أَفضَلُ مِنْ صَلاةِ الفَذِّ بِسَبْعٍ وَعِشْرِينَ درَجَةً )) متفقٌ عليه

Kutoka kwa ibnu 'Umar (Radhiya Allahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalah ya Jamaa ni bora kuliko Swalah ya pekee kwa daraja ishirini na saba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

وعن أَبي هريرة رضيَ اللَّه عنهُ قال : قال رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : ((صَلاةُ الرَّجُلِ في جَماعةٍ تُضَعَّفُ عَلى صلاتِهِ في بَيْتِهِ وفي سُوقِهِ خمساً وَعِشْرينَ ضِعفًا ، وذلكَ أَنَّهُ إِذا تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ الْوُضُوءَ ثُمَّ خَرَجَ إِلى المَسْجِدِ ، لا يُخْرِجُه إِلاَّ الصَّلاةُ ، لَمْ يَخْطُ خَطْوةً إِلاَّ رُفِعَتْ لَه بهَا دَرَجَةٌ ، وَحُطَّتْ عَنْه بهَا خَطِيئَةٌ ، فَإِذا صَلى لَمْ تَزَلِ المَلائِكَة تُصَلِّي عَلَيْهِ مَا دَامَ في مُصَلاَّه ، مَا لَمْ يُحْدِثْ ، تَقُولُ : اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَيْهِ ، اللَّهُمَّ ارحَمْهُ . وَلا يَزَالُ في صَلاةٍ مَا انْتَظَرَ الصَّلاةَ)) متفقٌ عليه . وهذا لفظ البخاري

Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalah ya Jamaa inazidi (thawabu) na Swalah ya mtu nyumbani kwake au dukani kwake kwa mara ishirini na tano, kwa hivyo anapotawadha akafanya vizuri wudhuu wake, kisha akatoka kwenda msikitini, hakuna lililomtoa ila Swalah, haendi hatua moja ila hupandishwa daraja (kwa hatua hiyo), na hufutiwa dhambi kwa hiyo hatua. Atakapokuwa anaswali, Malaika wanaendelea kumswalia madamu yumo kwenye Swalah ikiwa hatozungumza. Husema (Malaika) 'Ewe Allah Mswalie na Mrehemu'. Na huendelea hivyo wakati anasubiri Swalah nyingine)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Fadhila za kuswali Swalah ya Asubuhi na 'Ishaa katika Jamaa:

 

عنْ عثمانَ بنِ عفانَ رضيَ اللَّه عنهُ قالَ : سمعتُ رسولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقولُ : ((مَنْ صَلَّى العِشَاءَ في جَـمَاعَةٍ ، فَكَأَنَّما قامَ نِصْف اللَّيْل وَمَنْ صَلَّى الصبْح في جَمَاعَةٍ ، فَكَأَنَّما صَلَّى اللَّيْل كُلَّهُ)) رواه مسلم .

Kutoka kwa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba: Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Atakayeswali Swalah ya Ishaa katika Jamaa, atakuwa kama kwamba amesimama nusu ya usiku mzima. Na atakayeswali Asubuhi katika Jamaa atakuwa kama kwamba ameswali usiku wote)) [Muslim]

 

  عنْ عثمانَ بنِ عفانَ رضي اللَّه عنهُ قال : قال رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : ((مَنْ شَهِدَ العِشَاءَ في جمَاعةٍ كان لهُ قِيامُ نِصْفِ لَيْلَة ، ومَنْ صَلَّى العِشَاءَ والْفَجْر في جمَاعَةٍ، كَانَ لَهُ كَقِيَامِ لَيْلَة )) قال التِّرمذي : حديثٌ حسن صحيحٌ .

Kutoka kwa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Atakayehudhuria Swalah ya Ishaa katika Jamaa atakuwa kama kwamba amesimama nusu usiku, na atakayeswali Ishaa na Alfajrii katika Jamaa atakuwa kama kasimama usiku mzima)) [At-Tirmidhiy hadiyth hasan]

 

  عن أَبي هُريرة رضيَ اللَّه عنهُ أَنَّ رسولَ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : ((وَلَوْ يعْلَمُونَ مَا في العَتمَةِ والصُّبْحِ لأَتَوْهُما وَلَو حبْوًا )) متفقٌ عليه .

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Lau wangelijua faida katika (Swalah) ya ‘Ishaa na Asubuhi basi wangeliziendea (kuziswali) japo kwa kutambaa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

  عن أَبي هُريرة رضيَ اللَّه عنهُ   قال : قال رسولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : (( لَيْسَ صَلاةٌ أَثْقَلَ عَلَى المُنَافِقينَ مِنْ صلاة الفَجْرِ وَالعِشاءِ وَلَوْ يَعْلَمُونَ ما فِيهما لأَتَوْهُما وَلَوْ حبْوًا)) متفق عليه .

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Swalah iliyo nzito kwa wanafiki kama Swalah ya Alfajiri na ‘Ishaa. Lau kama wangelijua yaliyomo humo (fadhila na faida) wangeliziendea (kuziswali) japo kwa kutambaa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hivyo tumeona fadhila tukufu kama hizo na zaidi ya hizo, na pia faida kubwa zinazopatikana Muislam anapokwenda msikitini kuswali Jamaa. Basi kuziacha bila shaka ni hasara kubwa. Ama kama tulivyoona kwamba kunapotokea udhuru wa kutokuweza kwenda kwa sababu mbali mbali kama mvua, baridi, umbali wa msiktini basi hakuna ubaya kuswali nyumbani, na vizuri kuswali na familia kwa pamoja.

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share