Kukidhi Swalaah: Swalaah Ziloachwa Mingi Zilipwe Vipi? Nini Hukmu Ya Aliyeacha Kuswali Miaka Mingi?

 

SWALI LA KWANZA:

 

Asalam alaekum warahamatullah wabarakatu. Mimi nauliza hivi:  baadhi ya watu kuna baadhi ya swala ambazo hawakuziswali yaani walikuwa wanaswali na kuacha na hawana uhakika ni swalah gani na gani na ngapi. suala langu ni hivi (1) eti hawawezi kusali swalah za sunah?

(2) Sasa wafanye nini kukamilisha swala zao ili waweze kuswali swala za sunnah? Naomba ufanunuzi wenu. Wabillahi tawfiq. Mwenyezi Mungu awajaalie kila kheri hapa duniani na kesho akhera Amin.

 

SWALI LA PILI:

 

 

Asalamu alekum,

Suala langu ni kuwa vipi mtu alipe sala za miaka mingi nyuma? Nimesikia kwamba unatakiwa uziswali katika kila sala, mfano ukiswali dhuhuri usali na moja nyingine na ukisali alasiri usali moja nyingine extra ya kulipa , na eti uendelee hivo hivo miaka mingi, je ni kweli?

Nini hukmu ya mwenye kuacha kusali miaka mingi nyuma afanyeje ikiwa hawezi kulipa sala kama hivo?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwako ndugu yetu kwa swali lako kuhusu mas-ala ya kulipiza Swalah ulizoziacha. Wanazuoni wana rai mbili zenye kutofautiana:

 

Rai Ya Kwanza:

 

Kuwa kwa mtu ambaye hakuswali kwa sababu moja au nyengine anapoamua kuswali na hasa ikiwa kumepita muda mwingi ataleta toba kwa masharti yake yote. Hiyo ni kuwa atajuta, atajiondoa katika maasiya hayo na kuazimia kutorudia tena dhambi hilo la kutoswali. Pindi anapotubia na kujirekebisha basi huwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amemsamehe kwani hakuna haki ya binaadamu iliyoingia kati. Hayo ndio masharti yaliowekwa na kama Imaam an-Nawaawiy ambaye amesema katika Riyaadh asw-Swaalihiin, Mlango wa 2 kuwa wanazuoni wamesema hivyo.

 

 

Rai ya pili:

 

Ni ile inayosema kuwa ukiwa na deni la mwanaadamu mwenzio unatakiwa ulilipe ukiwa umesahau kufanya hivyo hata baada ya kupita muda wake. Deni la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) lina haki zaidi ya kulipwa. Hivyo, ukiwa umeghafilika kuswali Swalah yoyote ile, unatakiwa uiswali pindi unapokumbuka hata kama wakati wake umepita. Kwa mfano, umeona kuwa umeswali Swalah ya Alfajiri kwa kusahau ukakaa mpaka inafika saa sita mchana unakumbuka kuwa kumbe ulikuwa hujaswali inatakiwa hapo hapo uswali Swalah hiyo uliyosahau. Na ikiwa umepita muda basi utakisia muda wenyewe na kuweza kukidhi Swalah zenyewe. Hiyo itakuwa baada ya kuswali kwa mfano, Swalah ya Adhuhuri utachukua muda kwa kuswali Adhuhuri kadha za siku zilizopita na hivyo hivyo Swalah nyingine kama Alasiri na kadhalika. Jambo litafanyika mpaka muda uliokisia kuwa umeacha Swalah utakapofika yaani utaswali kwa idadi ya siku za nyuma ambazo ulikuwa huswali.

 

Msimamo sahihi - na Allaah ni Mjuzi zaidi - ni kuwa, aliyeacha Swalah kwa kupitiwa, kusahau, kulala...huyo anapaswa kulipa. Ama yule aliyeacha Swalah kwa makusudi, huyo hapaswi kuzilipa, bali anatakiwa kuomba msamaha na kufanya tawbah na kuzidisha mema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share