Kuchukua Mkopo Wa Ribaa kulipia Deni

 

SWALI:

 

ASSALAM ALAYKUM JAMIA:

 

Kwa sifa za M/Mungu mwenye kuneemesha neema ndogo na kubwa, pia sina budi kumshukuru M/Mungu kwa hapa nilipofika M/mungu awaje kheri kwa msaada wenu. AMIN

 

SUALA LANGU: Mimi naishi na familia yangu hapa UK tunajitegemea wenyewe ktk masuala ya Rent sasa kwa sasa tumefikwa na mtihani wa deni la kutokana na uwezo wetu hatuna uwezo wa kulilipa kwa pamoja ni kubwa sana sasa je naweza kwenda kuchukuwa MKOPO BENKI ili kufidia hii bill lakini tatizo benki unakopa 2 unalipa 4 sasa je ktk uislam na sheria za kiislamu sababu hii inakubalika kwani nitakuwa nalipa ribaa benki naomba ushauri wenu.

 

WABILLAHI TAWFIQ

 

WASALAAM ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu mas-ala haya ya ribaa ambayo yanajitokeza kila wakati japokuwa kulingana na maelezo yako inaonekana kuwa unajua ni haramu kukopesha kwa ajili ya kulipa ribaa. Kabla hatujakuja katika nasaha zetu kuhusu hilo ni vyema mwanzo tuitazame hukumu ya ribaa kwa uwazi zaidi.

 

Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ameharamisha kuchukua na kutoa ribaa katika njia zake zote. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Allaah Amehalalisha biashara na kuiharamisha ribaa” (2: 275).

Na amesema tena Aliyetukuka: “Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni yaliyobakia katika ribaa, ikiwa mmeamini. Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa mmetanganza vita na Allaah na Mtume Wake” (2: 278 – 279).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa: “Allaah Amemlaani mwenye kula ribaa, mwenye kuitoa na mashahidi wake na mwandishi wake” (Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

Na amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu uovu wa ribaa: “Dirhamu ya ribaa anayokula mtu na huku anajua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara thelathini na sita” (Ahmad).

Amesema tena: “ribaa ina milango 73 iliyo nyepesi na sahali ni mtu kumuoa (kumuingilia) mamake” (al-Haakim).

 

Hakika ni kuwa swali lako halipo wazi kama inavyohitajika ili tuweze kukusaidia vilivyo. Mfano ni ibara ifuatayo: “Tunajitegemea wenyewe ktk masuala ya Rent sasa kwa sasa tumefikwa na mtihani wa deni la kutokana na uwezo wetu hatuna uwezo wa kulilipa kwa pamoja ni kubwa sana sasa je naweza kwenda kuchukuwa MKOPO BENKI ili kufidia hii bill”. Mwanzo kabisa unasema kuwa mnajitegemea katika masuala ya Rent (ijara ya nyumba), lakini huu mtihani mliopata ni upi? Ilikuwaje mpaka mkawa na hilo deni kubwa ambalo kwa sasa mnashindwa kulilipa? Hiyo bill unayozungumzia ni gani? Mpaka tupate ufafanuzi wa wazi itakuwa tabu kuweza kukujibu inavyotakiwa.

 

Hata hivyo, inatakiwa utazame ile dharura uliyonayo kihakika na pia utazame njia nyingine za kupata mkopo bila ya ribaa kwa taasisi za Kiislamu. Inatakiwa uwe umefanya bidii na juhudi kubwa sana katika kutafuta mbinu za kisawa kwa mashirika ya Kiislamu pamoja na ndugu wenzako katika Dini. Ikiwa katika juhudi yako yote hukupata yeyote au shirika lolote lililoweza kukupatia mkopo ambao hauna ribaa basi kutegemea na ule uzito na shida uliyonayo tutaweza kukupatia ushauri.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akutolee njia ya kuweza kuondoka katika tatizo hilo na upate usahali mkubwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share