Biashara Ya Kuuza Maji Inafaa Kwa Ajili Ya Kuwahudumia Yatima?

SWALI:

 

Assalaamu alaikum wr.wb.


Naishi Canada (Toronto) na kwa hakika tuna chama chetu ambacho tunasaidiya mayatima sehemu za africa mashariki. Chama chenyewe kwa jina ni JUKUMU LETU. Kila mwezi tunalipa kiwango fulani kwa kila mtu aliyejiunga na hicho chama (members). Kwa maendeleo ya chama tukafanya majadiliano tuwe na biashara ambayo itaweza kutusaidiya baadaye, mojawapo ni kuuza maji, je 'uislamu unaruhusu uuzaji wa maji?
Inshaallah Mwenyezi mungu awajaaliwe maisha marefu na ajaaliye alhidaaya idumu masha inshaallah. Jazaakamullahu khairaan. Was salaamu alaikum wr. wb.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu biashara ya kuuza maji, na zaidi kwa du’aa zako nzuri kwetu. InshaAllaah Allaah Atutakabalie sisi na nyinyi wote.

Allaah Aliyetukuka Amehalalisha biashara zote ila zile ambazo zimekatazwa na Yeye. Biashara ambazo zimeruhusiwa ni nzuri na zenye baraka na zile zilizokatazwa basi hazina maslahi na wanaadamu bali ni madhara. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Allaah Ameihalalisha biashara na Ameiharimisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyokwishapita, na mambo yake yako kwa Allaah” (2: 275).

 

Kwa ajili ya maslahi yetu Allaah Aliyetukuka Akatuwekea mchana ili kufanya kazi na kupata chumo la halali ndani yake. Akasema Aliyetukuka: “Na Tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha?” (78: 11).

 

Biashara kwa ujumla wake ya halali imebarikiwa na Allaah Aliyetukuka. Na biashara inakuwa haramu tu inapokatazwa na sheria na ya maji si moja wapo katika hizo.

 

Hivyo, mnaweza kuendelea nayo na tunamuomba Allaah Aliyetukuka Azidi kuwabariki ili muweze kuwaangalia mayatima kwa njia nzuri zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share