Safari: Akitoka Dar Kwenda Arusha Anaruhusiwa Asifunge (Swawm)?

 

SWALI:

Mtu anaesafiri kutoka sehemu moja kwenda nyengine. Naomba ufafanuzi kidogo hapo kuhusu safari. Kilichokusudiwa katika safari ni nini hasa, maana mfano, mi natoka Dsm kwenda Arusha (Kilomita 850) nikitumia gari masaa 8-9 na nikitumia ndege ni saa 1-1.5 tu. naruhuswa kula kwa sababu nasafiri ama hii ni safari ipi hasa ambayo mwenye kufunga anaruhusiwa kula.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako la tatu. Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametuelezea kiujumla kuhusu mtu kutofunga kwa ajili ya safari wala Hakutuekea masafa yoyote na njia ya isafiri. Anasema Aliyetukuka: “Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine” (2: 184).

Kila mmoja wetu anajua safari pindi anapoazimia kufanya hivyo. Hakika ni kuwa wapo watu wanapata shida kwa kusafiri kwa ndege mbali na kuwa muda unakuwa mdogo. Hivyo, ikiwa unakwenda Arusha kutoka Dar es Salaam kwa ndege au gari uamuzi ni wako. Ikiwa hutakuwa na shida unapofunga waweza kufunga na ukitaka kufungua pia waweza fanya hivyo.

 

Lakini kutokufunga ni kutumia ruhusa na kufuata Sunnah hivyo itakuwa ni kupata thawabu zaidi kwani  usimulizi wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ufuatao unasema: 

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa amewekwa chini ya kivuli hali yake taabani baada ya kudhoofika kutokana na Swawm akamwambia: ((Sio katika wema (ucha Mungu) kufunga katika safari)) [Swahiyh Abiy Daawuud]

Kwa mwenye kufungua itambidi alipe siku alizokula akiwa katika safari.

 

Hata ukielekea Morogoro kutoka Dar pia ni safari na shari'ah imekupatia ruhusa ya kula.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share