Deni: Mama Anaweza Kumlipia Mwanawe Deni La Swawm?

SWALI:

assalaam alaykum warahmatullah wabarakatu.mwenyeezi mungu mtukufu akujaarieni kheri kwa kutuelimisha.swali langu ni hivi;mimi siumwi, nina deni la faradhi ya ramadhani. je mama yangu anaweza kunisaidia kufunga? tunafunga sote tukimaanishsa siku moja kwa malipo ya siku mbili. nilifungua wakti wa hedhi.je inaswihi?

 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Haifai mtu yeyote kumlipia mwingine deni la Swawm, kwani Fardhi hii ya Swawm inampasa kila Muislamu aliyekuwa baleghe, mwenye akili timamu, asiye na udhuru wa ugonjwa wa kumzuia kufunga Ramadhaan. Haifai kufanya hivyo hata kama anayetaka kumlipia ni mama au ndugu wa damu kwani kila mmoja ana jukumu lake la kutimiza fardhi zake na kila mmoja aatabeba madhambi yake kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 ((وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَى حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَى))

((Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine. (Kila mtu atachukua jukumu ya dhambi zake mwenyewe). Na kama aliyetopewa na mzigo wake akimwita (mwingine) kwa ajili ya mzigo wake (amchukulie) hautachukuliwa hata kidogo (na mtu huyo) inagawa ni jamaa yake)) [Faatwir:18]

Vile vile kila mtu atachuma yale tu aliyoyafanya yeye na atalipwa kwa mema au maovu aliyoyafanya:

 

((أَلَّا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى))   ((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَى))   ((وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَى))  (( ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاء الْأَوْفَى)) 

 

((Ya kwamba haichukui nafsi dhambi za nafsi nyingine))  

 

((Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyafanya mwenyewe)) 

 

((Na kwamba vitendo vyake vitaonekana))

 

 ((Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu))

 

[An-Najm:38-41]

Kwa hiyo kama mama yako alikusaidia kulipa deni la Swawm basi haikufaa Swawm yake, nawe itabidi uzilipe Swawm zote alizofunga mama yako kwa ajili yako. Na kama deni lilikuwa la Ramadhaan ya mwaka jana, basi itabidi ulipe hizo siku na pia kafara. Tafadhali bonyeza katika kiungo kifuatacho usome kuhusu mas-ala haya: 

Kulipa Swawm Na Kafara

Kuhusu kufunga katika hedhi, pia haifai Swawm yako itabidi pia uzilipe hizo siku ulizofunga katika hedhi. Mwanamke katika hedhi hatakiwi kufunga Swawm wala kusali, lakini anatakiwa alipe deni lake Swawm. Ama Swalah haimpasi kulipa, na hii ni Rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa wanawake wa Kiislamu kupunguziwa majukumu hayo ya kulipa Swalah za siku zao za hedhi.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share