Mwanamke Kaolewa Kwa Kudhani Mumewe Kafariki Safarini

 

SWALI:

Mwanamke ameolewa halafu wakaishi na mme wake kisha yule mme wake akasafiri na ktk hiyo safari akakaa mda. Na yule mwanamke akahisi kuwa mme wake atakuwa kisha kufa. Akatokea mtu akamuoa yule mwanamke, baada ya kufunga ndoa, jioni yake akalejea yule mme wake aliyekuwa kasafiri, sasa huyu mwanamme aliyefunga naye ndoa atarejeshewa mahari?

  

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako hilo. Hili ni swali ambalo ni zuri na hai kwani huwa linatokea kila leo.

Uislamu umeweka msingi kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Haifai kudhuru wala kulipana madhara” (Ibn Maajah, ad-Daraqutniy na Maalik).

Dhulma au kuduriana ni jambo ambalo limekatazwa, kwani pia Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema katika Hadithi Qudsiy:

Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhulma juu ya nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane” (Muslim).

Mume anaposafiri na akawa hajulikani alipo wala hakuna mawasiliano yoyote basi mwanamke ni mwenye kudhurika kisaikolojia; hisia na mawazo. Wanazuoni wametofautiana kuhusu kudhurika huku kwa mke ikiwa mume hajulikani alipo. Wapo wanaosema muda huo usizidi miezi minne na wengine sita na wengine tena ni mwaka mmoja. Lakini pindi mwanamke akawa hawezi tena kujizuilia kuelekea katika maasiya kwa kutokewepo mume na kutojulikana alipo ni sababu tosha ya kwenda kwa Qaadhi ili ajifusahi. Baada ya Qaadhi kumuachisha mke itabidi akae eda ya kufiwa na mume ikiwa mpaka muda huo hakujapatikana habari yoyote yake.

Ikiwa amekuja mume mwingine mwanamke huyo baada ya eda ataolewa kwa kulipwa mahari yake. Ikitokea tu ameolewa kisheria na yule mume wa awali akatokea mke atapatiwa uchaguzi baina ya mume wa awali na huyu aliyenaye sasa. Ikiwa mke atamchangua yule wa kwanza itabidi ajiachishe na huyu wa pili, naye wa pili hatadhulumiwa. Mke itabidi aombe khul‘u kwa Qaadhi na kujiachisha huko kisheria itabidi amlipe huyu mume mahari yake kwani si kosa lililotokana na mume huyo.  Baada ya hapo itabidi mwanamke akae eda kwa hedhi moja kama ilivyothubutu kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kisa cha Qays bin Thaabit (Radhiya Allaahu ‘anhu). Baada ya eda ikiwa hatakuwa na mimba, hapo atakuwa ni mwenye kuolewa na yule mume wake wa kwanza kwa Nikaah mpya na mahari mapya.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share