Ndugu Kwa Upande Wa Mama Zao Wanaweza Kuoana?

 

SWALI:

nawashukuru sana ndugu zangu hii ni mara ya pili naleta suala langu jengine. nilifurahi sana nilipojibiwa suala la mwanzo kuhusu mirathi na kweli muliokoa mali ambayo ilikuwa inarithiwa na warithi batili.

sasa nna rafiki yangu sote tuko nje ya Zanzibar na kwa kweli hapa tulipo ni taabu kupata ufumbuzi wa masuala yetu hasa ya sheria. 

Huyu rafiki yangu ana kaka yake (cousin), mama zao ni ndugu wa baba mmoja, mama mmoja. Huyu cousin wake ameoa mke ambaye aliwahi kuolewa na kupata watoto na sasa wameshapata watoto wengine. Rafiki yangu anataka kuoa mtoto wa huyu mama ambaye baba yake ni mwingine sie huyu cousin wake, je ndoa hii inafaa na kusihi?

Naomba jawabu. Nawatakia saumu njema ndugu zangu. Bye.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako ndugu yetu na twataraji kuwa utapata jawabu muafaka. Tunakutakia pamoja na kuwatakia Waislamu wote tuwe ni wenye kutakabaliwa Swawmu zetu, Ibaadah za mwezi wa Ramadhaan na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Atupe istiqaamah baada ya Ramadhaan.

Ama kuhusu swali lako ni kuwa ndugu wakiwa ni binamu au watoto wa halati (mama wadogo) ikiwa mwanzo wao wenyewe ni wa jinsia tofauti wanaweza kuoana. Lakini tukirudi katika swali lako ni kuwa hawa ndugu binamu (cousins), mmoja wao ameoa mke mwenye watoto na pia akapata watoto wake kwa mke huyo. Kisheria huyu rafiki yako anaweza kumuoa binti wa mke wa binamu (cousin) yako. Licha ya hivyo, hata binti wa huyo binamu (cousin) yake pia anaweza kumuoa kisheria bila tatizo lolote.

Kwa muhtasari ni kuwa ndoa hiyo inasihi na inafaa kisheria kabisa.

Na mwisho tunapenda kukushauri kuwa ukiaga ni bora utumie neno ‘Fiy AmaaniLlaah’ Uwe Pamoja na Amani ya Allaah, au ‘Assalaamu ‘alaykum’ Amani Iwe Juu Yenu badala ya kuwaiga wasio Waislam kwa kusema ‘bye’ unapomuaga Muislam.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share