Uhakikisho Wa Kusihi Ndoa (Talaka Mume Kurejea Kutenda Matendo Maovu)

 

SWALI:

 

nashukuru kwamajibu yenu na nimefahamu lkn sasanataka ushauri kwenu mume wangu nimemuambia  anasemayey hakusema hivyo na mmnakumbuka kanijibu kua ee hakusema kamndio talaka kanijibu ee sasa sijui niamue nini inshAllaah mataweza kunisaidia MUNGU atakulipeni kheri inshAllaah.



SWALI LA MWANZO LA MUULIZAJI linapatikana katika kiungo kifuatacho:

Talaka Kwa Mume Kurejea Matendo Maovu



 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Tunashukuru kuwa umepokea jibu la Swali lako, ila tunaona kuwa bado una mashaka na ndoa yako kama talaka imepita au haikupita kutokana na mazungumzo na mumeo.

Kutokana na maelezo yako kama ulivyoandika kwamba yeye hakusema hivyo,

Tukinukuu hapa chini maneno yako uliyosema kama yalivyo juu ya mstari:

nashukuru kwamajibu yenu na nimefahamu lkn sasanataka ushauri kwenu mume wangu nimemuambia anasemayey hakusema hivyo na mmnakumbuka kanijibu kua ee hakusema kamndio talaka kanijibu ee sasa sijui niamue nini inshAllaah mataweza kunisaidia MUNGU atakulipeni kheri inshAllaah.

Suala hilo liko wazi kabisa kuwa yeye amekanusha hayo maneno, kwa hiyo talaka haikupita hapo na ndoa yako inasihi bado. Talaka itakuwa imepita pindi angelikubali usemi huo au akikutamkia mwenyewe. Lakini madamu anakanusha usemi huo inaonyesha wazi kuwa bado anakutaka kuwa mke wake.

Tunakupa nasaha dada yetu kuwa usipendelee kumuanzia mumeo maneno kama hayo kwa sababu ya vitendo vyake viovu.

Unalopaswa kufanya ni kumuombea sana katika du'aa zako Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuepushe na maasi hayo na aridhike na wewe. Tambua dada yetu kuwa wanaume wameumbwa na udhaifu na udhaifu mkubwa mmojawapo ni huo na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akawaruhusu kuoa wake wanne, tofauti na hali za wanawake. Na hili ni jambo Alilolikidhi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa viumbe Vyake kwani Yeye Ndiye Aliyetuumba sisi binaadamu na Yeye Ndiye Mwenye kutujua tulivyo sisi na udhaifu wetu wote na ndipo Akatuwekea sheria mbali mbali, mojawapo kama hii ili pindi tunaposhindwa kujizuia udhaifu huo, tuishi katika uhalali na sio katika uharamu.

Na kuamini na kukubali sheria hii ya Mola wetu ndio dalili ya Muumini hasa, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))

((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allaah na Mtume Wake Wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi))[Al-Ahzaab:36]

 

Hata hivyo haina maana kwamba kwa udhaifu huo mwanamume anaruhusiwa afanye maasi hayo, bali anatakiwa amkhofu Mola Wake kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amekataza kabisa maasi hayo na Ametutahadharisha hata tusiyakaribie kama Anavyosema:

 

 ((وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً ))

))Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya)) [Al-Israa: ).

Kisha Ametupa maonyo makali kuhusu maasi hayo:  

((وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ  ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا))  

((يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا))

  ((إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ))

 ((Wale wasiomuomba mungu mwengine pamoja na Allaah wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara))   

((Aazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaama, na atadumu humo kwa kufedheheka))  

((Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema.  Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema.  Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-Furqaan: 68-70]

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amhidi kwa kumuwezesha kujiepusha na madhambi ya hatari kama hayo na tunakuombea ndoa ya kudumu, yenye furaha, amani, mapenzi na kuridhiana na mumeo.

 

 Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share