Kuzingua Kwa Kuwekea Nazi Na Kuku Ni Shirk?

 

 SWALI:

Shukran sana kwa juhudi zenu za kuzidi kutuelimisha kwa hili na lile, inshaallah Allah awajaze kila la kheri, awataqabalie swaumu zenu na awasamehe dhambi zenu, 'ameen'.

Kwanza ningependa kuwajulisha kwamba mimi sina elimu kubwa katika dini yetu ya kiislam hususan katika mambo ya zunguo, lakini namshukuru Allah kwa ile aliyonijaaliya nayo.

swali langu ni hili, Je inafaa kuzunguliwa kwa kuwekewa nazi mbele ya miguu na kuku upande wa kulia, kisha hiyo nazi ikavunjwa baada ya zunguo na kutabiriwa kama hasad imeondoka au la? Kuku akachinjwa kama sadaqa. kama ya ruhusiwa tafadhalini nielezeni kwa urefu ni fahamu kwani moyo wangu umekataa kabisa kuwa hii si shirk, na imenisababisha kugombana na waalimu wenye kuzunguwa kwa njia hizi na wametoa sababu kadhaa ambazo bado hazijanifanya kukubali kuwa ni sawa. tafadhali nielimisheni ili nami niwaelimishe wenzangu.

asalam aleykum.  


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu katika Imani na tunakuombea pia wewe Allaah Aliyetukuka Akutakabalie Swawm yako na pia kwa Ummah mzima wa Kiislamu. Pia tunamuomba Aliyetukuka Aturudishie misimu hii ya kheri kila mwaka ili tupate faida zake.

Ama kuhusu swali lako ambalo ulikuwa na shaka ndani yake itoe hiyo shaka na ujaze mahali pake yakini. Zunguo la Kiislamu linafahamika kwa kisomo ambacho kinakubaliana na sheria na matendo yanayokwenda sambamba nayo. Katika zunguo huwa hakuna kuku, nazi wala kitu kingine isipokuwa maji ambayo yanaweza kusomewa. Pia katika zunguo la kisheria huwa hakuna kutabiriwa kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na aliyoteremshiwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza thamani ya mbwa, mapato ya kahaba na mwangaliliaji (mtabiri) [Maalik].

Mwenye kuzungua baada ya kisomo huwa hakuambii chochote bali ikiwa ni hasadi itaondoka na akiwa ni jinni ambaye alikuwa amekuvaa atatolewa kwa kisomo. Kwa hivyo huko kuwekwa nazi na kuku ni amali za kishirikina na wazunguaji kwa maslahi yao wanawafanyia watu wasiojua Dini yao ili wao wawe ni wenye kupata faida.

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

Nitakuwa Nimelogwa? Je, Kutumia Kombe Inafaa?

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share