Bi Harusi Kujipamba Katika Mipaka Ya Sheria

 

Bi Harusi Kujipamba Katika Mipaka Ya Shariy’ah Ya Dini  

 

Alhidaaya.com

 

   

Swali:

 

In Shaa Allaah mutakuwa katika hali ya uzima na malipo mema kwa Allah amin.

 

Swali langu vp biharusi ajipambe kama ilivyokua ktk wake wa Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam  na watoto wake? jee mapambo ya sasa inakubalika katika sharia kama vile mamekap na kupaka piko na utowaji wa halawa (yaani malaika za mwilini)  na ma bleach? Naomba munijibu mapema shukran In Shaa Allaah Allah atawalipa. nami munikumbuke ktk email yangu iwe uepesi kwangu.

  

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika si bi harusi tu ambaye anafaa kujipamba katika mipaka ya Shariy’ah, bali mwanamke ambaye ameolewa na mume ambaye ameoa wanafaa wote kujipamba kwa ajili ya mwenziwe. Mume anafaa ampambie mkewe na mke kumpambia mumewe.

 

Kuhusu pambo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza:

 

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ ۚ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣٢﴾

Sema: “Nani aliyeharamisha mapambo ya Allaah ambayo Amewatolea waja Wake na vilivyo vizuri katika riziki?” Sema: “Hivyo ni kwa ajili ya wale walioamini katika uhai wa dunia; makhsusi (kwa Waumini) Siku ya Qiyaamah. Hivyo ndivyo Tunavyofasili waziwazi Aayaat kwa watu wanaojua.” [Al-A’raaf: 32]

 

Baada ya hayo itakuwa vyema tuangazie mapambo yanayokwenda sawa na Shariy’ah na yale ambayo yanakiuka mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Ama kuhusu vipodozi (make-up) havina tatizo kuvitumia kwa kujipamba ukiwa kwa mumeo au nyumbani kwako na Maharimu zako, ikiwa havitakuwa na madhara. Tunavyofahamu vipodozi hivi vya sasa vinatengenezwa na kemikali. Ikiwa kutapatikana kuwa utumiaji una madhara na mwana Aadam, basi havitakubaliwa na Shariy’ah kutumiwa. Hiyo ni kuwa msingi mkubwa wa Shariy’ah ni Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema:

 

"Haitakiwi kujidhuru wala kudhuriana" [Ibn Maajah na Ad-Daaraqutwniy, nayo ni Hasan]

 

Piko nayo ni aina ya urembo au pambo kama hinna hivyo hakutokuwa na utata wowote kuhusu matumizi yake. Hata hivyo imetambulika kwamba piko huwa ina athari kwa wengine wenye ugonjwa wa hasasiya (allergy - kuwa na mzio) na hivyo kumletea kuvimba kwa mwili na matatizo mengine ya kiafya. Pia zipo piko ambazo zinafanya ugozi kwenye ngozi hivyo kuzuia maji kufika kwenye ngozi wakati wa kutawadha au kuoga josho la janaba. Ikiwa piko kwako ina sifa ya kwanza au ya pili au zote mbili itakuwa haifai kwako kuitumia kwa misingi tuliyoeleza hapo juu.

 

 

Uislamu umetuletea  mambo ya Fitwrah (maumbile ya asli ya Uislam). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituagizia: " Mambo kumi ni katika Fitwrah (maumbile ya asli ya Kiislamu): 'Kupunguza masharubu, kufuga ndevu, kupiga mswaki, kupitisha maji puani (kusafisha), kukata kucha, kusafisha penyo za vidole, kung'ofoa (kunyoa) nywele za kwapa, kunyoa nywele za sehemu za siri, na kujisafisha kwa maji baada ya kujisaidia na msimuliaji akasema kasahau la kumi, lakini inaweza kuwa ni kusafisha mdomo (kusukutua)" [Muslim na Abu Daawuwd kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah  Radhwiya Allaahu 'anhaa].

 

 

Ukiyatizama mambo haya kumi utakuta yafuatayo ni kuweka unadhafa wa mwili, kwa mfano Kupunguza masharubu, kupiga mswaki, kupitisha maji puani (kusafisha), kukata kucha, kusafisha penyo za vidole, kung'ofoa (kunyoa) nywele za kwapa, kunyoa nywele za sehemu za siri, na kujisafisha kwa maji baada ya kujisaidia na lakini inaweza kuwa ni kusafisha mdomo (kusukutua). Hivyo, Muislamu amehimizwa kuweka usafi kwa kuosha viungo kadhaa, kutoa nywele ambazo ndio chanzo cha kuleta uchafu isipokuwa kunyoa ndevu (mwanaume) kumekatazwa kabisa.

 

 

Ama utoaji wa nywele ndogo ndogo ambazo baadhi ya watu huziita malaika hakuna tatizo lolote katika Dini ikiwa ni kwa sababu ya kujiremba au kujiweka katika hali ya usafi kama vile kunyoa nywele za kwapani na sehemu za siri. Ama katazo lililokuja ni kupunguza au kunyoa nyusi kwa dalili ya Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ عَلْقَمَةَ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ، وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، وَالْمُتَنَمِّصَاتِ وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ تَعَالَى، مَالِي لاَ أَلْعَنُ مَنْ لَعَنَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم وَهْوَ فِي كِتَابِ اللَّهِ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ‏ ‏‏.‏

Amesimulia ‘Alqamah (رضي الله عنه): Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: Allaah Amewalaani wenye kuchanja, na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah (سبحانه وتعالى). Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah?:

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

“Na lolote analokupeni Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi jiepusheni.” [Al-Hashr (59:7) Hadiyth amepokea Imaam Al-Bukhaariy Kitabu Cha Mavazi (77)]

 

 

Na katika Hadiyth nyingine tunaongezewa mapambo ambayo hayafai kufanywa na Muislamu. Na imepokewa kwa Asmaa' (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba mwanamke fulani alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

"Ee Rasuli wa Allaah! Binti yangu amepatwa na surua zikapuputika nywele zake, nami nimemuozesha; Je, niziunganishe?" Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: "Allaah Amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwengine kwa nywele nyengine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo )" [Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy].

 

 

Na Hadiyth ya 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) imenukuliwa na al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaa'iy). Na katika riwaayah nyengine:

 

"Mwenye kuunganisha nywele na mwenye kumtaka mwengine amfanyie kazi hiyo (mwenye kutamani kuzivaa nywele hizo za bandia)". Na 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anha) amepokea mfano wake.

 

 

Katika Hadiyth hizi na nyingine zilizo sahihi tunaelezewa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza baadhi ya mapambo nayo ni, kutoa au kuchonga nyusi, kuunga nywele, kuchonga meno kwa urembo, kuchanja kwenye mwili kwa kujichora tattoo. Hivyo ni juu yetu kutahadhari na mapambo hayo kwani kuyafanya huwa tunaingia katika laana ya Allaah ('Azza wa Jalla)  Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

  

إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَّرِيدًا ﴿١١٧﴾لَّعَنَهُ اللَّـهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿١١٨﴾وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ﴿١١٩﴾

Hawaombi badala Yake isipokuwa miungu ya kike na hawaombi isipokuwa shaytwaan muasi.

Allaah Amemlaani. Na (shaytwaan) akasema: "Kwa hakika nitashika katika waja Wako sehemu maalumu. Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah.” Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mwandani badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana. [An-Nisaa: 117-119]

 

Ama kuhusu kutia bleach ili kubadili rangi ya mwili au kwa pambo hilo haliruhusiwi na Uislamu. Sababu ni kuwa huwa unabadilisha umbile alilokuumba nalo Allaah ('Azza wa Jalla)  ambako kumekatazwa kama ilivyo Aayah iliyo juu [An-Nisaa  117 – 119]. Na pia bleach ni mchanganyiko wa makemikali ambayo yana madhara makubwa kwa mwili. Kwa sababu ya hiyo leo tunaona wanawake wenye kumea ndevu na kuwia vigumu kufanyiwa upasuaji kwa sababu ya ngozi ya juu kuathirika na kemikali na madhara mengine mengi.

 

 

Kwa ajili hiyo ni juu yetu kuwakumbusha wenye kutumia wasijitie kwenye maangamivu na hivyo kuhasirika hapa duniani na Kesho Aakhirah.

 

 

Vifuatavyo ni baadhi ya vipodozi vya asli ambavyo vinafaa kutumia na vimeonekana kuwa vinaleta manufaa katika kuiboresha ngozi na nywele za mwanamke:

 

1.    Hinna kwenye nywele.

 

2.   Mchanganyiko wa mafuta ya lozi, nazi na zaytuni.

 

3.   Majani ya mkunazi yaliyosagwa kwa ajili ya kusafishia uso na mwili.

 

4.  Mchanganyiko wa Habba Sawdaa iliyosagwa na mafuta ya zaytuni upake usoni kisha ukae nayo katika jua kwa muda kidogo kisha uoshe.      

 

      

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share