Kuweka Madawa Ya Nywele Na Kuvaa Nywele Za Bandia

 

Kuweka Madawa Ya Nywele Na Kuvaa Nywele Za Bandia

 

Alhidaaya.com 

 

 

SWALI:

 

 

Assalam Aleikum.

 

Wabbad dada yangu anataka kua na ujuzi wa kuwatengeneza wenzake nywele na kama walivyo watengezaji huwa wanatumia baadhi ya madawa ambayo si ya sawa au nama yoyote ile ya kuweka nywele bandia au lengine lolote. je ni yapi muhimu ayazingatie wakati anapofanya kazi hii ili mie ni mnasihi afanye au asifanye. Shukran 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwako kwa kumtakia mwenzio mazuri ya hapa duniani na Kesho Aakhirah. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akujazi na akupatie kila jema na mafanikio katika Nyumba mbili. Hakika ni kuwa, “Dini ni kupeana nasaha.” [Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy].

 

 

Na Jariyr bin Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: "Nilimbai Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kusimamisha Swaalah, kutoa Zakaah na kumnasihi kila Muislamu." [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy].

 

 

Kazi yoyote ambayo Muislamu anaifanya au anataka kuifanya ni lazima atazame kuwa inakwenda sambamba na kanuni za Sharia. Bila hivyo, inakuwa ni haramu kwake kuifanya. Katika mas-ala ya kusema kuwa utumiaji wa madawa ya nywele unaleta madhara kwa mwenye kuwekewa na mwenye kuweka. Ikiwa sifa ya madawa hayo ni hivyo basi itakuwa haifai kisheria kwani msingi wake muhimu: "Haifai kudhuru wala kulipana madhara." [Ibn Maajah na ad-Daaraqutniy].

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ

Wala msijitupe katika maangamizi.. [Al-Baqarah: 195].

 

Na pia,

وَلَا تَقْتُلُوا

Wala msijiue.. [An-Nisaa: 29].

 

 

Hakika ni kuwa madawa haya ya kemikali ya nywele yanaleta madhara makubwa sana na hivyo Uislamu unachunga maslahi ya mwanadamu na hautaki awe ni mwenye kudhurika.

 

 

Ama kuunganisha au kuunganishwa nywele za bandia ni jambo ambalo limekatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imam Abu Zakariyya Yahyaa an-Nawawiy ana mlango haswa kuhusu kuongeza au kuongezwa nywele katika kitabu chake Riyaadh asw-Swaalihiyn. Dalili za hilo ni kama zifuatazo:

Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَّرِيدًا ﴿١١٧﴾لَّعَنَهُ اللَّـهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿١١٨﴾وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ﴿١١٩﴾

Hawaombi badala Yake isipokuwa miungu ya kike na hawaombi isipokuwa shaytwaan muasi.Allaah Amemlaani. Na (shaytwaan) akasema: Kwa hakika nitashika katika waja Wako sehemu maalumu. Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah. Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mwandani badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana. [An-Nisaa 4: 117 – 119].

 

 

Imepokewa kwa Asmaa’ (Radhwiya Allaahuanha) kwamba mwanamke fulani alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ee Rasuli wa Allaah! Binti yangu amepatwa na shurua zikapuputika nywele zake, nami nimemuozesha; Je, niziunganishe?” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Allaah Amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwengine kwa nywele nyengine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo)” [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy].

 

 

Na katika riwaya nyengine: "Mwenye kuunganisha nywele na mwenye kumtaka mwengine amfanyie kazi hiyo (mwenye kutamani kuzivaa nywele hizo za bandia)". Na mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahuanhaa) ameeleza Hadiyth kama hiyo. [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy].

 

 

Pia imepokewa kwa Humayd bin ‘Abdir-Rahmaan kuwa alimsikia Mu‘awiyah (Radhwiya Allaahuanhuma), mwaka wa Hijjah, akiwa juu ya mimbari, akiwa ameshika nywele zilizokatwa katika mikono ya Harasiy (Mtoto wa Amiri), akasema: "Enyi watu wa Madinah! Wako wapi wanazuoni wenu? Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikataza tabia hii (nywele za bandia) na alikuwa akisema: ‘Hakika walihiliki Bani Israili pale wake zao walipoichukua tabia hii (ya kuunganisha nywele)’” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy].

 

 

Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allahuanhumaa) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake na mwenye kutaka mwengine amuunganishe nywele hizo na mchanjaji kwenye mwili na mwenye kuchanjwa. [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].

 

 

Hizi ni dalili za wazi kuhusu hilo uliloliuliza na tunatumai utaweza kumnasihi kwa kumkinaisha dada yetu ili asifanye kazi hiyo ya kuunganisha nywele bandia. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amfanikishe kuacha kazi hiyo na kupatiwa badali iliyo nzuri zaidi.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share