Kusoma Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah na Kuomba Du’aa Baada ya Mihadhara

 

Kusoma Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah na Kuomba Du’aa Baada ya Mihadhara

 

 www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Haikuthibiti kusimiliwa na maswahaba zake Mtume kua alikua akisoma dua kwa pamoja kwa saiti na wao wakiitikia ikiwa baada ya swala lakini leo tuna maimamu wengi wanatoa dua baada ya swala na maamuma wanaitikia na pia ikiwa kwenye mihadhara baada ya kumaliza inatolewa dua waliohudhuria wanaitikia na pia kwenye hutba za siku ya ijumaa.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

In-Shaa-Allaah tutajaribu kuliangazia suala hili kwa njia tofauti ili lipate kueleweka vilivyo.

 

Muislamu ni yule anayemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘alaa) na kumdhukuru kila saa na kila wakati ila akiwa katika sehemu zilizokatazwa kumtaja jina Lake kama chooni.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘alaa) Anatutaka tumuombe Yeye peke Yake pale Aliposema:

 

قَالَ  رَبُّكُمُ  ادْعُونِي  أَسْتَجِبْ  لَكُمْ    

 Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni.  [Ghaafir:60]

 

Tufahamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘alaa) Yupo karibu sana nasi kwa elimu Yake na usikivu na Anatujibu tunayomuomba:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

186. Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka.  [Al-Baqarah:186] 

 

 

Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kumjibu mwenye dhiki na kumuondolea kama Alivyosema:

 

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea ouvu na Akakufanyeni makhalifa wa ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka. [An-Naml: 62]

 

 

Hii ni kuwa Allaah (‘Azza wa Jalla)  Yu karibu sana nasi kwa elimu Yake kuliko mshipa wa shingo:

 

 وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. [Qaaf: 16]

 

Du’aa ina adabu zake ambazo tunafaa kufuata mojawapo ikiwa ni kuwa na unyenyekevu kama Anavyosema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾

  Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka [Al-A’raaf: 55]

 

Pia tumuombe tukiwa na hofu pamoja na matumaini:

 

وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾

  Na wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake; na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika rahmah ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf: 55]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

 

Duaa ni ‘Ibaadah.” [Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibbaan na al-Haakim kutoka kwa an-Nu‘umaan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa].

 

Tunatakiwa tumuombe Rabb wetu kila wakati na hasa wa neema na wakati ambao du’aa inatakabaliwa.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Mwenye kutaka ajibiwe na Allaah wakati wa shida na dhiki azidishe du'aa wakati wa neema” [At-Tirmidhiy na Al-Haakim, naye akaisahihisha na akakubaliana naye Adh-Dhahabiy kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].

 

Du'aa ni silaha kubwa ya Muumini kwani Rasuli wa  Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Du'aa ni silaha ya Muumini, na nguzo ya Dini na ni nuru ya mbingu na ardhi” [Al-Haakim, naye akaisahihisha na akakubaliana naye Adh-Dhahabiy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu)]

 

Ama kuhusu du’aa na utajo baada ya Swalaah matendo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yapo wazi kabisa kuhusu hilo. Utata unaondoka kabisa tunapoangazia hayo. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) anatueleza kuwa alikuwa akijua kumalizika kwa Swalah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa takbiyr aliyokuwa akitoa (Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  [Abuu Daawuwd].

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia mafakiri wa Muhajirina

 

Je, siwafundishi kitu ambacho kwayo mutawafikia waliowatangulia na kushindana na watakaokuja baadaye wala hatakuwa mmoja wenu bora ila atakayefanya kama mnavyofanya?” Wakasema: “Ndio, ee Rasuli wa Allaah?” Akawaambia: “Leteni Tasbiyh mara 33, Takbiyr 33 na Tahmiyd 33” [Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].

 

 

Riwaayah ya Ka‘b bin ‘Ujrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) inatueleza kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

Haimpiti msemaji wake baada ya kila Swalaah ya faradhi: Tasbiyh mara 33, Tahmiyd 33 na Takbiyr 34.” [Muslim, At-Tirmidhiy na An-Nasaa’iy].

 

Na amesema Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Mwenye kusoma Aayatul Kursiy baada ya kila Swalah haitomkataza yeye kuingia Peponi ila mauti.” [An-Nasaaiy]. 

 

Naye Thawbaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapomaliza Swalaah akileta Istighfaar mara tatu na kisha husema:

اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ، وَمِـنْكَ السَّلام، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام

Allahumma Antas Salaam wa Minkas Salaam Tabaarakta ya Dhaal Jalaal wal Ikraam. [Muslim].

 

Utajo wa kishariy'ah baada ya Swalaah ya faradhi kinachowajibisha kuwe kwa njia zilizopokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), sio katika sifa zilizozuliwa zinazofanywa hivi leo. Hapo juu tumeleta baadhi ya Hadiyth lakini kile ambacho mtu anafaa kufanya baada ya Swalaah. Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo bayana:

 

Hadiyth Kuhusu Kuomba Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah Ni Swahiyh Au Dhaifu?

 

Kila mmoja anatakiwa amdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta‘alaa) kwa sauti ya kiasi kivyake. Baada ya adhkaar hizi utamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘alaa) kwa siri kwa unayotaka, japo du'aa sehemu bora zaidi ni pale unaposujudu na mwisho wa tashahhud.  Kuleta du’aa kwa sauti ndogo au siri kuna faida kubwa kwani kufanya hivyo ni karibu zaidi na kuwa na ikhlaasw na unyenyekevu na kuwa mbali na riyaa.

 

Ama yale yanayofanywa na baadhi ya watu katika baadhi ya miji na nchi kwa kuleta du’aa kwa jamaa baada ya Swalaah kwa sauti kubwa au Imaam kuomba na Maamuma kuitikia Aamiyn. Kitendo hiki ni uzushi mbaya kwani haikunukuliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa anapowaswalisha watu akiomba baada ya Swalaah kwa njia hii ['Allaamah Swaalih bin Fawzaan bin ‘Abdallaah Al-Fawzaan, al-Mulakhkhaswu al-Fiqhiy, Mj. 1, uk. 159 – 160].  

 

Amesema Shaykhul Islaam, Ibn Taymiyyah kuhusu hilo la kuleta du’aa za pamoja baada ya Swalaah: “Mwenye kunukuu hayo kutoka kwa Imaam ash-Shaafi‘iy kuwa alipendekeza hilo, hakika amemkosea” (Majmuu‘ al-Fataawaa, Mj. 22, uk. 512).

 

Ama kuhusu du’aa wakati wa khutbah ipo Hadiyth ya ‘Ammaarah bin Ru’aybah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa alimuona Bishr bin Marwaan juu ya minbar akiwa amenyanyua mikono yake (akiomba), akasema: “Allaah Aipotoe mikono hii miwili, hakika nimemuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hazidishi kusema hivi, akaashiria kwa kidole cha shahada” [Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah)]

 

 

Abu Maalik Kamaal bin as-Sayyid Saalim amesema Hadiyth ya hapo juu inatupa faida mbili:

 

1. Dalili ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba katika khutbah zake.

 

2. Ukaraha wa Khatwiyb kunyanyua mikono yake anapoomba akiwa juu ya minbar. Sunnah ni kuashiria kwa kidole cha shahada (Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1, uk. 586).

 

Naye Shaykh Swaalih bin Fawzaan amesema: “Ni Sunnah kwa Khatwiyb kuwaombea Waislamu kwa yenye kutengeneza Dini na dunia yao, kumuombea Imaam wa Waislamu na viongozi wao kwa mambo yao kwa islahi na tawfiki. Du’aa kwa viongozi katika khutbah ni maarufu kwa Waislamu na juu yake amali zao, kwani du’aa kwa viongozi hao ni katika Manhaj ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa‘ah na kuacha kwake ni katika Manhaj ya wazushi. Haifai kwa Maamuma kuitikia Aamiyn kwa du’aa ya Khatwiyb kwa kunyanyua sauti wala mikono yake kwani kufanya hivyo ni haramu kwa itifaki ya wanazuoni.” [Al-Mulakhkhaswu al-Fiqhiy, Mj. 1, uk. 255, 264].

 

Ama suala la du’aa ambazo zinaletwa katika mihadhara inapomalizika ni suala la Ijtihaad za wanazuoni baada ya kuisoma ile du’aa ya kafara ya kikao. Ama du’aa nyingine nyingi zinazotolewa hazijathubutu kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa akitoa du’aa hizo baada ya darsa au muhadhara aliokuwa akiwatolea Maswahaba zake.

Du’aa iliyothibitu ni Kafaaratul-Majlis (kafara ya kikao) inayosema:

 

سُبْحـانَكَ اللّهُـمَّ وَبِحَمدِك، أَشْهَـدُ أَنْ لا إِلهَ إِلاّ أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتوبُ إِلَـيْك

 Subhaanaka-Allaahumma wabihamdika, ash-hadu an laa ilaaha illaa Anta astaghfiruka wa atuwbu Ilayka

 

Utakasifu ni Wako ee Allaah, na Himdi ni Zako. Nashuhudia (kwa kuamini moyoni na kukiri) kwamba Hapana muabudiwa wa haki ila Wewe. Nakuomba Unigfhurie na ninarejea Kwako kutubia.  [Al-Bukhaariy, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Na nyingine ni ile iliyonukiliwa kutoka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa: “Hajapatapo kukaa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kikao, wala kusoma Qur-aan, wala kuswali ila atamaliza na du’aa hii:

 

سُبْحـانَكَ  وَبِحَمدِك، لا إِلهَ إِلاّ أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتوبُ إِلَـيْك

Subhaanaka wa Bihamdika laa ilaaha illa Anta Astaghfiruka wa atuwbu Ilayka

 

Kutakasika ni Kwako, na Himdi ni Zako, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, nakuomba maghfirah na ninarejea kutubia Kwako”.

 

Nilimuuliza kwa nini unasoma du’aa hiyo. Akasema: “Ndio, anayesema kheri amalize kwa kheri, na anayesema shari yanakuwa maneno haya ni kafara kwake” [An-Nasaaiy].

 

Na zipo Hadiyth zenye maana ya kijumla kama mfano:

 

Imepokewa na Ibn Mas‘uwd (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema:

 

Ee Rabb wangu! Nakuomba uniongoze na unipatie taqwa na uniepushe na zinaa na unipe kinaa” [Muslim].

 

Na Anas amesema, duaa aliyokuwa akiiomba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kila wakati ni,

اللهم رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الأَخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

Allaahumma Rabbaana Aatinaa fid dun-ya hasanah, wa fiyl Aakhirati hasanah waqinaa ‘adhaaban Naar

 

Ee Allaah! Rabb wetu tupe mema duniani na tupe mema Aakhirah na tuepushe na Moto” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Kwa ajili ya Hadiyth hizi na nyenginezo wanazuoni wamefanya ijtihadi ya kuwa hapana tatizo kwa kuomba du’aa baada ya muhadhara ingawa kilicho bora cha kufanywa ni kuomba du’aa ya kufunga kikao ambayo ni maarufu kwa Du’aa ya kafara ya kikao ‘Kaffaaratul-Majlis’ ambayo tumeshaitaja juu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share