Ikiwa Amesahau kitendo Au Ametia Shaka Ya Kuzidisha Kitendo Afanye Vipi Sajdatus-Sahw?

 

SWALI:

Ikiwa umesahau kitendo au umepunguza kitendo (sio rakaa kamili) inabidi ufanye "Sijdatus-sahw" kabla ya kutoa Salaam na ikiwa umezidisha utafanya "Sijdatus-sahw baada ya kutoa Salaam; je ikiwa huna uhakika unawasiwasi ya yote mawili kuwa umesahau kitendo fulani katika Swalah au Rakaa na pia unawasisi umezidisha kitendo au rakaa utafanya nini?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na Salaam zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Ukiwa na shaka na huna uhakika kuhusu jambo lilotokea una uko hatihati baina ya mambo mawili huko ndiko kunakojulikana kama ‘Shakk’; na shaka haina uzito wowote kwenye mas-ala ya ibaadah katika mambo matatu;

1.     Kudanganyika, kutokuwa na ukweli wowote, kama vile mnong'ono wa Shetani.

2.     Ni pale mtu anapokuwa na wasiwasi kiasi cha kwamba kila afanyapo ibaadah ya aina yoyote, huandamana na shaka.

3.     Au pale mtu anapojiwa na shaka baada ya kukamilisha kitendo cha ibaadah basi huwa haina uzito wowote, maadamu hana uhakika wa shaka hiyo, basi itampasa atekeleze lile alilonahakika nalo.

Tunaweza kutoa mfano wa mtu ameswali Swalah ya Adhuhuri, na baada ya kuikamilisha Swalah yake akawa na shaka emma ameswali rakaa tatu au nne. Kisha shaka isimjie mpaka awe na uhakika ya kwamba yeye ameswali rakaa tatu tu, na katika hali hii itampasa aikamilishe Swalah yake likimtokea jambo hilo muda mchache baadae, kisha atoe Salaam, asujudu (Sujuud as-Sahw) na hatimae atoe tena Salaam. Hata hivyo, ikiwa hatokumbuka mpaka muda mrefu ukapita, basi itambidi airudie Swalah yote kamili.

 
Zile shaka zisizokuwepo katika hali hizo tatu, basi zitakuwa ni zenye kuhesabiwa. Shaka katika Swalah ni aina mbili:

1.     Katika fahamu zake, jambo moja litakuwa na uzito kuliko jengine, basi atalifuata lile lenye uzito kwake, kisha aikamilishe Swalah yake kulingana na hilo (lenye uzito), kisha atoe Salaam, asujudu (Sujuud as-Sahw) na hatimae atoe tena Salaam. Mfano wake ni iwapo mtu ameswali Swalah ya Adhuhuri na akatia shaka katika rakaa kuwa ni ya pili au ya tatu? lakini iliyo na uzito katika fahamu yake ni kwamba hiyo ni rakaa ya tatu, kwa hivyo ataifanya kuwa ni ya tatu. Basi baada ya kuitekeleza rakaa moja zaidi, atatoa Salaam, asujudu (Sujuud as-Sahw) na hatimae atoe tena Salaam. Ushahidi huu umethibitishwa kwenye Swahiyh mbili na kwengineko kutoka katika Hadiyth ya 'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:((Awapo na shaka mmoja wenu katika Swalah yake, basi ajitahidi kulifikilia lililo sawa na aikamilishe juu ya msingi huwo. Kisha na atoe Salaam atekeleze sijda mbili)) [al-Bukhaariy na Muslim] Hayo ni maneno yalonukuliwa kutoka kwa al-Bukhaariy.

2.     Njia zote mbili za uwezekano hazina uzito katika fahamu yake. Kwa hivyo itambidi alitekeleze lile alilo na hakika nalo, ambalo litakuwa ni lenye uchache miongoni mwa mambo mawili, kisha aikamilishe Swalah yake juu ya msingi huwo, kisha asujudu (Sujuud as-Sahw) kabla ya kutoa Salaam.

Mfano wa hayo ni iwapo mtu ameswali Swalah ya Alasiri na akawa na shaka katika rakaa kuwa ni ya pili au ya tatu na hizo zote zisiwe na uzito wowote katika fahamu yake. Kwa hivyo ataifanya hiyo kuwa ni ya pili, atekeleze tashahhud ya kwanza na rakaa mbili baada ya hapo na kisha asujudu (Sujuud as-Sahw) na hatimae atoe Salaam. Au ikiwa ametia shaka kuwa hiyo aliyomo ni rakaa ya tatu au ya nne, basi aondoshe shaka na ashikilie pale alipo na yakni napo. Ushahidi wa hili umetokana na riwaya ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم : ((إِذَا شَكَّ أَحَدُكُمْ فِي صَلَاتِهِ فَلَمْ يَدْرِ كَمْ صَلَّى ثَلَاثًا أَمْ أَرْبَعًا فَلْيَطْرَحِ الشَّكَّ وَلْيَبْنِ عَلَى مَا اسْتَيْقَنَ ، ثُمَّ يَسْجُدُ سَجْدَتَيْنِ قَبْلَ أَنْ يُسَلِّمَ ، فَإِنْ كَانَ صَلَّى خَمْسًا شَفَعْنَ لَهُ صَلَاتَهُ ، وَإِنْ كَانَ صَلَّى إِتْمَامًا لِأَرْبَعٍ كَانَتَا تَرْغِيمًا لِلشَّيْطَانِ)) أخرجه مسلم



Kutoka kwa  Abu Sa'iydil khudriyy  (Radhia Allaahu 'anhu)  kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika Swalah yake na asijue ameswali (rakaa) ngapi - iwapo ni rakaa tatu au nne, basi na aitupilie mbali shaka na ashikilie (aendelee) pale alipo na hakika napo. Kisha asuduju sajda mbili kabla ya Salaam. Na ikiwa ameswali (rakaa) tano, hiyo itamkamilishia Swalah yake, na ikiwa ameziswali nne kamili, basi utakuwa huwo ni utwevu (tahayuri) kwa Shetani)) [Muslim]

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share