Anamkhalif Imaam Kwa Kusoma Du'aa Ya Qunuwt Wakati Imaam Anasujudu

 

Anamkhalif Imaam Kwa Kusoma Du'aa Ya Qunuwt Wakati Imaam Anasujudu

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Asalamu aleykum warahmatullahi wabarakatu.

 

Mimi msimamo wangu kuhusu kunuti katika swala ya alfajiri ni lazima niisome ima niwe maamuma au imamu, yaani hata kama imamu hakuisoma basi mimi huwa namuhalifu naisoma yeye anapokwenda kusujudu. Je  kwa hali hii nipo sahihi? Na swala yangu inakubaliwa? Na hili mbona ni jambo dogo tu? Naomba ufafanuzi zaidi wa kielimu.

Waslmu aleykum.

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwa jinsi swali lilivyokuja inaonyesha dhahiri kuwa muulizaji anaegemea katika dhehebu la Ki-Shaafi‘iyy katika Fiqh yake. Mbali na hayo inafahamika katika madhehbu zote kuwa Qunuwt si nguzo wala wajibu wa kukamilika na kutimia Swalaah ya Muislamu. Inafahamika kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweka ada ya kusoma Qunuwt katika kila Swalaah ya Alfajiri bali wakati wa matatizo alikuwa anasoma Qunuwt katika Swalaah zote kwa muda fulani.

 

Zipo nyakati ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri lakini haikuwa kila siku. Hata hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituwekea msingi katika Hadiyth yake Swahiyh: “Imaam amewekwa ili afuatwe”. Kwa hiyo, haifai kwa Maamuma kumkhalifu Imaam, kumkhalifu Imaam ni kuharibikiwa na Swalaah yake. Mfano mzuri wa kuonyesha kuwa Qunuwt si wajibu wala ukiikosa hutawajibika hata kuleta Sijdah ya kusahau ni yale yaliyotokea pale Imaam Ash-Shaafi‘iy alipokwenda kuzuru Kufah. Aliombwa Imaam aswalishe Swalaah ya Alfajiri katika Msikiti ambao Imaam Abuu Haniyfah alikuwa akifundisha na kuswali. Maamuma walitarajia kuwa Imaam atashikilia msimamo wake wa kusoma Qunuwt lakini hakusoma wala hakuleta Sijdah ya kusahau, hilo likawastaajabisha wengi. Hivyo, wakamuuliza imekuwaje naye akawajibu: “Je, basi hata nisiheshimu rai ya Imaam mkubwa wa sehemu hii?” Ibara hiyo alikuwa anamaanisha Imaam Abuu Haniyfah aliyezikwa katika mji huo wa Kufah.

 

Hivyo, ndugu yetu ikiwa Imaam hatasoma Qunuwt itabidi umfuate na Swalaah yako itakuwa sahihi kabisa. Na pia kauli yako ya kusema kuwa, “Na hili mbona ni jambo dogo tu”  Inathibitisha kuwa huna wewe haja ya kulazimisha jambo hilo na hali ni suala dogo na lisilohitaji fujo hizo za lazima uisome ukiwa ni Imaam au Maamuma.

 

Kwa hiyo tunakushauri ufuate alivyofanya Imaam wako alipokwenda Kufah na zaidi ya yote ufuate Sunnah za Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilizokamilika na kuacha kung’ang’ania umadhehebu hadi ukakhalifu Sunnah za Nabiy wetu mhashamu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Pia unaweza kupata faida zaidi kwenye viungo vifuatavyo:

 

Kusoma Du'aa Ya Qunuwt Katika Swalaah Ya Alfajiri Ni Sunnah?

 

 

Du'aa za Qunuwt Ziko Ngapi Na Je Lazima Zisomwe Katika Swalaah Ya Alfajiri?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share