SWALI:
swali langu linausu twahara, nauliza kuwa mwanamke kujishika katika nafasi zake za siri simaanishi ndani ni hapa juu utakua umetenguka udhu? lingine
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu kwa muulizaji swali kuhusu mas-ala ya wudhuu. Muulizaji hakutubainishia wazi wazi katika kushika uchi huko alikokutaja.
Kushika sehemu zako za siri kwa matamanio au bila matamanio kuna ikhtilaaf baina ya wanachuoni kutokana na ufahamu wao wa Hadiyth mbalimbali za kukataza na kuruhusu suala hilo. Tunakuwekea hapa dalili hizo na kauli mbalimbali za wanachuoni na hoja zao. Ingawa kauli yenye nguvu zaidi ni kuwa ukishika utupu wako kwa matamanio basi wudhuu utakuwa umevunjika, ama bila matamanio ukajishika kama wakati wa kuoga, kuvaa au vinginevyo basi hakutengui wudhuu na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
Katika sehemu ya pili ya swali lako ni kuwa ni madhambi kwa Muislamu mwanamme au mwanamke kukaa kwenye runinga (TV) na kuanza kuangalia vipindi vya ngono. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametukataza
“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).
Jambo lolote ambalo litakukaribisha na zinaa pia ni zinaa mbali na kuwa madhambi yake ni madogo kuliko kitendo chenyewe. Unapokaa mbele ya TV na kuanza kuangalia vipindi au Video/Dvd/Vcd visivyo na adabu utakuwa una makosa. Ni makosa kwa Muislamu kutazama uchi wa mwenziwe akiwa ni wa jinsiya moja au tofauti. Uchi ulioruhusiwa kutazama ni mume kumtazama mkewe na kinyume chake.
Inatakiwa tujiepushe na mambo ambayo yanaweza kutupeleka karibu na zinaa yenyewe
Na Allaah Anajua zaidi