Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho

 

Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:
 

Assalam aleykum.

 

Napenda kuuliza suali langu kama ifuatavyo?

 

Nimewahi kusikia kama kuchora au kupiga picha ya kiumbe chochote chenye uhai haifai katika uislam na mimi miongoni mwa kazi zangu ni graphic designing ambazo zinahusisha sana picha za watu na wanyama jee kauli hii ina ushahidi na usahihi wowote? Naomba msaada wenu katika suala hili

 

Natanguliza shukrani zangu.

 

 

Jibu:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Swali lako muulizaji lina mas-ala mawili, nayo ni; kuchora picha za viumbe na kupiga picha za viumbe.

 

Kuchora picha za viumbe (vyenye roho):     

 

Imekatazwa jambo hili la kuchora picha za viumbe kutokana na Hadiyth nyingi tunazitaja hapa ambazo zinaelezea ubaya wake, na adhabu yake:

 

Ya kwanza:

 

Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

((كل مصوّر في النار)) مسلم

"Kila mwenye kutengeneza picha atakuwa motoni" [Muslim]

 

Ya pili:

 

عن عائشة رضي الله عنها قالت:  دخل علي رسول الله صلى الله عليه وسلم وقد سترت سهوةً لي بقرام فيه تماثيل، ( وفي رواية: فيه الخيل ذوات الأجنحة )، فلما رآه هتكة، وتلون وجهه، وقال:  (( يا عائشة! أشد الناس عذاباً عند الله يوم القيامة الذين يضاهون بخلق الله))  ( وفي رواية: ((إن أصحاب هذه الصور يعذبون، ويقال لهم: أحيوا ما خلقتم))  ثم قال: ((إن البيت الذي فيه الصور لا تدخله الملائكة ))، قالت: عائشة: فقطعناه فجعلنا منه وسادة أو وسادتين، [فقد رأيته متكئاً على إحداهما وفيها صورة]  ))  البخاري , مسلم و عيرهم

Kutoka kwa Bibi 'Aishah (Radhwiya Allahu 'anhaa) ambaye amesema:"Nilifungua pazia la chumba cha hazina ambalo llikuwa na  picha (katika maelezo mengine: ambalo llikuwa ina picha za farasi wenye mbawa). Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipoliona, alichaninilia mbali na uso wake ukabadilika kuwa mwekundu kisha akasema: ((Ee 'Aishah, watu watakaopewa adhabu kali kabisa mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiza maumbile ya Allaah)) (katika usemi mwingine) ((Hakika wanaochora picha hizi wataadhibiwa na wataambiwa: Tieni uhai vile mlivyoviumba!)). Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea kusema: ((Hakika Malaika hawaingii nyumba ambayo ina picha)). 'Aishah akasema: Tukalikata pazia na tukalitumia kufanyia mto au mito miwili. Nimemuona akiegemea mto mmojawapo uliokuwa na picha. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

Hadiyth nyingine:

 

((حشوت وسادة للنبي صلى الله عليه وسلم فيها تماثيل كأنها نمرقة، فقام بين البابين، وجعل يتغير وجهه، فقلت: ما لنا يا رسول الله؟ [أتوب إلى الله مما أذنبت]، قال: ما بال هذه الوسادة؟ قالت: قلت: وسادة جعلتها لك لتضطجع عليها، قال: أما علمت أن الملائكة لا تدخل بيتاً فيه صورة، وأن من صنع الصور يعذب يوم القيامة، فيقال: أحيوا ما خلقتم؟! وفي رواية: إن أصحاب هذه الصور يعذبون يوم القيامة [قالت: فما دخل حتى أخرجتها]  )) البخاري  

Kutoka kwa Bibi 'Aishah (Radhwiya Allahu 'anhaa) ambaye amesema: "Niliujaza mto (pamba au sufi) wa kuegemea kwa ajili Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao ulikuwa na picha. Alisimama mlangoni na uso wake ukabadilika rangi kwa ghadhabu. Nikasema: Nimefanya nini Ee Rasuli Wa Allaah? Nimetubu kwa Allaah kwa dhambi zozote nilizofanya. Akasema: ((Mto huu una nini?)) Nikasema: Nimueutengeneza kwa ajili yako ili uegemee. Akasema: ((Hukujua kama Malaika hawaingii katika nyumba ambayo ina picha na kwamba anayetengeneza hizi picha ataadhibiwa siku ya Qiyaamah na ataambiwa, vipe uhai ulivyoviumba?)) (Na katika riwaya nyingine) ((Wenye (kuchora) picha hizi wataadhibiwa siku ya Qiyaamah)). Akasema: Hakuingia hadi nilivyouondosha. [Al-Bukhaariy]

 

Kuchora picha za vitu visivyokuwa na uhai:

 

Kutokana na kauli ya 'Ulamaa, wamesema kuwa hakuna dhambi kuchora vitu vya asli (vya kimaumbile) kama miti, bahari, majabali, gari, nyumba n.k.

 

Ama kuhusu kupiga picha kwa kamera ambayo huwa ni picha ya kuakisi (kigezo) cha viumbe vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama vile kupiga picha za watu, Video n.k, 'Ulamaa hawakupendelea jambo hili ila tu kama kuna dharura fulani kama kuhitajika picha kwa ajili pasipoti, au picha za majambazi wanaotafutwa n.k.

 

Kutokana na swali lako, inaonyesha kuwa unachora picha ambazo hazikuruhusiwa, kwa hivyo jitahidi ubadilishe kazi yako ili kujiepusha na dhambi hizo, huku ukimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akuruzuku kazi iliyo bora zaidi kuliko hiyo kwani Yeye Ndiye Mwenye Kumruzuku na Kumjaalia kheri nyingi mja wake anapomtii kama Anavyosema:

 

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا﴿٢﴾وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾

Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani). Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza kusudio Lake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu makadirio. [Atw-Twalaaq: 2-3]

 

Na hapa tunachukua fursa ya kuwanasihi ndugu zetu wanafunzi wanapotaka kusomea kazi kwa ajili ya kipato cha maisha yao, wafikirie kwanza kama kazi hiyo haina kipingamizi katika dini yetu, na kama inayo basi waache na kusomea kazi nyinginezo ambazo ziko nyingi sana kuliko hizo zenye mashaka ya dini yetu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share