Hapati Kuswali Kwa Wakati, Kila Siku Anakidhi Swalaah

 

SWALI:

 

mimi ni mgeni kwenye site hii ila alhamdullillah nashukuru kuwa moja kati ya wanachama ya al hidaaya, swali langu ni kuwa mimi ni mwanafunzi na soma Malaysia, kwa hiyo huwa na kuwa na darasa kwanzia asubuhi mpaka jioni japokuwa huwa napewa mapumziko kutoka saa 6 na nusu mpaka saa nane ila huwa na kuwa cna mahali pakuswali swala ya adhuhur na pia na pokaa na shule ni mbali kwa hiyo cwezi kurudi nyumbani sasa nikirudi saa 10 au saa 11 huwa ndio naiswali hiyo swala ya saa saba halafu na ya la'asr, sasa swali langu ni je swala yangu hiyo ya adhuhur  inakubalika au haifai, na kama haifai naomba mnifafanulie ni kwa nini na pia mniambie makosa yangu.......shukran

wabillahi tawfiq,

 


 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu aliye mwanafunzi nasi tunakuombea kila la kheri katika masomo yako.

 

Swalah yako hiyo ina makosa nawe hufai kuchanganya Swalah hizo mbili. Hilo ulilolieleza si udhuru unaokubalika kisheria. Hakika ni kuwa wewe una fursa nzuri ya kuweza kuswali Swalah ya Adhuhuri bila matatizo. Tufahamu kuwa japokuwa ni bora kwa Muislamu kuswali Swalah zake Msikitini kwa wakati wake lakini kukiwa hakuna budi umepatiwa ruhusa kuswali nyumbani au sehemu nyingine yoyote ile.

 

Huu ndio uzuri wa Uislamu na pia umuhimu wa Swalah kwa wakati wake. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (4: 103).

Kwa kuwa hakuna Msikiti na nyumba iko mbali unaweza kuswali Swalah yako sehemu nyingine yoyote, kwa mfano ofisini, darasani, uwanjani au mahali ambapo una fursa ya kuswali Swalah yako. Hili ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amemnukuu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

Ardhi yote imefanywa kwangu mimi ni twahara na ni Msikiti (sehemu ya mtu kuswali ndani yake)” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

 

Na katika Hadiyth nyingine Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amemnukuu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

Tumefanywa bora kuliko watu wengine katika mambo matatu: Safu zetu zimefanywa katika safu za Malaika, ardhi yote imefanywa kwetu kuwa Msikiti na mchanga wake umefanywa twahara kwetu ikiwa hakuna maji” (Muslim).

 

Waweza kuswali bila matatizo sehemu yoyote ya ulimwengu.

 

Bali wewe unatakiwa uende zaidi ya hapo kwa kujaribu kuzungumza na Waislamu wengine au Muislamu ni peke yako? Ikiwa wapo wengine mnaweza kusaidiana na kwenda kwenye idara ya chuo na mkapeleka madai yenu ambayo hakika ni madai ya haki za msingi kabisa za kibinaadam ili wawapatie sehemu au eneo la kufanyia ibaadah yenu na muweze kujumuika na kuswali pamoja. Ukifanya hivyo utakuwa umepata thawabu nyingi zaidi kwani kila mwenye kuswali utakuwa wewe ni mwenye kupata thawabu. Muislamu hawi mgeni mahali popote pale kwani ana ndugu zake katika Imani. Toa hofu na fanya bidii na Allaah Aliyetukuka Atakupatia tawfiki. 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share