Kuchelewesha Swalaah Ya Alfajiri Mpaka Atakapoamka Kwenda Shule inajuzu?

SWALI:

 

Assalam Aleikum ndungu zangu in islam. swali langu linahusu salah. ninaishi na mtoto wa dada yangu ana miaka kumi na mbili na anaswali ALHAMDULLILAH. Salah ya fajr huku kwetu ni saa tisa na dakika hamsini na sunrise saa kumi na moja na dakika hamsini na moja anawesa kuswali saa kumi na mbili saa ya kuenda shule??? JAZAAKA ALLAH KHEYRAN] ASSLAM ALEIKUM] REHMA YA ALLAH SUBHAANA WATA'ALA EWE JUU YENU NDUGU ZANGU IN ISLAM]


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Swalah na wakati wake. Ni jambo linalofahamika kuwa kila Dini au ideolojia hapa ina kanuni zake ambazo zinafaa kufahamika na kufuatwa na wafuasi wake.

 

Uislamu kama Dini ina kanuni zake ambazo ni za kipekee katika kila nyanja. Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wameweka kanuni na masharti katika kila Ibadah ili iweze kukubaliwa na kupatiwa thawabu. Swalah si tofauti na Ibadah nyingine. Katika masharti ya kukubaliwa Ibadah yoyote ile ni:

 

  1. Kuwa na Ikhlaasw na nia njema.

  2. Kufuata kama ilivyofundishwa au kufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na hasa katika Swalah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:

"Swalini kama mlivyoniona nikiswali" (al-Bukhaariy).

 

Katika sharti la kukubaliwa Swalah ni kuiswali kwa wakati wake makhsusi. Ndio kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Amesema:

"Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu" (4: 103).

 

Na wenye kuitoa katika wakati wake basi wanangojewa na adhabu kali kama Alivyosema Aliyetukuka:

"Basi adhabu itawathubutikia wanaoswali. Ambao wanapuuza Swalah zao" (107: 4 – 5).

 

Hivyo, haifai kabisa kwa Muislamu kuitoa katika wakati wake makhsusi uliowekewa. Swalah ya Alfajiri ni kabla ya kuchomoza jua hivyo hata kama ni saa tisa inabidi umuamshe aswali na azoee hivyo kwani huenda kijana huyo wako amebalighi au karibu kubaleghe. Kumuachia hivyo atazoea na ataona kuwa hakuna tatizo lolote la kuchelewesha Swalah hata kama hakuna udhuru wa kisheria. Malezi ya kumzoeza mtoto njia njema na bora ndio yatakayomuweka yeye katika maadili mema na mazuri.

 

Hatuoni kama itakuwa mashaka makubwa ukimuamsha nusu saa kabla ya hapo, ambayo ni saa kumi na moja na nusu akaswali na kisha akafanya mengine kama kusoma Qur-aan na kujiandaa kwa shule, na kisha akirudi jioni baada ya kula na kuswali akapumzika kidogo.

 

Kwa hiyo tunakunasihi uwe unamzoeza katika mafunzo hayo ili awe mtoto mzuri zaidi. Na kuswaliwa mapema huko inaonekana muko katika masika ya joto ambamo mchana unakuwa mrefu na hatudhani ya kuwa mwaka mzima wakati unakuwa ni huo. Na hata kama utakuwa huo hatuna budi ila kufuata maagizo ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tupate kuongoka duniani na Akhera.

 

Allaah Atamwezesha kijana wako kufanya hilo na zaidi ya hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share