Kubakia Imara (Thabiti) Baada ya Ramadhwaan

 

Kubakia Imara (Thabiti) Baada ya Ramadhwaan

 

Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Ahaadiyth Zinazohusiana na Swawm:

 

Kanuni na Adabu (Za Swawm)

 

Sufyaan bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Ee Nabiy wa Allaah niambie kitu kuhusu Uislaam ambacho hamna yeyote ambaye naweza kuumuliza isipokuwa wewe. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Sema: Namuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na shikilia (kuwa na msimamo juu ya jambo hilo).” [Swahiyh Muslim (38)]

  

Hadiyth hii inathibitisha ya kwamba mja anawajibika baada ya kuwa na imani ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ajiendeleze na ajiimarishe katika kumtii Yeye kwa kutekeleza vitendo vya faradhi na kujiepusha na yaliyokatazwa. Haya yote yanapatikana kwa kufuata njia iliyonyooka, ambayo ni dini imara, bila ya kwenda upande mwengine (wowote ule) ikiwa kulia au kushoto.  

  

Ikiwa Muislamu anaishi maisha yake katika mwezi wa Ramadhwaan huku akifunga siku nzima na akitumia usiku wake katika kuswali na akajizoesha kufanya matendo mema, basi na aendelee kubaki katika utiifu wa kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) saa zote.

 

Hii ndio hali halisi ya mja, kwani Rabb wa miezi yote ni Mmoja na daima huwa ni Mwangalifu na ni mwenye kuwaangalia waja wake saa zote.    

 

Kwa hakika kubaki imara (thaabit) baada ya Ramadhwaan na mtu kurekebisha kauli na vitendo vyake ni ishara kubwa ambayo inaashiria ya kwamba mtu amejipatia faida kutoka katika mwezi wa Ramadhwaan na amefanya jitihada katika utiifu [katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)]. Hayo ni dalili ya kukubaliwa (‘ibaadah) na ni ishara ya mafanikio.

  

Zaidi ya hapo, ‘amali za mja hazifiki mwisho katika mwisho wa mwezi, ambapo mwezi mwengine unaanza, bali ‘amali hizo zinaendelea na kusogea hadi mauti yamfikie. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema.  

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 99]

 

Ikiwa kama funga ya Ramadhwaan imefikia mwisho, basi kwa hakika funga za Sunnah bado zimeamriwa kwa mwaka mzima. Ikiwa kusimama usiku kuswali wakati wa Ramadhwaan kumefikia mwisho, basi (jua) kwamba kwa hakika mwaka mzima wote ni wakati wa kutekeleza Swalah za usiku.

 

Na ikiwa Zakaatul-Fitwr imefikia mwisho, basi (jua kwamba) Zakaah ya wajibu bado ingali ipo na vile vile sadaka ambayo itaendelea kuwapo mwaka mzima. Na vilevile hali hizo zinahusiana pia na kusoma Qur-aan na kuchambua juu ya maana yake (usiache endelea kuisoma baada ya Ramadhwaan) na pia kila tendo jema ambalo linafatutwa, kwani matendo mema yanaweza kufanywa kwa wakati wowote.

 

Katika fadhila nyingi ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewapa waja wake ni kule kuuwawekea aina tofauti za matendo mema na Akawapa njia chungu nzima za kutenda matendo mema. Kwa hiyo, bidii na juhudi za Muislam lazima ziwe zenye kuimarishwa na Muislam lazima aendelee kubaki katika kumtumikia Rabb wake. 

 

Share