Kufanya Zinaa Na Mwanamke Asiye Muislamu Kisha Kumuoa

 

SWALI:

Ndugu zangu wa Alhidaaya.kuingiliana na mwanamke kabla ya kumuoa (mwanamke si mwislamu). Na baadae kumuoa.kwa sababu dini tofauti, harusi ilifanyika kwa hatua za kiserikali (civil ceremony). Vile vile kufanya mapenzi kama mke wa ndoa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan inakubalika hivyo? Ahsante sana. Nategemea kupata uhakika kutoka kwenu. Asalam aleikum ndugu zangu wa Alhidaaya.



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza swali. Tufahamu kuwa zinaa ni zinaa katika Uislamu ikiwa utafanya kitendo hicho na Muislamu au asiyekuwa Muislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32). Na tujue kuwa madhambi anayepata mzinifu ni mamoja bila ya kutazama unayefanya naye.

Inatakiwa awali ya yote kwa kuwa umefanya dhambi tena kubwa urudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa kutubia kwa kitendo hicho kibaya, kujuta, kuweka azma ya kutorudia tena na kufanya amali njema. Muislamu hafai kabisa kumuoa mwanamke mshirikina:

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni” (2: 221).

Muislamu mwanamme anaruhusiwa tu kumuoa mwanamke wa Ahlul Kitaab akiwa ni mtwaharifu wala sio mzinifu: “Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa waliopewa Kitabu kabla yenu, mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba” (5: 5).

Ndoa ya Kiislamu kukubalika inafaa itimize masharti yafuatayo:

  1. Idhini ya walii wa mwanamke.

  2. Bibi Harusi kuridhia ndoa hiyo.

  3. Bibi harusi kupewa mahari yake.

  4. Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

Ndoa za kiserikali zinazofanywa katika nchi zetu za Afrika Mashariki au nchi zisizokuwa za Waislamu kwani kimsingi huwa ni ndoa za Kikristo hivyo kutokubalika kisheria kwa namna hiyo ya ndoa. Hata tungesema inakubalika bado kutakuwa na utata kwani Uislamu umetukataza kuoa wanawake wa Ahlul Kitaab walio wazinifu mpaka mwanzo mwanamke mwenyewe awe ni mwenye kutubia, kujirekebisha, kuwa mwema na kujitenga na mwanamume kwa muda kabla ya kuruhusiwa hilo.

Ndugu yetu, wanawake wa Waisilamu wema na wazuri wapo tele kwa nini tunatafuta wengine ambao watatuletea matatizo katika maisha yetu na Dini yetu?

Ama kufanya mapenzi baina ya mume na mkewe wa halali kisheria inakubalika wakati wa usiku wa Ramadhaan lakini sio wakati wa mchana. Ifahamike kuwa yeyote atakayefanya kitendo cha mapenzi na mkewe mchana wa Ramadhaan inabidi atoe kafara kwa kuacha mtumwa huru, akitoweza afunge miezi miwili mfululizo na akishindwa alishe masikini sitini.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share