Waliofanya Zinaa Wanaweza Kuoana?


SWALI:

 

Walioanza kufanya zinaa kabla ya ndoa, wakitaka kuoana wanaruhusiwa?

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Watu hao wawili wanaruhusiwa kuoana baada ya kukamilisha masharti fulani. Sharti muhimu sana ni kujuta kwa kitendo hicho na kuomba msamaha (tawbah) kwa kufanya hivyo na aazimie kutorudia tena, na lau kungekuwa na dola ya Kiislamu basi angejipeleka ili ahukumiwe, na pia kufanya mambo mazuri kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Mche Allah popote pale ulipo. Na fuatisha baya kwa zuri nalo litalifuta hilo baya” (At-Tirmidhiy kutoka kwa Mu‘adh na Abu Dharr [Radhiya Allaahu ‘anhu] ).

Na baada ya kufanya hivyo hawatakiwi kukaa pamoja na wale wasifanye kitendo hicho mara nyingine. Wanatakiwa wawe mbali kwa muda wa miezi mitatu ili kuhakikisha kama mwanamke ana mimba au hana. Ikiwa ana mimba, mtoto huyo hatokuwa wa mwanamume huyo na wala hawawezi kurithiana. Baada ya muda huo na baada ya kuthibitika kuwa wameshajirudi kwa madhambi yao na kukaonekana mabadiliko ya kitabia baina yao, watu hao wawili wataweza kuoana kwa kufunga ndoa na kufuata masharti ya ndoa katika Uislamu. Allah Anasema:

Mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo ya. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke meharimishwa kwa Waumini” (24: 3).

Tanbihi: Uislamu umefanya ndoa kuwa ni nyepesi kutekelezeka hivyo ni kwa vijana na wasichana wasijipeleke katika mambo ambayo yanaleta matamanio badala yake waoane na hili linapunguza mengi na pia kujiondoa na mengi yaliyo machafu na ya uasherati. Na Mtume ametupatia kinga pale alipowahutubia vijana:

“Enyi kongamano la vijana! Yule mwenye uwezo wa kuoa na afanye hivyo, kwani hilo linamfanya ainamishe macho yake na inahifadhi utupu wake. Ama kwa yule asiyeweza basi afunge, kwani kufanya hivyo ni kinga kwake” (Al-Bukhaariy).

Kwa maelezo zaidi, tafadhali soma majibu yalioko katika viungo vifuatavyo:

Ndoa Ya Waliozini

Wazinifu Waliotubu Wanaweza Kufunga Ndoa Na Waliotakasika

Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

 

Share