Mke Anayefanya Kazi Anatakiwa Atoe Masurufu Ya Nyumba?

 

Mke Anayefanya Kazi Anatakiwa Atoe Masurufu Ya Nyumba?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Navyojua mume ni mtu msimamizi wa nyumba kutosheleza nyumba na mahitaji yake kama kodi, chakula na hali kadhalika je ikiwa mke ana kazi yake basi ana lazima ya kutoa nusu kodi na nusu chakula au vitu hivyo ni wajibu wa mume na mke akiwa atatoa basi mapenzi yake?? Maana natatanika sana kuwa nilazima ulipe!! Kama kuwajibika vile - naomba msaada wenu hapa.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Bila shaka ni jambo linaloeleweka kuwa mume katika Uislamu anahitajika kumtimizia mkewe mahitaji ya msingi kama malazi, chakula, matibabu na mengineo. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Aliyesema:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ

Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. [An-Nisaa: 34].

 

Pia Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa,

 

وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ ۚ 

Na ni juu ya mzazi wa kiume kuwapatia chakula chao na nguo kwa mujibu wa ada. Hailazimishwi nafsi ila kwa iliwezalo. Asidhuriwe mzazi wa kike kwa ajili ya mwanawe, na wala mzazi wa kiume kwa ajili ya mwanawe. [Al-Baqarah: 233].

 

 

Mke na mwanamke kwa ujumla katika Uislamu amepatiwa haki ya kuweza kurithi au kuchuma chumo la halali. Kwa hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿٧﴾

Wanaume wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu. Na wanawake wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu, ikiwa ni kidogo au kingi; ni mgao uliofaridhishwa. [An-Nisaa: 7].

 

 

Amesema tena (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):

 

..لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٣٢﴾

Wanaume wanayo sehemu katika waliyoyachuma, na wanawake wana sehemu katika waliyoyachuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu. [An-Nisaa: 32].

 

 

Baada ya kupatiwa haki mwanamke ya kumiliki mali, hapo hapo amepatiwa uwezo wa kuitumia katika njia za wema kama kutoa Zakaah, sadaka, kusaidia miradi ya Kiislamu na mambo mengineyo. Hata hivyo, hawajibiki kutoa masrufu yoyote ya nyumbani hata akiwa yeye ni tajiri kuliko mumewe ila ikiwa ataridhika mwenyewe kufanya hivyo.

 

 

Ikiwa mke anaona mumewe ni dhaifu katika kipato na ni matatizo kutazama nyumba, mke kama huyo anaweza kumsaidia mumewe katika baadhi ya majukumu naye atapata ujira kwa hilo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa). Tunapata mifano mingi katika maisha ya Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa wanasaidiwa na wake zao waliokuwa na uwezo zaidi wa kifedha. Mmoja wao ni ‘Abdullaah bin Mas‘uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akisaidiwa na mkewe Zaynab (Radhwiya Allaahu ‘anha).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share