Du’aa Gani Ya Kuwaombea Wazazi Waliofariki Zamani?

SWALI  

Assalamu aleikum,

Tunashukuru kwa kutufunza mengi mno ambayo tulikuwa hatuyajui kama kuwatendea wazazi waliofariki. Mimi nilidhani ni kuwaombea dua tu sikujua yote hayo mliyotufunza. Hivyo tunafaidika sana. Swali langu ni kuhusu dua mliyonukuu ya kuwaombea. Je, inafaa kuwaombea hiyo duaa japokuwa mzazi amefariki zamani, au hiyo dua ni wakati pale anapofariki tu anaposaliwa au kuzikwa? Na kama sio, basi dua gani nyingine ya kuwaombea?

Asanteni sana.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du’aa ya kumuombea aliyefariki mzazi au wazazi walioaga dunia. Hakika hiyo du’aa iliyopo hapo ni ile inayosomwa wakati wa kumswalia maiti katika Swalah ya jeneza. Wakati mmemaliza kuzika unaweza kumuombea mzazi wako ili Allaah Aliyetukuka Ampatie thabati ya kuweza kujibu maswali atakayoulizwa na Malaika wawili.

Ama baada ya hapo du’aa ya kuwaombea wazazi imetajwa katika Qur-aan nayo ni kama ifuatayo: “Rabbirhamhumaa kama rabbayaani swaghiyra”. Pia du’aa yoyote ambayo utamuombea basi mzazi wako atakuwa ni mwenye kupata thawabu kama katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyonukuliwa na Imaam Muslim ambayo inazungumzia mambo matatu yatakayomfaa maiti likiwemo hilo na mwana kumuombea mzazi wake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share