Hilaal: Kila Mji Ufuate Mwezi Unapoonekena Kwao Au Mwandamo Wa Kimataifa?

 

Hilaal (Mwandamo Wa Mwezi) Kila Mji Ufuate Mwezi Unapoonekena Kwao

Au Mwandamo Wa Kimataifa?

 

 Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Nimesikia kupitia radio wakisema wanao warka uliosambazwa na mufti wa saudia kwamba kila sehemu wafunge kwa kufata mwez wa sehem zao, vipi hamkubaliani na warka huo kuwepo? Ama hamkubalian na mufti huyo kwa sababu zipi? Ukizingatia hapo ndio mahala patakatifu zaidi?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

 

Fataawa za 'Ulamaa wakati mwingine zinabadilika kwa sababu moja au nyingine ima kwa kupatiwa maelezo yanayotumwa kwao kwa kwa kubadilika mazingira. Uko waraka wake, aliekuwa Mufti wa Saudi Arabia, Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz wa Sha‘abaan 1392 H (sawa na 1971) unaosema: “… lililo bora zaidi katika mas-alah haya ni kuweka wasaa (uhuru wa kuchagua) katika jambo hili, nako ni kujuzisha kuchukuliwa kauli moja yoyote kati ya kauli mbili (ya kufuata mwandamo wa kitaifa au kimataifa), kulingana na vile wanavyoona Wanachuoni wa nchi inayohusika. Nami nasema hii ndiyo kauli ya kati na kati na ndiyo iliyokusanya dalili na kauli za wenye elimu…” (Majallatul Buhuuuth Al-Islaamiyah, na. 22, uk. 335).

 

Kauli hii ya Shaykh haifuatwi wala haitolewi na wenye mrengo mmoja. Baadhi ya nchi  huwa ni tatizo sugu kwani watu wengi ni wenye kufuata dhehebu la Imaam fulani, na hivyo hawataki kukaa na wenziwao wenye muelekeo tofauti ili kujadili hilo kielimu.

 

Tunatambua kuwepo kwa kauli hiyo ya Shaykh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) na tunaiheshimu. 

 

 

Vilevile, kuna baadhi ya Wanachuoni wengine pia wanaoonelea kila mtu afunge na mwezi wa nchi yake au utakaotangazwa na Kiongozi wa Kiislamu wa nchi yake.

 

Kifupi, haya mas-laha yana ikhtilaaf na haipaswi upande mmoja kuwalaumu wengine au kuwabeza.

 

 

Lakini hata hivyo wapo Wanachuoni wengi waliosema kuwa kufuatwe mwandamo wa kimataifa na hiyo ndio kauli ya Jamhuur (Wanachuoni wengi). Msimamo huu ndio muono wa madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, Maalik, na Ahmad bin Hanbal. Wengine wenye msimamo huu ni Ibn Taymiyyah, Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy, Ash-Shawkaaniy, Al-Albaaniy katika moja ya rai zake mbili, Ibn Baaz katika moja ya rai zake mbili, Abuu Maalik Kamaal, Dkt. Ahmad Shaakir, Dkt. Wahbah Az-Zuhayliy, ‘Abdur-Rahman Al-Juzairiy na pia Sayyid Saabiq mwenye Fiqhis-Sunnah, Muhammad bin Hizaam wa Yemen. Na kwa upande wa dalili, rai hii ya kufuata mwezi wa kimataifa ina nguvu zaidi kuliko kufuata mwezi wa kitaifa.

 

Tazama masuala hayo kwenye vitabu vya Fiqh kama Fiqhus Sunnah cha Shaykh Sayyid Saabiq, na Swahiyh Fiqhis Sunnah cha Shaykh Abuu Maalik Kamaal bin Sayyid Saalim, utaona kuwa rai yenye nguvu ni ya kufunga kwa kufuata mwezi wa kimataifa popote utakapoonekana Muislam hutakiwa kufunga.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share