Suwrah Gani Zisomwe Swalaah Ya Alfajiri Na Magharibi? Inafaa Kusoma Suwrah Kubwa Na Ndogo?

 

SWALI:

Swala langu ni kama ifuatavyo, Je ni vipi kusoma surah, ikiwa ndefu au fupi, katika swala ya Maghrib au Swala ya Alfajir. 

Rafiki yangu amenieleze kwamba ni Sunnah kusoma surah ndefu katika rakaa ya mwanzo na kufuata surah fupi katika rakaa ya pili ya swala 

Kwa mfano kama naswali Maghrib nikasoma surah Ikhlas, au sura nyengine fupi katika rakaa ya mwanzo, halafu nikasoma Qara ya mwanzo ya surah Yasin katika rakaa ya pili, Je swala yangu inakidhi, Je nini hukmu yake, kutoka katika hadith na sunnah.

Shukran kwa hilo.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu usomi wa Surah katika Swalah za faradhi. Hilo ni kweli na sivyo alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  

Hata hivyo, tufahamu kuwa si Sunnah kurefusha Swalah ya faradhi anapokuwa Imaam anaswalisha wengine. Sababu ni kuwa miongoni mwa maamuma wapo wazee, wagonjwa na wenye haja (al-Bukhaariy na Muslim) na pia wanawake wanaokuwa na watoto wao, na wale watu vilema na kadhalika. Ikiwa mtu anaswali peke yake basi anaweza kurefusha anavyotaka kama alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hadiyth tunayoipata ni ile ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusoma Suratul Baqarah, an-Nisaa'i na al-'Imraan katika rakaa moja. Na ni Sunnah pia kurefusha rakaa ya kwanza ili kuwapatia fursa waliochelewa kujiunga na Swalah hiyo ya jamaa.

Haipendezi kusoma Suratul Ikhlaasw katika rakaa ya kwanza na Qara moja katika Surah Yaasin katika rakaa pili, hivyo kuifanya rakaa ya pili kuwa ndefu zaidi. Pia inapendekeza kuwa usome Surah kama zilivyo katika Qur-aan yenyewe. Kwa mfano ikiwa unataka kusoma Suratul Ikhlaasw na Yaasin, basi rakaa ya kwanza usome Yaasin na ya pili Ikhlaasw. Ukienda kinyume na hivyo bado Swalah yako itakuwa ni sahihi na huna haja ya kukidhi.

Na alikuwa mkali sana (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Mu'adh bin Jabal (Radhiya Allaahu 'anhu) alipokuwa anarefusha Swalah wakati watu walipolalamika kuwa anawarefushia Swalah wakati akiwaswalisha na kumwambia angeweza kuswalisha kwa kusoma Suratul al-A'laa na Suratush Shams na al-Layl (al-Bukhaariy na Muslim). Lau maamuma watakuwa hawaoni tatizo la kufanywa Swalah ndefu kiasi basi wakati huo kutakuwa hakuna tatizo. Hata hivyo, kusema Swalah inaweza kufanywa fupi haimaanishi kuwa basi usitekeleze nguzo zake. Inatakiwa utimize nguzo zake zote na uswali kwa utulivu na khushuu ya hali ya juu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share