Kuomba Du'aa Baada Ya Swalaah Na Kunyanyua Mikono Inajuzu?

Kuomba Duaa Baada Ya Swalaah Na Kunyanyua Mikono Inajuzu?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

 

Assalam Alleykum je ni sahihi kujiombea dua peke baada ya Swala Kwa kunyanyua mikono juu

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Suala la kuomba du’aa baada ya Swalaah linahitaji ufafanuzi.

 

Kuna suala kuomba du’aa ya pamoja baada ya Swalaah ya fardhi, Imaam anaomba na Maamuma wanaitikia. Au Maamuma anaomba du’aa mwenyewe mara baada ya Swalaah. Na kunyanyua mikono wakati huo wa du’aa. Na vilevile kupangusa uso baada ya du’aa.

 

Yote hayo hayana ushahidi wala hayajapokelewa kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuyafundisha au kuyatenda hayo yeye mwenyewe.

 

Kuna ufafanuzi zaidi ya masuala hayo kwenye majibu yaliyo ndani ya kiungo chini kabisa ya maelezo haya.

 

Ama kwenye baada ya Swalaah za Sunnah, ‘Ulamaa wanaonelea mtu anaweza kujiombea du’aa. Hata hivyo, wanasema anaweza kujisomea baadhi ya Swalaah na isiwe ni ada kila siku kwa sababu ni jambo ambalo vilevile halina dalili.

 

Pamoja na maoni hayo ya ‘Ulamaa, lakini usahihi na salama na sehemu sahihi ambayo imethibiti kwa dalili nyingi na za wazi, ni mtu kuomba du’aa ndani ya Swalaah. Na sehemu bora kabisa iliyotajwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuomba du’aa ni wakati wa kusujudu ambapo amesema:

“Karibu kabisa anapokuwa mmoja wen una Mola wake ni wakati anaposujudu. Kwa hiyo, omba du’aa kwa wingi wakati huo.” [Muslim]

 

Na sehemu nyingine ambayo mtu anaweza kuomba du’aa aitakayo, ni pale kwenye At-Tashahhud kabla hajatoa Salaam. Ataomba kwanza kinga ya mambo manne kama ilivyofundishwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); kinga ya adhabu ya Jahannam, kinga ya adhabu ya kaburi, kinga ya mitihani ya Uhai na Mauti na kinga ya shari ya Masiyhud-Dajjaal. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kisha baada ya hapo ataomba duaa anayoitaka ya kuomba mema/mazuri ya dunia na Aakhirah. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ikiwa mtu atafuata mafundisho hayo na atatumia fursa hiyo kama dalili zilivyoonyesha hapo juu kwa mafunzo hayo yaliyothibiti, basi mtu hatosumbuka tena kutafuta wakati mwengine ambao haujafundishwa kutenga muda kwa ajili ya jambo hilo.

 

 

Kwa faida zaidi, bonyeza kiungo hiki hapa chini usome yaliyomo:

 

Hadiyth Kuhusu Kuomba Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah Ni Swahiyh Au Dhaifu?

Kuomba Duaa Pamoja Baada Ya Swalah Na Kunyanyua Mikono Sunnah Au Bid-ah?

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi

 

 

Share