Tafsiri ya Aayah Mbili Za Mwanzo Za Suratut Twalaaq Kuhusu Talaka

 

SWALI:

 

Natoa shukran nyingi sana kwa kutumia wakati wenu kujaribu kujibu swali langu, na shukran kwa kunifahamisha kuhusu kutofupisha majina ya Allaah (Subhana wata'ala) na mtume wetu Muhammad (swala Llahu a'alahi wa salam) InshaAllah nitakuwa nikifanya hivyo. Hakika swali langu ilikua nikiuliza kuhusu maana ya aya ya 1 na ya 2 katika sura ya Talaq. Kuna ubishani baina ya mume na mke, mume amemuacha mkewe kwa kumuandikia talaka, halafu anadai talaka haikuswihi kwa sababu ya aya hizo mbili za sura Talaq. Na mke amemuamini aliposoma tafsiri ya aya hizo mbili kua talaka haikupita. Tafadhali ndugu yangu Muislam nifafanulie talaq kutumia aya hizi mbili ili tufate yalio sawa. Anadai mume ikiwa utaratibu huo anaosema Allaah (Subhana wa Ta'ala) kumwambia kipenzi chake Muhammad (swala Llahu a'alahi wa salam) haukufatwa basi hakuna talaka, ndio nikatoa mfano wa swala haiswihi bila udhu na mengineo. InshaAllah umenifahamu kwa sasa tatizo langu nini. Nawatakia kula la kheir duniani na kiama kwa kutuelimisha kwani mnatupa faida kubwa sana. Jazaka Llaahu khairan.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako ambalo unadhania kuwa hatukulielewa vyema. Hata hivyo, tunawanasihi ndugu zetu katika Imani kuwa waandike maswali yao kwa njia yenye kueleweka ili iondoe tashwishi kwa mwenye kujibu naye ajibu kwa njia iliyo sawa kabisa.

 

Kabla hatujalijibu swali lako hilo ni vyema tulete tafsiri ya Aayah hizo ili ziwe wazi kwa kila msomaji kuhusu mazungumzo yetu haya. Allaah Aliyetukuka Anasema: Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allaah, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allaah, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Allaah Ataleta jambo jengine baada ya haya. Basi wanapofikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah. Hivyo ndivyo Anavyoagizwa anayemuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea” (65: 1- 2).

 

Tufahamu kuwa Aayah hizi ziliteremshwa kama anavyotueleza Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaliki mkewe Hafswah. Hafswah alirudi nyumbani kwa watu wake, Allaah Aliyetukuka Akateremsha: Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao”. Akaambiwa: Mrudie, kwani yeye ni mwenye kufunga sana na kuswali sana Swalah za usiku, naye ni miongoni mwa wakezo na wanawake wako Peponi (Tafsiyr Ibn Kathiir).

 

Pale ambapo tunapopataka sisi ni katika sehemu ya Aayah ya pili ambayo tumeipiga msitari: Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu”. Mara kadhaa mwanadamu na hasa Muislamu hufanya makosa katika jambo lakini badala ya kukiri hilo hutafuta vipengele vya kuweza kujitoa katika tatizo. Mfano ni hili suala ambalo aliyetoa talaka amelitumia bila ya kuuliza maana yake halisi.

 

Maimamu wanne wa Kiislamu walio mashuhuri (Abu Haniyfah, Maalik, Shaafi‘iy na Ahmad bin Hanbal) wamekubaliana kuwa kuwepo kwa mashahidi wawili – wenye sifa ya uadilifu, msimamo mzuri wa kidini, wanaoaminiwa kwa Dini yao na amana yao wakati wa talaka na kurudiana baada ya talaka si sharti kwa usahihi wa vitendo hivyo. Kiasi kwamba lau hakuna mashahidi, basi talaka na kurudiana hakusihi kisheria. Hata hivyo, sharti hii imewekwa na kuhimizwa ili pande mbili hizo hazitaruka na kukataa baadaye kuhusu hakika hiyo na kama kutakuwa na mzozano au mabishano kuhusu suala hilo, jambo hilo litasuluhishwa kwa wepesi na tashwishi yoyote na shaka kuondoka.

 

Amri hii ni kama lile agizo la Allaah Aliyetukuka: Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi (2: 282). Hii haimanishi kuwa ni lazima kuwa na mashahidi katika mahusiano na muamala wa kibiashara na ikiwa hakuna mashahidi, mauzo na makubaliano hayo yatakuwa batili. Hata hivyo, hili ni agizo la busara na zuri lililotolewa kuepusha malumbano na ni vyema kulifuata. Hivyo hivyo, katika mas-ala ya talaka na kurudiana, japokuwa matendo ya mtu yatakuwa sahihi kisheria hata bila mashahidi, ni vyema kuchukua tahadhari kuona chochote kinachofanywa, kinashuhudiwa ili kuondoa malalamishi baadaye.

 

Kulingana na hayo na kuhusu Aayah hizo ni kuwa talaka imepita na kule kumchukua tena na kurudiana kunachukuliwa hivyo, yaani kwa sasa hao ni mume na mke baada ya kurudiana. Hata hivyo, ikiwa hiyo ni talaka ya tatu iliyotolewa watakuwa wameachana mpaka mke aolewe na mtu mwingine wakutane kimwili kisha amuache kwa kawaida kabla ya hao wawili kuweza kurudiana tena. Katika mas-ala ya talaka hakuna mzaha.

 

Tunatumai kuwa utafahamu hivi sasa inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share