006-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kuelekea Ka'abah Na Kusimama Kwenye Swalah

 

KUELEKEA QIBLAH

 

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa anasimama kuswali Swalah zote za Fardhi na za Sunnah alikuwa anaelekea upande wa Ka'abah[1]

 

Naye Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliliamrisha hilo kwa kumwambia "mtu aliyeswali vibaya”[2]: ((Unaposimama kuswali, fanya wudhuu sawasawa, kisha elekea Qiblah na upige Takbiyr))[3].

 

"Wakati yuko safarini, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali Swalah za Sunnah na Swalah ya Witr na huku amepanda mnyama popote alipoelekea. (Mashariki au Magharibi)[4]

 

 

Hilo ni kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

 فَأَيْنَمَا تُوَلُّواْ فَثَمَّ وَجْهُ ٱللَّهِ  ... 

((Basi kokote mnakoelekea, huko kuna wajihi wa Allaah))

[Al-Baqarah: 115]

 

Kauli hii inahusiana na Hadiyth hiyo[5] .

 

“Wakati mwengine alipokuwa anataka kuswali Swalah zisizo za fardhi juu ya ngamia wake, alikuwa akimwelekeza Qiblah, kisha akisema Takbiyr na akiswali kuelekea popote kule msafara unapoelekea.”[6].

 

"Alikuwa akifanya rukuu na sujuud huku amempanda mnyama kwa kuinamisha kichwa chake, na akiinamisha kichwa zaidi chini katika sujuud kuliko alivyoinamisha katika rukuu.”[7]

 

"Alipotaka kuswali Swalah za fardhi alikuwa akiteremka kutoka kwa mnyama na akielekea Qiblah.”[8]

 

Ama katika Swalah ya mtaharuki wa vita vilivyopamba moto, Mtume  (صلى الله عليه وآله وسلم) aliweka kwa ummah wake kanuni ya kuswali "wakiwa wamesimama na kutembea kwa miguu yao, au wakiwa wamepanda mnyama, wakielekea Qiblah au kutokuelekea”[9]. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)  akasema: ((Wanapokutana majeshi Swalah ni Takbiyr na kuashiria kwa kichwa))[10]

 

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)  pia alikuwa akisema ((Kilichokuweko baina ya Mashariki na Magharibi ni Qiblah))[11]

 

Jaabir (رضي الله عنه) amesema,

"Mara moja tulikuwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)  katika msafara au kikosi cha jeshi, na kulikuwa na mawingu, tukajaribu kutafuta Qiblah lakini tulikhtilafiana, kwa hiyo kila mmoja wetu akaswali kuelekea upande tofauti na kila mmoja wetu alichora mstari mbele yake ili kuweka alama mahali pake. Ilipofikia asubuhi, tukazitazama tukaona kwamba hatukuswali kuelekea Qiblah. Kwa hiyo tukamuelezea Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)  lakini hakutuamrisha tuirudie (Swalah) na akasema:

((Swalah yenu imetosheleza)).[12]

 

Mtume  (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali kuelekea Bayt Al-Maqdis (na Ka'abah ikiwa mbele yake) kabla ya kuteremshwa Aayah ifuatayo:

 

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي ٱلسَّمَاء فَلَنُوَلّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلّ وَجْهَكَ شَطْرَ ٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ ...

((Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza kwenye Qiblah ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo…)) [Al-Baqarah, 2: 144]

 

Ilipoteremshwa Aayah hii alielekeza uso wake Ka'abah.  Walikuwa watu katika msikiti wa Qubaa' wakiswali Swalah ya Alfajiri, alipokwenda mtu kuwaambia "Hakika Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameteremshiwa Aayah jana usiku na ameamrishwa kuelekeza uso wake Ka'bah. Basi jueni na elekeeni huko". Nyuso zao zilikuwa zimeelekea Shaam kwa hiyo wakageuka (na Imaam wao akageuza uso kuelekea Qiblah pamoja nao).[13]

 

 

 

KUSIMAMA KATIKA SWALAH

 

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali kwa kusimama katika Swalah zote mbili za fardhi na za Sunnah kwa kufuata maamrisho ya Allaah 

 

وَقُومُواْ لِلَّهِ قَـٰنِتِينَ  

((…na simameni kwa ajili ya Allaah nanyi ni kuqunuti (kunyenyekea)) [Al-Baqarah, 2: 238]

 

 

Ama katika safari alikuwa akiswali Swalah za Sunnah na huku amempanda (mnyama).

 

Ameweka kanuni kwa ummah wake kuswali wakati wa khofu kubwa kwa kusimama juu ya mnyama. Na hili ni kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

حَـٰفِظُواْ عَلَى ٱلصَّلَوٰتِ وٱلصَّلَوٰةِ ٱلْوُسْطَىٰ وَقُومُواْ لِلَّهِ قَـٰنِتِينَ   فَإنْ خِفْتُمْ فَرِجَالاً أَوْ رُكْبَانًا فَإِذَا أَمِنتُمْ فَٱذْكُرُواْ ٱللَّهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُواْ تَعْلَمُونَ 

 

 ((Zilindeni Swalah, na khasa Swalah ya katikati,[14] na simameni kwa ajili ya Allaah nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea))) 

 

 ((Ikiwa mnakhofu (Swalini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Allaah kama Alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamyajui)) [Al-Baqarah, 2: 238-239]

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali kwa kukaa wakati alipokuwa akiumwa hata akafariki[15]. Vile vile aliswali kwa kukaa kwa mara nyingine kabla ya hivyo wakati alipojeruhiwa, na watu waliokuwa nyuma yake waliswali kwa kusimama, akawaashiria wakae nao, wakakaa (na kuswali).  Alipomaliza, akasema, Mlikuwa mnataka kufanya kama wanavyofanya wa-Fursi na Warumi wanavyofanya, wanawasimamia wafalme wao waliokuwa wanakaa. Kwa hiyo msifanye hivyo tena, kwani Imaam ni kwa ajili ya kumfuata, anapofanya rukuu fanyeni rukuu, anaposimama simameni, anaposwali kwa kukaa na nyinyi swalini kwa kukaa (nyote).[16]

 

 

[1] Jambo hili halina shaka yoyote kutokana na mlolongo wa umashuhuri wake (tawaatur). Kwa hiyo, halihitaji maelezo zaidi ingawa baadhi ya dalili zitafuata.

 

[2] Tazama Kiambatisho 3.

 

[3] Imekusanywa na Al-Bukhaariy, Muslim na Siraaj.

 

[4] Imekusanywa na Al-Bukhaariy, Muslim na Siraaj. Takhriyj yake imetolewa katika “Irwa'a Al-Ghaliyl” (289 na 588).

 

[5] Muslim. At-Tirmidhiy amekiri kuwa ni Hadiythi Swahiyh.

 

[6]Abu Daawuud na Ibn Hibbaan katika “Ath-Thiqaat” (1/12) na Adh-Dhiyaa  katika “Al-Mukhtaarah” ikiwa na sanad hasan. Ibn As-Sukn amekiri kuwa ni Swahiyh na pia Ibn al-Mulaqqin katika “Khulaaswat Al-Badr Al-Muniyr” (22/1) na kabla yao, ‘Abdul-Haqq Al-Ishbiyli katika “Ahkaamuh” (Namba 1394 kwa uhakiki wangu). Ahmad ameitumia kama ni uthibitisho kama alivyoripoti Ibn Haani kutoka kwake katika “Masaailuh” (1/67).

 

[7] Ahmad na At-Tirmidhiy ambao wamekiri kuwa ni Swahiyh.

 

[8] Al-Bukhaariy na Muslim.

 

[9] Al-Bukhaariy na Muslim.

 

[10] Al-Bayhaqiy na Sanad inayoelekeana na mahitajio ya Al-Bukhaariy na Muslim.

 

[11] At-Tirmidhiy na Haakim wamekiri kuwa ni Swahiyh. Nimeitowa katika “Irwaa  Al-Ghaliyl fiy takhriyj Ahaadiyth manaar As-Sabiyl” (292).  Uchapisho wake Allaah (سبحانه وتعالى ) Ameufanya wepesi.

 

[12] Ad-Daara Qutniy, Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na At-Twabaraaniy.  Imetolewa katika “Al-Irwaa” (296).

 

[13] Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad, As-Siraaj, At-Twabaraaniy (3/108/2) na Ibn Sa'ad (1/243).  Pia iko katika “Al-Irwaa” (290).

 

[14] Yaani Swalah ya 'Alasiri kutokana na usemi ulio Swahiyhi wa Maulamaa wengi. Miongoni mwao ni Abu Haniyfah na wanafunzi wake wawili.   Kuna Hadiyth kuhusu kauli hii ambayo Ibn Kathiyr ameiweka katika Tafsiyr yake ya Qur-aan.

 

[15] At-Tirmidhiy ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh na Ahmad.

 

[16] Muslim na Al-Bukhaariy na imetolewa katika kitabu changu Irwaa' Al-Ghaliyl katika Hadiyth 394.

 

Share