007-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Swalah Ya Mgonjwa Na Swalah Ya Kwenye Meli

 

SWALAH YA MGONJWA KATIKA HALI YA KUKAA

 

'Imraan bin Huswayn (رضي الله عنه) alisema: "Nilikuwa naumwa ugonjwa wa bawasili (futuru), nikamuuliza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) naye akasema:

((Swali kwa kusimama, ikiwa huwezi, swali kwa kukaa, ikiwa huwezi swali kwa kulala ubavu))”. [1]

 

'Imraan bin Huswayn pia amesema, "Nilimuuliza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Swalah ya mtu anayeswali kwa kukaa, akasema:

((Anayeswali kwa kusimama ni bora, na anayeswali kwa kukaa, thawabu zake ni nusu ya anayeswali kwa kusimama, na anayeswali  kwa kulala (na katika riwaya nyingine kwa kulala chali), basi atapata thawabu nusu ya yule mwenye kuswali kwa kukaa)).[2]

 

Makusudio hapa ni mtu mgonjwa, kwani Anas amesema: "Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alitoka mbele ya watu waliokuwa wakiswali kwa kukaa kwa sababu ya ugonjwa, akasema:

((Hakika Swalah ya mwenye kukaa ni (sawa) na nusu ya Swalah ya mwenye kuswali kwa kusimama)).[3]

 

Siku moja Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimtembelea mgonjwa na akamuona anaswali (huku ameegemea) juu ya mto. Akauchukua na akautupa (pembeni). Kisha mgonjwa akachukua kipande cha mti ili akiegemee katika Swalah yake. (Mtume) akakichukua akakitupa (pembeni) na akasema:

((Swali juu ya ardhi ukiweza, na kama huwezi, basi fanya harakaati kwa kichwa chako kwa kufanya sujuud iwe ya kuinama chini zaidi ya rukuu)).[4]

 

 

 

SWALAH YA KWENYE MELI (CHOMBO CHA BAHARINI)

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliulizwa kuhusu Swalah katika meli, akasema:   ((Swali ukiwa umesimama ila ukiogopa kuzama)).[5]

 

Alipokuwa mzee mtu mzima, alijiwekea kiguzo katika sehemu ya kuswali ili kukiegemea.[6]

 

 


 


 

[1] Al-Bukhaariy, Abu Daawuud na Ahmad.

 

[2] Al-Bukhaariy, Abu Daawuud na Ahmad. Al-Khatwaabiy amesema: "Makusudio ya Hadiyth ya 'Imraan ni mgonjwa wa kukisiwa anayeweza kuchechemea na kusimama kwa tabu, na kwa hivyo, thawabu za mwenye kukaa zimefanywa nusu ya mwenye kusimama kwa ajili ya kumpa msukumo asimame ingawa inajuzu kwake kukaa.” Al-Haafidhw Ibn Hajr amesema katika Fat-h Al-Baariy (2/468): “Nayo ni makisio yenye kukubalika.”

 

[3] Ahmad na Ibn Maajah kwa sanad Swahiyh.

 

[4] At-Twabaraaniy, Al-Bazzaar, Ibn As-Samaak katika “Hadiythih” (2/67) na Al-Bayhaaqiy. Sanad yake ni Swahiyh kama nilivyoeleza katika Silisilah Al-Ahaadiyth As-Swahiyhah (323).

 

[5]  Al -Bazzaar (68), Ad-Daaraqutniy na Abdul-Ghaaniy Al-Maqdisi katika “As-Sunan” (2/82). Na Al-Haakim amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy ameikubali.

 

[6] Abu Daawuud na Al-Haakim ambao wamekiri kuwa ni Swahiyh kama alivyokiri Adh-Dhahabiy. Nimeiweka katika “As-Swahiyhah” (319) na “Al-Irwaa” (383).

 

Share