009-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Swalah Kwa Kuvaa Viatu Na Swalah Juu Ya Minbar

 

 

SWALAH KWA KUVAA VIATU NA MAAMRISHO YA KUFANYA HIVYO

 

"Alikuwa akisimama (katika Swalah) bila ya viatu wakati mwingine na kuvaa viatu wakati mwingine"[1]

 

Ameruhusu kufanya hivyo kwa Ummah wake na kusema:

((Mmoja wenu anaposwali, basi avae viatu vyake au avivue baina ya miguu yake, na wala asimkere mtu kwa viatu hivyo)).[2]

 

Aliwasisitizia kuswali na viatu wakati mwingine, na kusema:

((Kuweni tofauti na Mayahudi, kwani wao hawaswali na viatu vyao wala na khufu [soksi za ngozi] zao)).[3]

 

Mara moja moja alikuwa anavivua wakati anaswali na kisha akiendelea na Swalah yake kama alivyosema Abu Sa'iyd Al-Khudriy:

 

"Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha siku moja, na alipokuwa yumo katika Swalah, alivua viatu vyake na akaviweka upande wa kushoto kwake. Watu walipoona hivyo, nao pia wakavua viatu vyao.  Alipomaliza kuswali alisema: ((Kwa nini mmevua viatu vyenu?)) Wakajibu: "Tumekuona wewe unavua viatu vyako  na sisi pia ndio tukavua viatu vyetu". Akasema:

((Hakika Jibriyl alinijia na kunijulisha kwamba kulikuwa na uchafu)) au kasema (kulikuwa na) kitu cha madhara)).  Katika riwaya nyingine ((uchafu/ Najsi)) katika viatu vyangu, kwa hiyo nikavivua. Kwa hivyo, mmoja wenu anapokuja msikitini, basi atazame viatu vyake. Akiona vina uchafu, au kasema kitu chenye madhara, na (katika riwaya nyingine) najsi, basi avifute kisha aswali navyo)).[4]

 

"Alipokuwa akivivua, alikuwa akiviweka upande wa kushoto kwake.”[5]

 

Na pia alikuwa akisema: ((Mmoja wenu anaposwali, asiweke viatu vyake upande wa kulia wala kushoto kwake, ambako vitakuwa katika upande wa kulia wa mwenzake, isipokuwa kama kutakuwa hakuna mtu upande wa kushoto, lakini aviweke baina ya miguu yake)).[6]

 

 

 

SWALAH KATIKA MINBAR

 

Mara moja Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali katika Minbar (na katika riwaya nyingine: iliyokuwa na daraja (vijingazi) tatu[7]). Hivyo (akasimama juu yake na akapiga Takbiyr (akasema 'Allaahu Akbar') na watu nyuma yake wakapiga Takbiyr wakati yuko juu ya Minbar), (kisha akarukuu juu ya Minbar), halafu akainuka na kushuka kinyume nyume mpaka akasujudu katika kitako cha Minbar. Kisha akarudi (na akafanya kama alivyofanya katika raka'ah ya mwanzo) mpaka akamaliza Swalah yake. Kisha akageuka kwa watu na kusema: ((Enyi watu! Nimefanya hivyo ili mnifuate na mjifunze Swalah yangu))[8].

 

 



 

[1] Abu Daawuud na Ibn Maajah. Ni Hadiyth yenye mapokezi mengi (Mutawaatir) kama alivyotaja  atw-Twahaawiy.

 

[2] Abu Daawuud na Bazzaar (53, Az-Zawa'id), al-Haakim amekiri kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy amekubali.

 

[3] Abu Daawuud na Bazzaar.

 

[4] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah na al-Haakim ambao wamekiri kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy na an-Nawawiy wamekubali. Ya kwanza imetolewa katika Irwaa.

 

[5] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah na al-Haakim.

 

[6] Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ibn Khuzaymah (1/110/2) na kwa Sanadi iliyo Swahiyh.

 

[7] Hii ni Sunnah kuhusu Minbar, kwamba iwe na daraja tatu, na sio zaidi. Kuwa na zaidi ya daraja tatu ni bid'ah iliyoanzishwa na Bani Umayyah. Ni mara nyingi safu hukatika. Na kuliepuka hilo kwa kuiweka pembezoni mwa upande wa Magharibi wa Msikiti au wa Mihraab, ni bid'ah nyingine. Vile vile ni (bid’ah) kuipandisha katika ukuta wa kusini kama roshani ambako mtu hupanda kwa ngazi zilizoshikanishwa na ukuta! Na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم) ). Tazama Fat-h Al-Baariy (2/331).

 

[8] Al-Bukhaariy na Muslim. Riwaya nyingine ni yake Muslim na Ibn Sa'd (1/253).  Imetolewa katika “Al-Irwaa” (545).

 

Share